Na Saleh Ally
NILISHANGAZWA na taarifa ya mwandishi mmoja
wa Kenya kutupia maneno kwenye mtandao akisema mshambuliaji wa Simba, Danny
Sserunkuma aliamua kurejea kwao Uganda kwa kuwa viongozi wa Simba wamekuwa
wakimlazimisha kutumia ushirikina.
Kauli ya mwandishi huyo ilinifanya niingie
kufanya uchunguzi kwa mara nyingine tena kuhakikisha mambo mawili ambayo tayari
niliwahi kuyafanyia utafiti wa kawaida kabisa.
Moja, kweli amekuwa akilazimishwa? Pili,
Uganda au Kenya, hawafanyi mambo ya kishirikina katika mchezo wa soka kama
ilivyo hapa nyumbani?
Mimi ninaweza kuthibitisha kokote kwa Yanga,
Simba na klabu nyingine wamekuwa wakifanya mambo ya kishirikina. Hata klabu za
daraja la kwanza, la pili, tatu na mechi za mchangani, ushirikina umekuwa
ukifanyika.
Ushirikina katika soka ni miradi ya watu au
nio kuridhisha imani za wanaoamini ushirikina unafanya kazi katika soka. Ukweli
hakuna lolote lonaloweza kusaidiwa na ushirikina. Vipi wasiofanya wanafanikiwa
na sisi ni ziro halafu tuamini ushirikina ndiyo uokozi?
Uchunguzi wangu unaonyesha kwanza Kenya na
Uganda nao wamekuwa wakiamini mambo hayo ya ushirikina. Raha zaidi niliamua
kufanya mahojiano na mmoja wa makocha wa zamani wa Gor Mahia ambayo alikuwa akichezea
Sserunkuma, akanithibitishia ni jambo la kawaida kufanya ushirikina na mambo
mengi ya kimira kwa kuwa ile ni timu ya kikabila!
Kamwe sitaunga mkono ushirikina, lakini
tayari I mradi wa watu fulani wanaoutumia kupata fedha katika soka la Afrika
ukizijumlisha Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na kwingineko. Lakini
ukweli, hausaidii lolote kwa mchezaji wala timu na wengine wamekuwa wakikubali
kushiriki kama utaratibu tu wa kabla ya mechi, lakini hawaamini.
Baada ya hapo nikarudi kufanya mahojiano na
viongozi wa Simba kupata usahihi wa kipi alichokifanya Sserunkuma na kama kweli
alitishia kutorejea na kuhusisha ushirikina, licha ya kupigwa sana chenga,
mwisho nikagundua ni kweli.
Sserunkuma alilalamika kwamba ameshindwa
kuonyesha kiwango chake kwa kuwa anafanyiwa ushirikina. Mwisho akawaambia
viongozi wa Simba anataka kuvunja mkataba, alifanya hivyo mara mbili kupitia
kwake na kwa meneja wake.
Simba walishangazwa naye na kumtaka aachane
na kuamini ushirikina. Mwisho yeye akasisitiza hatarejea na suala la kuvunja
mkataba atalipa kipaumbele.
Baada ya Simba kukaa kimya, mwenye alituma
tena ujumbe kupitia barua pepe akiomba radhi kwamba wakati anasema anataka
kuvunja mkataba hakuwa katika hali nzuri. Siku iliyofuata meneja wake naye
alituma narua pepe Simba na kusisitiza “wakati mwingine wachezaji ni kama
watoto”, hivyo wamsamehe na atarejea kazini. Kweli alirejea na siku iliyofuata
alionekana jukwaani wakati Simba ikishinda mabao 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja
wa Taifa jijini Dar!
Maswali mawili ya haraka. Moja, vipi
mchezaji kama Sserunkuma anaanza kuamini utendaji wake umeshuka kutokana na
kufanyiwa ushirikina? Pili, aliamua kuvunja mkataba, sasa vipi mbona ameamua
kurudi?
Inawezekana majibu niliyoyapata yanaweza
yasiwe sahihi, lakini lile la kuamini kuwa hata Sserunkuma naye ni tatizo
linaweza kuwa sahihi zaidi.
Anaamini ushirikina unaweza kumfanya
mchezaji fulani asicheze! Kweli unaweza kumroga Lionel Messi au Cristiano
Ronaldo akashindwa kucheza? Kama anarogwa yeye ambaye hata bado hajakaa vizuri
kwa kiwango, vipi hafanyiwi hivyo Emmanuel Okwi au Juuko Murishid ambao wote ni
Waganda?
Ninaamini Sserunkuma ni kati ya wachezaji
wenye uwezo. Amedhihirisha hayo akiwa Kenya, ameonyesha anaweza kwa kuitwa
kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uganda, The Cranes na inajulikana ina
ushindani mkubwa.
Lakini hawezi kukataa kuwa ameingia kwenye
mlango usio sahihi na kama ataendelea hivyo, basi hatainuka na ataendelea
kuyumba hadi siku atakayoondoka Tanzania. Ukiuamini ushirikina, kweli
unakushuka. Kama Mungu yupo, anayefanya ushirikina hawezi kuwa bora kuliko
anayemuamini Mungu.
Kama Sserunkuma anaamini alikuwa staa Kenya,
basi atafika hapa siku mbili na kuwa staa tena kajidanganya. Okwi hakung’ara
siku ya kwanza au msimu wa kwanza, kapambana kweli.
Juuko, sasa ameanza kukubalika, anajituma na
kazi anafanya. Sasa vipi yeye anataka alale au kutembelea nyota ya historia
yake ya Kenya ambako aliishakubalika!
Kila himaya ina mfalme wake, kubadili mambo
lazima uonyeshe kipya ulichonacho. Sserunkuma ndiyo ana uwezo na ana uwezo wa
kufanya makubwa, lakini lazima ajipange, ajitume na kuwa mbunifu pia aache
longolongo, acheze soka la sivyo, Bongo
kutamshinda na ataondoka watu wakiwa hawana lolote litakalofanya
wamkumbuke.
dah mkuu umeshuka nondo sana ila sioni kibofyo cha Like
ReplyDeletedah mkuu umeshuka nondo sana ila sioni kibofyo cha Like
ReplyDelete