Unapozungumzia kikosi cha El
Merreikh, hakuna ubishi ni sehemu ya historia ya soka la Bara la Afrika.
El Merreikh ni moja ya
klabu kubwa na kongwe katika Bara la Afrika, yenye uzoefu mkubwa na michuano ya
kimataifa, tena inayoundwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa.
Makocha wanaoifundisha El Merreikh
kama waliyekuja naye, pia ni wa kiwango cha juu kabisa kwa kuwa aliwahi kuipa TP
Mazembe ubingwa wa Afrika.
Usisahau El Merreikh
wamekuwa wakicheza katika hatua za makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa, ikiwa
na maana kwamba si kikosi cha kung’olewa mapema.
Lakini Azam FC wameonyesha
kuna ambalo linawezekana licha ya kwamba wengi waliona haliwezekani. Wameifunga
El Merreikh kwa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa.
Azam FC wameweka rekodi
nzuri sana, kwamba mechi yao ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika tena dhidi ya
kigogo cha Afrika, wao wamefanikiwa kuibuka na ushindi, si kazi rahisi.
Ushindi wa Azam ni sehemu
ya picha kwamba kuna mambo yanawezekana na kujipanga ndiyo jambo la msingi. Tunajua
Azam FC wamekuwa wakijipanga kila siku zinavyosonga mbele.
Utakumbuka Azam FC walianza
kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho, walifanya hivyo mara mbili kabla ya
kutwaa ubingwa kwa mara ya kwanza na kufanikiwa kupata nafasi ya kushiriki Ligi
ya Mabingwa kwa mara ya kwanza.
Wakati wanaingia katika Ligi
ya Mabingwa Afrika, walikuwa wamejifunza mambo kadhaa kupitia katika Kombe la Shirikisho
waliloshiriki mara mbili. Wameanza na rekodi nzuri kwa kushinda dhidi ya vigogo.
Azam FC wameshinda huku
wakionyesha soka safi, wakishambulia zaidi na walionyesha ufundi mkubwa katika
kujilinda dhidi ya timu hiyo ngumu ya El Merreikh.
Kitu ambacho wanapaswa Azam
FC kukikubali kabla ya safari yao ya wiki mbili zijazo kwenda Sudan, bado
hawajaimaliza El Merreikh na wanachotakiwa kuamini dakika 90 nyingine ndizo
zenye uwezo wa kuwavusha mbele na kuing’oa timu hiyo ngumu na kongwe barani Afrika.
Ushindi wa mabao 2-0
uliopatikana Dar es Salaam Azam FC wakiwa wenyeji, unaweza kupatikana Sudan El Merreikh
wakiwa wenyeji pia kwa kuwa ni timu yenye uwezo wa kufanya hivyo.
Tuliona uchezaji wao, kwamba
licha ya Azam kufanya vizuri sana katika mechi ya jana, lakini kikosi hicho cha
Wasudan kilionyesha soka safi linalothibitisha kwamba kweli wana kikosi kizuri.
Kawaida wanacheza taratibu,
lakini wanaojiamini na wanaojua wanafanya nini. Watakapokuwa nyumbani kwao
lazima kutakuwa na mabadiliko makubwa kiuchezaji.
Lakini uchezaji uwanjani
hauwezi kutosha kuifanya Azam FC ipite katika michuano hiyo. Wewe utakataa, mimi
nitakuambia kwamba michuano kama hiyo chini ya Caf ina mambo mengi pamoja na
fitina nje ya uwanja.
Kamwe sisemi Azam FC
wafanye ushirikina, lakini nawakumbusha umakini kabla hawajaingia uwanjani kwa kuwa
Wasudan wana sifa ya kupulizia dawa ya kupunguza nguvu kwenye vyumba vya timu
pinzani au kwenye lifti.
Taifa Stars wakati inafuzu
kucheza kombe la Chan mwaka 2009, nguvu kubwa ya wadau na watu wa TFF ilitumika
kuwazuia Wasudan hao kufanya fitina zao mbaya. Wachezaji hawakupanda lifti, wakatumia
ngazi.
Safari hii Azam FC watajilipia
hoteli kutokana na mabadiliko ya Caf. Lakini bado watakuwa ugenini, hivyo wanapaswa
kuwa makini katika masuala ya chakula na wapi watalala.
Halafu baada ya hapo
waingie uwanjani na kuhakikisha wanacheza soka kwa umakini mkubwa wakiamini
bado wanaweza kufanya vizuri lakini nidhamu ya mchezo waliyoionyesha jana, basi
wakiwa Sudan, iwe mara tatu yake. Kila la kheri.







0 COMMENTS:
Post a Comment