January 7, 2015


Benchi limetajwa ndiyo chanzo cha beki wa kati wa Simba Mganda, Joseph Owino kuchukua maamuzi ya kurudi kwao na kuiacha timu hiyo inayoendelea na michuano ya Kombe la Mapinduzi.


Beki huyo, hivi karibuni alirejea nyumbani kwao Uganda mara baada ya kumalizika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar iliyomalizika kwa Simba kufungwa bao 1-0 huku Owino akianzia benchi.

Wakati hali hiyo ikiendelea, zipo tetesi kuwa beki huyo aliyebakisha miezi sita kwenye mkataba wake, amepangwa kuondolewa kwenye usajili wa msimu ujao wa ligi kuu ili nafasi yake ichukuliwe na Mkenya, Paul Kiongera ambaye anaendelea na matibabu.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka kwa rafiki wa karibu wa beki huyo, Owino hana matatizo yoyote ya kifamilia yaliyomsababishia arejee kwao zaidi kukerwa na kitendo cha yeye kuwekwa benchi.

Chanzo hicho kilisema, beki huyo alianza kushtukia kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga iliyochezwa Uwanja wa Taifa na mechi kumalizika kwa Simba kushinda mabao 2-0 ambayo alianzia benchi lakini baadaye akaingia.

 “Ugumu wa namba kwa Owino ulianza baada ya timu hiyo kumsajili Musheed (Juko) katika usajili wa dirisha dogo kwa ajili ya kukiboresha kikosi hicho.

“Wakati anasajiliwa beki huyo, Owino alijua kwamba yeye watacheza pamoja, lakini baadaye mambo yakabadilika na nafasi yake kupangwa Isihaka (Hassani).

“Kwa mujibu wa Owino, yeye alikuwa ameshtukia kuwepo na mipango kutoka kwa mmoja wa viongozi wa juu wa timu hiyo ambaye yeye hamtaki Owino, hivyo akaona ni vyema aondoke zake ili awapishe mabeki hao waendelee kuichezea Simba,”kilisema chanzo hicho.

Alipoulizwa Katibu Mkuu wa timu hiyo, Stephene Ally kuhusiana na beki huyo alisema kuwa: Owino aliomba ruhusu baada ya kumalizika mechi dhidi ya Kagera.”


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic