January 30, 2015

BDF XI

Kikosi cha timu ya BDF XI kimeshitukiwa kutokana na uamuzi wake wa kutangaza kutaka kujiondoa katika michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga kwa madai ya ukata.


Ratiba inaonyesha Yanga itaanza kuivaa BDF, Februari 14 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.

Shirikisho la Soka Afrika (Caf), limeingilia na kuonya kwamba BDF XI inachotakiwa ni kuwasilisha barua mara moja kama kweli imejitoa badala ya kutumia suala hilo kama mtego wa kuwababaisha wapinzani.

Caf imesisitiza, iwapo BDF XI itajitoa basi itakumbana na adhabu ya kufungiwa kutoshiriki michuano ya Caf kwa misimu miwili na faini ya dola 5,000 (Sh milioni tisa).

Msemaji wa BDF XI, Peo Keatlholetswe ameliambia Gazeti la Daily News la nchini humo kwamba Caf imewapa onyo na kutaka kupata uhakika katika hilo.

“Tumeelezwa kuwa tunatakiwa kutoa uhakika wa tunashiriki au la, wanaamini kusema bila kuweka mambo wazi unaweza kuwa sawa na mchezo mchafu wa kutaka kuwababaisha wapinzani wetu kutoka Tanzania.

 “Tutaweka kila kitu wazi hivi karibuni, lengo ni kujaribu kila namna ili tuweze kushiriki,” alisema Keatlholetswe.

Wakati Keatlholetswe anaeleza kuhusiana na onyo hilo la Caf, benchi la ufundi la Yanga limesema linajua mbinu zilivyo za kila aina, hivyo haliwezi kupunguza au kuisimamisha programu yake ya maandalizi.

Bosi msaidizi wa benchi la ufundi la Yanga, Charles Boniface Mkwasa, amefunguka zaidi. “Tumesikia suala lao la kujitoa, lakini hatutasitisha jambo katika programu yetu ya mazoezi. Tunachofanya ni kuendelea kama inavyotakiwa.

“Tutakuwa makini maana timu inaweza kusema imejitoa kumbe inaendelea na maandalizi. Michuano hii yenye ushindani mkubwa ina mbinu nyingi,” alisema Mkwasa ambaye anaweza kuondoka siku yoyote kwenda Botswana kusoma mchezo wa wapinzani wao.

Hivi karibuni Ligi Kuu ya Botswana ilipata bosi mpya wa bodi ya ligi ambaye amesema BDF XI na mabingwa Township Rollers watakaoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, lazima wataiwakilisha Botswana.

Arnold Somolokae amesema tayari juhudi za kuhakikisha Township Rollers inapata fedha zake za ubingwa zimefanyika na sasa wanahangaika na BDF kuona inashiriki michuano hiyo.

“Lazima zishiriki, tayari tumeanza kampeni ya kuhamasisha watu zaidi kupenda soka. Iwapo hazitashiriki haitakuwa na maana, tutapambana,” alisema.

Kwa kauli hiyo, maana yake timu hiyo itacheza na Yanga ambayo inapaswa kushikilia msimamo wake wa kuendelea na maandalizi ya kutosha.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic