Kiungo mkabaji wa Simba, Jonas Mkude, ameiweka
njia panda timu yake baada ya jana Ijumaa kuumia mguu wake wa kulia wakati
kikosi hicho kikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Boko Veteran uliopo nje kidogo
ya jiji la Dar wakijiandaa na mchezo wa kesho wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam.
Mkude aliumia baada ya kugongana na beki wa
timu hiyo, Abdi Banda wakati wakiwa kwenye harakati za kugombania mpira.
Championi lilikuwepo uwanjani hapo na
kushuhudia tukio hilo ambapo baada ya kiungo huyo kuumia, daktari wa timu hiyo,
Yassin Gembe, aliingia uwanjani na kuanza kumtibu lakini akaona haitoshi,
akamchukua na kumpeleka hospitali kwa ajili ya kumchuguza ameumia kwa kiasi
gani.
Endapo kiungo huyo akikutwa ameumia sana na
kuukosa mchezo huo, basi Simba watalazimika kukuna kichwa ili kuweza kuliziba
pengo hilo kikamilifu kwani Mkude ni mchezaji tegemeo kikosini hapo.
Katika mazoezi hayo, kocha wa timu hiyo,
Mserbia, Goran Kopunovic, alikuwa anawaelekeza wachezaji wake jinsi ya
kushambulia kwa nguvu ili kuhakikisha wanapata mabao ya mapema na haraka katika
mchezo huo.
0 COMMENTS:
Post a Comment