AFRICAN SPORTS... |
Na Saleh Ally
AFRICAN Sports imefikisha jumla ya pointi 38
baada ya kucheza mechi 18 na ndiyo inayoongoza kundi lake, unaweza kusema
inanukia kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kuna makundi mawili na kila moja
litapandisha timu mbili. African Sports imebakiza mechi nne na kama itashinda
mbili kati ya hizo, basi ina uhakika.
Wakati African Sports inapambana kurejea
Ligi Kuu Bara, usisahau kuwa imekuwa chini ya udhamini wa kampuni ya Bin Slum
Tyres Ltd ya jijini Dar es Salaam ambayo mmiliki wake ni mnazi mkubwa wa
Coastal Union ya Tanga.
Coastal Union na African Sports ni
washindani wakubwa katika mji wa Tanga na usisahau historia inawabeba kama
ndugu wa Yanga na Simba.
Coastal ni ndugu wa Simba na African Sports
maarufu kama Wana Kimanumanu ni ndugu wa Yanga.
Bin Slum ni familia yenye wanazi wa Coastal
Union ambao ni washindani wakubwa wa African Sports lakini ndiyo kampuni
inayopambana kuhakikisha timu hiyo inapanda.
MOHAMMED BIN SLUM (KULIA) WAKATI WA KUSAINI MKATABA NA MBEYA CITY. |
Taarifa zinaeleza kwamba uongozi wa kampuni
hiyo ya matairi umekuwa ukipambana vilivyo kwa kushirikiana kwa karibu na
uongozi wa African Sports ‘Wana Kimanumanu’ ili kuhakikisha timu hiyo inarejea
Ligi Kuu Bara!
Maswali ni kama hivyo, vipi Bin Slum
anaisaidia African Sports wakati yeye ni Coastal Union tena wa kutupwa?
Kweli mdau wa Simba anaweza kuisaidia Yanga
kufanya vizuri? Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo ya kuuza matairi, Nassor Bin
Slum anafafanua.
“Kwanza nikubali kwamba hatujawa na mkataba
wa kikazi na African Sports. Lakini timu hiyo inadhaminiwa na kampuni hii
kupitia mdogo wangu ambaye pia ni shabiki wake.
“Mohammed bin Slum ni mmoja wa wanachama wa
African Sports kabisa. Kama mimi ambavyo niliwahi kupambana kuisaidia Coastal
Union, naye anafanya hivyo kwa African Sports.
“Wengi wamekuwa wakichanganya wanaposikia
Bin Slum wanadhani ni mimi. Lakini kampuni ndiyo hiyohiyo,” anasema bin Slum.
NASSOR BIN SLUM (KULIA) WAKATI WA KUINGIA MKATABA NA NDANDA FC. |
“Ingawa mimi ninaamini tofauti na watu
wengi. Kwamba kama African Sports itapanda daraja basi itakuwa ni manufaa
makubwa kwa Coastal Union.
“Mimi ni mnazi wa Coastal hata kama
siidhamini. African Sports ikiwa changamoto, najua na watu wa timu yangu wataongeza
juhudi kuhakikisha wanafanya vizuri kwa kuwa ushindani wa wapinzani wao utakuwa
karibu.”
Juhudi za kumpata Mohammed, zilifanikiwa.
Yeye ambaye ni mmoja wa vijana wanaopenda michezo anasisitiza kwamba African
Sports itakuwa changamoto kwa soka la mkoa wa Tanga.
“Mimi natokea Tanga, kampuni yetu iko Dar es
Salaam lakini bado inaweza kusaidia maendeleo ya soka katika mkoa wa Tanga pia.
“Utaona tuliwahi kuidhamini Coastal, sasa
tunaidhamini Stand United, Mbeya City na Ndanda FC. Hivyo kurudi nyumbani na kuisaidia
timu ya nyumbani si jambo baya.
“Naweza kusema katika suala la African
Sports, Bin Slum imekuwa ikijitolea kwa hali na mali ili kurudisha ushindani
katika soka mkoani Tanga,” ansema Bin Slum mdogo.
Kampuni hiyo maarufu ya kuuza matairi nchini
ndiyo inayoongoza kwa kudhamini timu nyingi zaidi katika Ligi Kuu Bara.
Bin Slum Tyres Ltd inadhamini timu tatu za
Mbeya City, Stand United na Ndanda FC na pia imeweka rekodi ya kuwa kampuni ya
kwanza kudhamini timu zilizopanda daraja ndani ya miaka miwili.
Iliiamini Mbeya City ikiwa ni msimu mmoja tu
baada ya kupanda daraja lakini ikafanya hivyo kwa Stand United na Ndanda FC
zikiwa ndiyo zimepanda daraja msimu huohuo.
0 COMMENTS:
Post a Comment