| KIKOSI CHA BDF... |
Na Saleh Ally
KIKOSI cha Yanga chini ya Hans van der Pluijm kilionyesha soka safi
katika mechi yake ya kwanza ya Kombe la Shirikisho dhidi ya BDF XI ya Botswana.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam,
juzi, ilikuwa na burudani za kila aina, lakini BDF XI walitia fora kuanza na
kujilinda kuanzia dakika ya kwanza huku wakitumia watu 10 nyuma ya mpira.
Kwa kifupi timu nzima ilikuwa inakaba nyuma ya mpira, hivyo
kuwafanya wachezaji 18 wa timu zote mbili kucheza kwenye nusu moja ya uwanja na
kimahesabu husababisha mchezo kuwa mgumu.
Walitumia ujanja huo kuwazuia Yanga kufunga, lakini Yanga
walifanikiwa kuzuia mtego huo na kufunga mabao mawili ya krosi, yote yakifungwa
na Amissi Tambwe aliyeunganisha mipira ya kona na krosi ya Simon Msuva na
Mrisho Ngassa.
Ukiiangalia kwa haraka unaweza kudhani BDF XI ni timu laini lakini
uchezaji wao wakiwa ugenini umeonyesha bado wana sumu kali na Yanga watakutana
nayo huko Botswana katika mechi ya marudiano Februari 28.
Hakuna haja ya kuogopa, lakini ni vizuri kuwa na hofu kwa lengo la
kuweka tahadhari kwamba bao
mbili za Yanga si nyingi kwa kuwa BDF XI wanaweza kupata kama hizo wakiwa kwao.
Hivyo, ikiwezekana lazima Yanga wafunge wakiwa ugenini kwa kuwa
wanaweza kufanya hivyo au wahakikishe wanalinda tena kwa umakini mkubwa na si
makosa zaidi ya nane waliyofanya katikati ya eneo la boksi na BDF wakashindwa
kuyatumia. Wakiwa kwao, hawatazubaa hivyo.
Mashambulizi:
Walifanya mashambulizi takribani 11 ukilinganisha na zaidi ya 28 ya
Yanga lakini ilionekana wazi wastani wa ukali wa mashambulizi yao yalikuwa
makali zaidi.
Katika mashambulizi 11 makini yaliyokwenda kwenye lango la Yanga
kutoka upande wa BDF XI, nane yalionekana kuwa hatari.
Katika mashambulizi 28 waliyofikisha langoni kwa Waswana hao, 16
ndiyo yalionekana kuwa hatari sana na mawili yalizaa mabao ya Tambwe.
Utaona wastani kidogo kwa upande wa BDF XI unakuwa juu kuonyesha
kuwa ni hatari wanaposhambulia.
Hakuna ubishi kuwa BDF XI, wana mashambulizi hatari kupitia upande
wa kushoto na katikati hasa wakati wakimtumia sana Kabelo Seakanyeng aliyekuwa
amevaa jezi namba 7.
Wamchunge:
Hakuna ubishi, hata wafanyeje, Yanga wanalazimika kufanya kila
linalowezekana kuzuia mipango ya Seakanyeng.
Mgongoni alikuwa na namba 7, umbo lake si kubwa sana lakini ana kasi
na ni mwepesi wa kufanya maamuzi.
Hatari yake nyingine ni mtu anayechanganya, mjanja sana. Huwezi
kujua kama anapiga langoni au anatoa krosi. Kidogo unaweza kumfananisha na
Msuva, lakini si vibaya kusema ni mjanja zaidi na huenda ni sababu ya uzoefu.
Alisababisha hatari mara nane katika lango la Yanga.
Alisababisha beki Mbuyu Twite
kulambwa kadi ya njano.
Mara moja, mwamuzi alifanya huruma baada ya Twite kulazimika kumvuta
katika eneo la boksi. Hii inaonyesha kiasi gani alikuwa ni hatari kwa Yanga,
tena akiwa ugenini.
Pluijm lazima ajiulize mara mbili, kama ugenini kiungo huyo mwenye
kasi amekuwa moto hivyo, vipi akiwa nyumbani mbele ya mashabiki wake na anataka
kuibeba timu yake? Lazima itakuwa kazi ngumu inayohitaji umakini sana.
Wakati Yanga wanafanya juhudi za kumlinda Seakanyeng lazima wajue
hata Master Masitara ni hatari sana.
Masitara alikuwa amevaa jezi namba 26. Huenda ndiye mchezaji
aliyepiga mashuti mengi zaidi kwa upande wa kikosi chake.
Kweli zaidi ya mara nne hayakulenga lango, lakini ilionekana nguvu
ya mashuti au yalivyokwenda kwamba akijirekebisha ni hatari. Alipolenga lango,
tuliona Ally Mustapha alivyofanya kazi ya ziada kuokoa.
Akiwa kwao, atakuwa anajua namna ya kujirekebisha lakini kama fowadi
mjanja, atakuwa amesoma baadhi ya makosa ya safu ya ulinzi, hivyo atajua kitu
tofauti cha kufanya.
Ukiacha hao wawili, mwingine ni Keleagetse Gaolaolwe aliyekuwa na
jezi namba 27. Jamaa wajanja, katika listi alionekana ndiye namba sita, kumbe
namba 10.
Alisaidiana na Masitara sana, wanaonekana wanaelewana na mwepesi
kutoa pasi. Mara mbili ameruka juu na kupiga vichwa juu ya Yondani. Hivyo ni
bora katika mipira ya juu na pasi za mwisho, wasimpe nafasi hasa kwa makosa
yale iliyoyafanya difensi ya Yanga zaidi ya mara tano, badala ya kukaba,
wanarudi nyuma!
Moyo:
Pamoja na yote, Yanga wana kila sababu ya kuharibu moyo wa
mashambulizi wa BDF XI kwani wakiuacha ukatulia, basi utafanya kazi yake vema
na kuwamaliza.
Thatp Ogoposte aliyekuwa amevaa jezi namba 15, wakati wa upangaji
listi waliyogawiwa waandishi alionekana ni mshambuliaji wa kati, yaani namba 9.
Mechi ilipoanza alikuwa ndiye kiungo mkabaji, sema namba sita.
Yeye ndiye alipanga mashambulizi yote na ni mchezaji aliyekaba na
kutembea uwanjani ikiwezekana kuliko wote, juzi.
Jamaa mrefu hivi, maji ya kunde na mwenye mapafu ya mbwa. Usipokuwa
makini, huenda usijue kama yuko uwanjani lakini alikaba na kugawa mipira vizuri.
Ndiye alikuwa ‘friji’ yao. Kila waliposhambuliwa sana, wakiupata
mpira, alipelekewa yeye na kuanza kupoza presha kwa kucheza pasi fupifupi kabla
ya kuanza kuongoza mashambulizi kwenda mbele.
Yanga wakimuacha atulie akiwa kwao, basi atawamaliza kwa kuwa ni
mchezaji mjanja sana.







Naona unaongea mapenzi tu kama vile Yanga hawabadiliki na sku zote watacheza hivyo na makosa ni yaleyale!! Mpira unabadilika
ReplyDelete