Timu tatu zinazochuana vikali katika kilele
cha Ligi Kuu Bara, Yanga, Azam na Simba wapo ngoma droo katika kuzifumania
nyavu za ligi hiyo ambapo mpaka sasa kila moja imefunga mabao 25.
Timu hizo zote zipo katika nafasi tatu za juu
kwenye msimamo wa ligi hiyo ambayo inatarajiwa kufikia tamati Mei 9, mwaka huu.
Yanga ambao ndiyo vinara baada ya kuwa na
pointi 37, wamecheza michezo 18, sawa na Azam wenye 36, huku Simba wakiwa
wamecheza michezo 20, wakiwa na pointi 32 na leo Wanajangwani hao wanatarajia
kushuka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar kupambana na JKT Ruvu.
Licha ya kuwa sawa kwenye kufunga mabao, ukuta
wa Simba ndiyo unaonekana kuwa mbovu kwani umeruhusu mabao 14, Azam wao
wameruhusu mabao 12, huku Yanga wakifungwa 10.
Katika orodha ya wachezaji wanaoongoza kwa
kuzifumania nyavu, Didier Kavumbagu wa Azam ndiye anaongoza kwa kuwa na mabao
10, huku Simon Msuva wa Yanga akiwa na tisa na kwa upande wa Simba kinara ni
Emmanuel Okwi baada ya kufunga mabao saba.
Timu hizo zote zipo katika nafasi ya kuutwaa
ubingwa msimu huu lakini Yanga na Azam ndizo zinatajwa sana kwa kuwa zina
michezo mingi mkononi zaidi ya Simba.
0 COMMENTS:
Post a Comment