March 16, 2015


Na Saleh Ally
BAO alilofungwa kipa Ally Mustapha ‘Barthez’ wa Yanga katika mechi dhidi ya Simba, lilionekana ni kosa la karne kwake, hakuna aliyejali mfungaji alikuwa mahiri kiasi gani.

Acha wengine waamini Barthez ni mzembe sana! Lakini bao kama hilo au linalofanana kwa kiasi cha asilimia 80, amefungwa pia kipa Said Mohammed ‘Nduda’ wa Mtibwa Sugar.

Nakukumbusha aliyemfunga Barthez, ndiye aliyemfunga kipa huyo wa Mtibwa. Hawa ndiyo makipa wazembe zaidi kwa mwezi huu? Au mfungaji anapaswa kupongezwa kwa umahiri wa hali ya juu aliouonyesha?
Kila mmoja anaweza kuchagua anavyoona yeye kulingana na msukumo, uwe wa kishabiki au kitalaamu, ila ukweli Mganda Emmanuel Okwi ni hatari.

Hawezi kuwa hatari wa maneno, lakini uwezo mkubwa wa kufunga ambao amekuwa akiuonyesha sasa hauna ubishi.

Si mara moja ameifunga Yanga au timu nyingine ya Ligi Kuu Bara unayoijua, lakini amefunga mabao mawili yenye kiwango cha juu kabisa katika kipindi cha siku kumi tu.

Ameonyesha uwezo mkubwa unaotoa majibu kuwa kiutendaji Okwi ni tofauti na wachezaji wengi wengine wakiwemo wazawa na wale wa nje.

Okwi ni mbunifu, Okwi ni aina ya wachezaji wenye kipawa cha juu cha soka. Lakini bado unaweza kumlaumu kwa utukutu.

Ana mambo mengi amekuwa akijadiliwa au kutotekeleza kile alichoomba au kuahidi kukifanya. Kama kuwahi kurejea lakini mwisho asifanye hivyo.

Mwisho wa ukweli uko hivi, Okwi ana uwezo mkubwa ambao unatakiwa kuwa changamoto kwa wachezaji wa nyumbani.

Kweli timu kama Simba, Yanga, Azam FC, Mtibwa Sugar na nyingine zinawaleta wachezaji bora katika vikosi vyao kwa lengo la kufanya vyema.

Lakini taifa litafaidika katika maendeleo ya soka kwa kuwa na wachezaji kutoka nje wenye uwezo wa juu kama Okwi. Wanaotaka kujifunza, hakika watafaidika.


Bao dhidi ya Yanga, huenda ilikuwa ni rahisi sana au alibahatisha. Lakini alipofunga dhidi ya Mtibwa Sugar, waliokataa au walioamini alibahatisha, si rahisi kufungua tena midomo yao kusema jambo hilo.

Binadamu kawaida hatukubali mapema, inawezekana wako wanaoendelea kukataa licha ya Okwi kufunga dhidi ya Yanga na akafanya hivyo dhidi ya Mtibwa Sugar.

Pointi sita muhimu kupitia mabao mawili bomba kabisa. Okwi anahitaji kujivunia ingawa yeye anasisitiza kuwa ameamua kuongeza mazoezi.

“Lengo langu ni kufunga, nikishindwa basi nitoe pasi izae bao au niwe na mchango mkubwa kwenye timu kwa kusaidiana na wenzangu.

“Mambo yote ni Mungu na ndiye ninayemshukuru sana. Lakini nimepania kusaidiana na wenzangu kuleta mabadiliko Simba,” alisisitiza.

 Mabao:
Okwi ndiye mshambuliaji aliyefunga mabao mazuri zaidi kwa msimu huu kama utalinganisha yote yaliyofungwa.
Kabla ya mchezo wa jana wa Mbeya City dhidi ya Mgambo JKT, mabao 223 yalikuwa yamefungwa katika Ligi Kuu Bara ikiwa inaenda ukingoni. Hadi sasa asilimia 50 ya mabao yake yanaonyesha kipaji na uwezo wa juu zaidi.

