Wawakilishi wa Tanzania
katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam FC leo Jumamosi wanacheza mechi ya
marudiano dhidi ya El Merreikh ya Sudan nchini hapa ikiwa na kumbukumbu ya kushinda
mabao 2-0 wiki mbili zilizopita.
Ili kuvuka hatua hii ya
awali, Azam inatakiwa itoke sare au ifungwe si zaidi ya idadi ya bao 1-0 au
kufungwa kokote kunakofanana na huko na ikishinda itakuwa vizuri zaidi. Mchezo
huo utakaochezwa na mwamuzi Wellington Kaoma wa Zambia utachezwa hapa jijini
Khartoum, Sudan.
Katika mchezo wa kwanza ni
wazi El Merreikh ilikumbana na kitu ambacho haikukitarajia kwani kipigo cha
mabao 2-0, kiliwashutua hivyo sasa wana kazi moja ya kuhakikisha hawafanyi
makosa kama ilivyotokea katika mchezo wa awali.
Maandalizi ya El Merreikh
yameonekana kuegemea zaidi katika safu yao ya ulinzi na Kocha Diego Garzitto
ameonekana kuchanganywa na kipigo cha ugenini hivyo anataka kuthibitisha
thamani yake katika mchezo wa leo.
Tangu kupoteza mechi yake
ya kwanza na Azam, mashabiki wa El Merreikh wamekuwa na shahuku ya kufahamu
ubora wa Azam na sababu kubwa ni ipi hadi timu yao ikapoteza mechi hiyo jijini
Dar es Salaam kwa mabao 2-0.
USHINDI AU KAZI BASI
Baadhi ya maofisa wa El
Merreikh wamelithibitishia gazeti hili kwamba endapo Azam itafanikiwa kusonga
mbele na wao kutolewa kuna uwezekano mkubwa, Garzitto akapoteza kazi yake kwani
inaonekana uwezo wake utakuwa umeishia hapo katika kuwasaidia.
Katika mazoezi yake
kujiandaa na mechi dhidi ya Azam, Garzitto ameonekana akiwasisitiza
washambuliaji wake kuwa makini katika eneo la hatari ili kupata mabao mengi ya
mapema ili kuidhohofisha Azam itakayokuwa chini ya beki wa kati, Pascal Wawa
aliyewahi kuichezea El Merreikh.
“Hatuhitaji mambo mengi
sana uwanjani zaidi ya kufanya vizuri na kusonga mbele, kocha ameshaambiwa nini
tunachokihitaji kutoka kwake hapo mwanzo hatukuifikiria Azam kama ingeweza
kupata ushindi wa aina hii.
“Ni zamani sana sisi kuishia
hatua ya awali kwenye michuano hii mikubwa Afrika, ni jukumu la benchi la
ufundi kuhakikisha hatufanyi vibaya nyumbani mbele ya mashabiki wetu lukuki,
kuna kitu kibaya kinaweza kutokea endapo tutapoteza mchezo huu,” alisema mmoja
wa maofisa wa El Merreikh.
Kwa mujibu wa ofisa huyo,
Garzitto anaonekana kuyafanyia kazi maneno aliyoambiwa na muda mwingi amekuwa
akitoa maelekezo yake kwa washambuliaji wake, Allan Wanga na Mohamed Traore ili
waweze kufanya vizuri.
Inaonekana tegemeo pekee la
kocha huyo ni Wanga na Traore ambao walikutana kipindi cha pili katika mechi
dhidi ya Azam jijini Dar es Salaam na kudhibitiwa vikali na Wawa raia wa Ivory
Coast.
WANGA, TRAORE KUANZA
Kwa mujibu wa maofisa wa El
Merreikh, Garzitto amepanga kuanza na washambuliaji Wanga na Traore kwa pamoja
ili kupata ushindi wa mapema na kumchanganya beki Wawa aliyeonekana kuwa
kikwazo kwao katika mchezo wa awali.
“Lilikuwa kosa kumuingiza
Traore kipindi cha pili katika mchezo ule wa awali, hapa tatizo lilikuwa kocha
kutoifahamu vizuri Azam hasa kuongezeka kwa Wawa kwenye kikosi chao kwani
tulipocheza nao kwenye Kombe la Kagame, Wawa tulikuwa naye huku.
“Hakuijua vizuri safu ya
ulinzi ya Azam lakini sasa ana kitu cha kufanyia kazi na amesisitiza kumtumia
Traore mapema ili kuidhoofisha timu pinzani, kocha anapambana sana kuhakikisha
kikosi chake kinafanya vizuri,” anasema ofisa huyo.
Ofisa huyo anasema
anafahamu Azam ina faida ya Wawa ambaye si kwamba anawafahamu washambuliaji wa
El Merreikh bali ni mzoefu wa soka la Afrika ndiyo maana aliwamudu jijini Dar
es Salaam. “Wote wataanza na hata kama Wawa atawazuia, atachoka tu kwani uwezo
wake si sawa na wa wenzake katika safu ya ulinzi,” anasema.
KAZI YA AZAM
Tangu ilipowasili Azam
inaonekana kufanyia kazi zaidi ulinzi huku Wawa akionekana kuwa msaada mkubwa
wa kutoa baadhi ya maelekezo kwa wenzake kwenye Uwanja wa Jeshi waliofanyia
mazoezi jijini Khartoum.
Kitu kimoja muhimu kwa Azam
ni kutokubali kuruhusu icheze kwa kujilinda ikiamini mabao mawili iliyopata
awali ni mengi na yanayoweza kuwavusha katika hatua ya awali.
“Lengo ni kucheza kwa
kujilinda zaidi ili timu isonge mbele na kutopata madhara ugenini hivyo ni
lazima tujilinde, lakini kwa akili sana siyo kila mara kwani tunahitaji ushindi
pia kuweza kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele,” anasema kocha wa Azam,
Joseph Omog.
Katika mazoezi ya siku
tangu jana ilipowasili hapa, wachezaji wa Azam wameonekana kuwa na furaha muda
wote wakiishi kwa kushirikiana kwa kila kitu.
Mchezo huu umekuwa gumzo
jijini Khartoum na kila mdau wa soka anataka kuitazama Azam ni timu ya aina
gani hadi iweze kuifunga El Merreikh mabao 2-0 nyumbani. Tusubiri dakika 90.
Vikosi vinavyotarajiwa
kuanza leo;
Azam; Aishi Manula, Shomari
Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Pascal Wawa, Michael Bolou, Salum Aboubakari
‘Sure Boy’, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Kipre Tchetche na Brian Majwega.
El Merreikh; Magoola Salim,
Kamal Amir, Gafar Ali, Alrayah Maki, Babeker Bakri, Okrah Augustine, Mussa
Mussab, Hado Alaa, Traore, Shareif Ramadhan na Wanga.
Fin…
0 COMMENTS:
Post a Comment