Kocha
Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic, ameibuka na kutamba kuwa sasa kikosi chake
kimeingia kwenye vita ya kuwania ubingwa wa ligi kuu msimu huu.
Tambo
hizo zimekuja kufuatia kasi ya kugawa dozi, ambapo timu hiyo imeshinda michezo
mitatu mfululizo; dhidi ya Prisons, Yanga kabla ya juzi Jumamosi kuinyuka
Mtibwa Sugar bao 1-0.
Simba
ilianza msimu kwa kusuasua ikiwa chini ya Mzambia, Patrick Phiri lakini kwa
sasa ndiyo timu tishio ikiwa chini ya Mserbia, Kopunovic.
Kopunovic
amesema awali alianza kwa kukijenga upya kikosi chake, lakini kwa sasa
wameingia rasmi kwenye kinyang’anyiro cha ubingwa, unaowaniwa pia na vinara
Yanga na Azam ambao wanautetea.
“Tuko kwenye vita ya kuwania ubingwa, naamini
kwa idadi ya pointi tulizonazo pamoja na wale walio juu yetu, nina imani
tunaweza kuuwania. Awali tulikuwa tunajenga kikosi kutokana na kukikuta hakina
morali lakini sasa tunaangalia jinsi ya kutwaa taji,” alisema Mserbia huyo,
kabla ya Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Idd Kajuna kufunguka zaidi.
“Huu
ndiyo mwanzo wa kuwania ubingwa, tulikuwa kwenye kipindi cha mpito, tulianza
vibaya ligi lakini sisi kama viongozi tumehimiza mshikamano kuhakikisha timu
inarejesha imani ya kutwaa ubingwa. Naamini tunaweza kufanya hivyo sasa,”
alisema Kajuna.
Ushindi
wa juzi uliifanya Simba kufikisha pointi 29, mbili nyuma ya vinara Yanga ambao
wana mechi mbili mkononi.
0 COMMENTS:
Post a Comment