Straika wa kimataifa wa Yanga, Amissi Tambwe, ambaye msimu uliopita alikuwa Simba, jana
Jumapili alizua jambo kwenye Mkutano Mkuu wa Klabu ya Simba uliofanyika kwenye
Bwalo la Polisi, Oysterbay jijini Dar.
Uongozi wa
Simba ulikutana na wanachama katika bwalo hilo kwa ajili ya kujadili mambo
mbalimbali yanayoihusu timu yao, yakiwemo mwenendo wa timu, suala la uwanja na
ukata.
Hata hivyo,
wakati mkutano huo ukiendelea, jina la mchezaji huyo aliyefungashiwa virago na
nafasi yake kuchukuliwa na Mganda, Simon Serunkuma lilitajwa na rais wa klabu
hiyo, Evans Aveva alipokuwa akizungumzia mwenendo mbovu wa timu hiyo kwenye
ligi kuu.
Alisema
baada ya kuingia madarakani, walikuta kikosi cha timu hiyo kikifundishwa na
Mcroatia, Zdravko Logarusic, lakini wakaachana naye kutokana na kutokuwa na
maadili mazuri kwa faida yao na kuamua kumchukua Mzambia, Patrick Phiri.
“Sababu
kubwa iliyosabibisha tukamchukua Phiri ni rekodi yake ndani ya Simba lakini
baada ya mambo kwenda kinyume na tulivyotarajia, tukaamua kuachana naye na
kumchukua huyu wa sasa (Mserbia, Goran Kopunovic).
“Hata hivyo,
huyohuyo Phiri ndiye aliyependekeza tumuache Tambwe kwa madai kuwa hakuwa na
sifa za kuitumikia Simba na sisi tulifanya hivyo bila ya kujua kwa sababu yeye
ndiye alikuwa mtaalamu wetu, ikabidi tufuate mapendekezo yake.
“Lakini hayo yote yameshapita isipokuwa kwa
sasa tunaomba tuwe wavumilivu na tuendelee kumpatia muda Kopunovic, kwani ni
matumaini yetu atatufikisha mbali kutokana na mafanikio mafupi tuliyoyapata
baada ya kuanza kuifundisha timu yetu,” alisema Aveva.
Kauli hiyo
ya Aveva kuhusu Tambwe iliwasikitisha baadhi ya wanachama waliokuwa katika
mkutano huo na kufikia hatua ya kuutupia lawama uongozi huo kwa kukubali mapendekezo
ya Phiri na matokeo yake wakawanufaisha wapinzani wao wa jadi, Yanga ambapo
nyota huyo kwa sasa amekuwa mtu hatari kwa kufumania nyavu.
Tambwe
tayari ameshaifungia Yanga mabao manne kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho
na ligi kuu msimu huu.
0 COMMENTS:
Post a Comment