Mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva na
beki wa pembeni wa Mtibwa Sugar, David Luhende, kila mmoja kwa muda wake ametoa
vitisho vya kuhakikisha anamzimisha mwenzake katika mechi baina ya timu hizo kwenye
Ligi Kuu Bara, kesho Jumapili.
Yanga inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mtibwa
kwenye Uwanja wa Taifa, ambapo Msuva ndiye amekuwa staa wa Yanga katika siku za
hivi karibuni huku Luhende ndiye beki wa Mtibwa ambaye anaweza kukutana naye
mara kwa mara ikiwa wote watacheza mechi hiyo.
Msuva ameliambia gazeti hili kuwa, yupo fiti
kupambana na beki yeyote atakayekutana naye bila kujali ni Luhende au mwingine.
“Nikwambie ukweli tu, mimi nikiamua jambo langu
uwanjani, hakuna mchezaji yeyote atakayenizuia, hivyo huyo beki wa Mtibwa
atakayepangwa basi anatakiwa ajiandae.
“Kama atapangwa kuanza Luhende, itakuwa vizuri
kwangu kwa sababu ninamjua vizuri, nitamtia hasira tu kwa kumpiga chenga za
maudhi na kukokota mpira kwa kasi kwa ajili ya kumchosha,” alisema Msuva.
Upande wa Luhende ambaye ni mchezaji wa zamani
wa Yanga, alisema: “Mimi hakuna mshambuliaji ninayemhofia, nimejiandaa vizuri
na mechi hiyo dhidi ya Yanga, sitaki kuongea sana, tuonane uwanjani.”







0 COMMENTS:
Post a Comment