Sifa kubwa ya myama Simba ni uwindaji na
ulaji nyama mbicho. Swali Simba ya Dar es Salaam itaweza kula miwa?
Leo ina kibarua katika mechi ya fainali ya
Kombe la Mapinduzi dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro ambayo inamilikiwa na
kampuni inayotengeneza sukari inayotokana na miwa.
Mtibwa Sugar ndiyo vinara wa Ligi Kuu Bara,
tayari wamekutana na Simba kwenye ligi hiyo, matokeo yakawa sare ya mabao 1-1.
Mtibwa Sugar walisawazisha kwa bao la Mussa
Hassan Mgosi kutokana na makosa ya kipa kinda, Peter Manyika.
Baada ya hapo, timu hiyo zilikutana katika
mechi ya kirafiki mwishoni mwa mwaka jana,Simba ikalala kwa mabao 4-2 kwenye
Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar.
Halafu mechi ya kwanza ya uzinduzi wa
michuano ya Mapinduzi, Simba ikalala tena kwa bao 1-0.
Kama utazijumlisha mechi hizo tatu, Simba
imefunga mabao matatu, Mtibwa Sugar imefunga sita.
Hivyo kimahesabu Simba ina udhaifu kwenye
beki na ushambuliaji kama utalinganisha na Mtibwa Sugar.
Lakini kuna mabadiliko kwenye safu ya ulinzi
ya Simba hasa beki Juuko Murishid raia wa Uganda ambaye ameongeza nguvu, beki
huyo hakuwepo hata mechi ya ufunguzi wa Mapinduzi.
Lakini hata benchi la ufundi la Simba lina
Kocha Goran Kopunovic raia wa Serbia wakati Mtibwa Sugar inaongozwa na mzalendo,
Mecky Maxime.
Mchezo utakuwaje? Majibu yatapatikana leo
Saa 2;15 Usiku kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar wakati kila upande utakapocheza
ukitaka kuibuka na kombe hilo.
Tayari kombe halina mwenyewe baada ya
waliokuwa mabingwa KCCA ya Uganda kutolewa kwenye hatua ya robo fainali na nusu
fainali timu mbili za Visiwani na mbili kutoka Bara zilikutana na zile za Bara
ndiyo zimeingia fainali.
Kila upande umechanganyika kwa kuwa na
wachezaji wakongwe na makinda na hakika mechi itakuwa na ushindani mkubwa.
Simba itakuwa raha kwao kuhakikisha
inashinda mechi hiyo, kwani pamoja na kubeba kombe, itakuwa imelipa kisasi.
Lakini kwa Mtibwa Sugar, licha ya kutaka
kombe, lakini ina hamu ya kuendeleza ubabe dhidi ya vigogo hao.
Kosa kubwa kwa Mtibwa litakuwa ni kuidharau
Simba ambayo kusema bado haijakaa sawa ni kujidanganya kwa kuwa imefika
fainali.








0 COMMENTS:
Post a Comment