 Kiboko ya mabeki:
Simba inapomkosa Okwi, hakuna ubishi nguvu kubwa inapungua kwa kuwa ndiye tishio la kila ngome inayokutana na Simba.

Huenda anaingia kwenye akili za kila kocha anayekutana na Simba. Hivyo kufanya kumwekea umakini na wakati mwingine kuharibu mipango mingine ya kawaida.

Hakuna ngome ambayo imeweza kudhibiti makali yake kwa asilimia mia. Kwani hata ile inayoongozwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani ambao ndiyo viongozi wa ngome ya Taifa Stars, wamemshindwa!

Pasi nzuri:
Mmoja wa wachezaji wanaotoa pasi nzuri za mwisho zinazozaa mabao ni Okwi, iwe ni pasi ya kawaida au krosi.

Okwi anajua afanye nini katika wakati mwafaka na mfano mzuri pasi alizompa Danny Sserunkuma katika mabao yake mawili aliyofunga.

Lakini anajua mpira uende kwa nani katika wakati upi, hasa timu inapokuwa inashambulia kwa kasi.

Kuipandisha timu:
Anaposhika mpira, hasa kama Simba ilikuwa inashambuliwa halafu akauchukua yeye, ndiyo kipindi ambacho timu hupanda kwa kasi zaidi.

Anajua kuipandisha timu kwa kasi, huku akiwa na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira akiwa anawachanganya mabeki kwa kuwa hawajui atafanya kipi kwa wakati mmoja.

Maana ana uwezo wa kupiga na kufunga, kutoa pasi ya bao au kuendelea kuumiliki mpira. Hii ni sehemu ya sifa kubwa mno aliyonayo na huenda asilimia 85 ya wachezaji wanaocheza Ligi Kuu Bara katika timu 14 wasiwe nayo.


Msumbufu:
Kumekuwa na lawama mara kadhaa kutoka kwa wachezaji wenzake ambazo zinaonyesha kweli Okwi naye kama binadamu ana matatizo yake.

Moja ni kutoshiriki mazoezi vya kutosha, hali inayowaudhi wenzake. Kuchelewa mazoezini au kutoonyesha yuko na wenzake pamoja.

Kuaga akachelewa kurudi, ingawa hili kalirekebisha sana. Kikubwa hapa ni ule msemo wa kuangalia mazuri ya mtu zaidi kuliko mabaya yake.

Kesi:
Okwi ana kesi ameishtaki Etoile du Sahel kwa kutompa mshahara wake kwa wakati mwafaka, timu hiyo ya Tunisia nayo imeshtaki pia.

Hali kadhalika, Yanga imemshtaki, naye pia kaishtaki. Hii inaonyesha kiasi gani Okwi anavyoongoza kwa kesi.

Hii inaweza kuwa tafsiri mara mbili tofauti. Mchezaji mtukutu kwa kuwa na kesi lukuki alizoshtaki na kushtakiwa, pia mchezaji anayezijua haki zake.

Uchungu:
Hata ajiunge na timu gani, Okwi ameonyesha Simba ni nyumbani. Kwani ndiyo timu anayoichezea kwa kiwango cha juu zaidi anapokuwa nayo. Unaweza kupima alipokuwa Etoile du Sahel, Yanga na sasa Simba.

Mfano mzuri aliamua kumuacha mkewe na kuahirisha fungate ili arejee na kuichezea Simba dhidi ya Kagera.

Bado utamuona anavyohangaika uwanjani kuhakikisha inapata ushindi kila anapokuwa anacheza. Unaweza kujifunza kupitia mazuri au mabaya yake.




1 COMMENTS:

  1. Kaka unamahaba na msimbazi kumshinda hata Kaduguda!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic