Baada ya Kocha Mkuu wa Yanga, Mholanzi, Hans
van Der Pluijm, kufanikiwa kuiongoza timu hiyo kufanya vizuri katika mechi zake
kadhaa ikiwemo ya kimataifa dhidi ya BDF XI ya Botswana, hatimaye uongozi wa
klabu hiyo umeamua kumuongezea mkataba.
Uamuzi wa kumuongezea mkataba kocha huyo wa
zamani wa Berekum Chelsea ya Ghana, ulikuja baada ya kikao cha viongozi wa Yanga kilichoketi
takriban wiki moja iliyopita kwa lengo la kufanya tathmini ya ufundishaji na
uwezo wa kocha huyo.
Kikao hicho kilitoka na majibu kuwa Pluijm
anafaa kuendelea kuinoa timu hiyo kulingana na idadi ya mechi alizoshinda na
soka linalotandazwa uwanjani kwa sasa na vijana hao wa Jangwani tangu atue
rasmi Desemba, mwaka jana, hivyo tayari mpaka sasa kamati ya mashindano ipo
kwenye mchakato wa kuzungumza na Pluijm juu ya mkataba huo mpya ingawa
haukuwekwa wazi kuwa utakuwa ni wa muda gani.
Msemaji wa Yanga, Jerry Muro, amefafanua kuwa tathmini
imeonyesha kwamba Pluijm amekuwa na asilimia nyingi zaidi za kuibuka na ushindi
katika mechi za mashindano yote alizoiongoza timu hiyo tangu aliporithi mikoba
ya Mbrazili, Marcio Maximo aliyefungashiwa virago siku chache baada ya kufungwa
mabao 2-0 na Simba kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe.
“Kama tulivyosema kuwa kocha tutamfanyia tathmini
baada ya mechi kadhaa na kweli kumekuwa na kikao hicho ambacho kiligundua kuwa
amekuwa na mafanikio kwa asilimia nyingi zaidi.
“Kutokana na hilo, tumegundua ni kocha
anayetufaa kwa misimu mingine, hivyo tuna lengo kubwa la kuendelea kuwa naye
hapa, tunaangalia pia jinsi gani tunaweza kuzungumza naye na kumpa mkataba wa
kuendelea kuwa nasi,” alisema Muro.
Pluijm ambaye alisaini mkataba wa mwaka mmoja
na nusu, mpaka sasa ameiongoza timu hiyo kwenye michezo sita ya Ligi Kuu Bara,
akishinda mitatu na kusuluhu mitatu. Kwenye Kombe la Mapinduzi, Yanga ilijitupa
dimbani mara nne, ikashinda mara tatu na kufungwa mara moja.
Mechi za Pluijm:
Kushinda: Polisi Moro 1-0, Coastal 1-0, Mtibwa
2-0, Taifa Jang’ombe 4-0, Polisi 4-0, Shaba 1-0, BDF XI 2-0
Sare: Azam 2-2, Ruvu Shooting 0-0, Ndanda 0-0
Kufungwa: JKU 1-0







0 COMMENTS:
Post a Comment