Kamati ya
Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemfungia mechi tatu
beki George Michael Osei wa Ruvu Shooting kutokana na makosa ya kinidhamu aliyoyafanya
akiwa uwanjani.
Osei
ambaye alilalamikiwa na TFF kwa kumkaba na kumchezea kibabe mshambuliaji wa
Yanga, Amisi Tambwe ambapo ni kinyume na mchezo wa kiungwana (fair play)
ameadhibiwa kwa kuzingatia Ibara ya 48(1)(d) ya Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo
la 2012.
Mlalamikiwa
alifika mbele ya Kamati hiyo jana (Februari 9 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Akisoma
uamuzi huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wakili Jerome Msemwa alisema Osei
alipopewa nafasi ya kujitetea alikana kufanya kosa hilo na kudai magazeti
yametengeneza picha hizo. TFF iliwasilisha ushahidi wa magazeti mawili ya
Championi na moja la The Guardian kwa kuzingatia Ibara ya 96(3) ya Kanuni ya Nidhamu ya TFF Toleo la 2012.
Katika
uamuzi wake, Kamati imesema kitendo cha Osei ni kinyume na kanuni ya mchezo wa
kiungwana (fair play), na kuongeza kuwa kanuni za TFF kwa makosa kama hayo ni
dhaifu, hivyo kuagiza zirekebishwe ili ziweze kuwa kali zaidi.
Katika
hatua nyingine Kamati hiyo, imetupa malalamiko yaliyowasilishwa na TFF dhidi
Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM), Mugisha Galibona,
na Katibu wa Simiyu (SIFA), Emmanuel Sorogo.
Kwa upande
wa Sorogo, Kamati imesema baada ya kupitia vielelezo vya pande zote, hasa
upande mlalamikiwa imeridhika kuwa hakushiriki katika kumpiga refa kwenye mechi
ya Kombe la Taifa kwa Wanawake kati ya Shinyanga na Simiyu.
Badala
yake aliyehusika ni Kocha wa Simiyu, Emmanuel Babu ambaye tayari uongozi
umeshachukua hatua dhidi yake kwa kumsimamisha kwanza wakati akisubiri
kufikishwa mbele ya Kamati ya Nidhamu ya SIFA.
Pia barua
ya kumsimamisha kocha huyo ilitumwa kwa Katibu Mkuu wa TFF na Mkurugenzi wa
Mashindano. Kamati imeyachukulia maneno ya mlalamikiwa kuwa ni sahihi ndiyo
maana hayakupingwa na TFF, hivyo malalamiko dhidi ya mlalamikiwa hayana msingi
na yametupwa.
Kwa upande
wa Galibona ambaye ripoti za Kamishna na refa zilionyesha kuwa alishiriki
kuhamasisha marefa kupigwa baada ya mechi ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati
ya Polisi Mara FC na Mwadui FC, Kamati imesema mlalamikiwa aliwasilisha
vielelezo vinne kuthibitisha kuwa hakuhusika.
Kamati
imesema licha ya ripoti ya Saleh Mang'ola kumtaja Galibona, lakini maelezo ya
refa huyo na msaidizi wake Rebecca Mulokozi waliyoandika Kituo cha Polisi baada
ya tukio hilo hayakumtaja mlalamikiwa mahali popote.
Pia barua
ya FAM kwenda TFF kuhusu matukio ya mechi hiyo yanamtoa hatiani mlalamikiwa,
hivyo Kamati imeamuru kuwa malalamiko dhidi ya Galibona hayana msingi na
yametupiliwa mbali.
0 COMMENTS:
Post a Comment