Na Saleh Ally
OKTOBA 28, 1998 beki John Terry akiwa kinda
aliingia uwanjani kuichezea Chelsea mechi yake ya kwanza ikipambana na Aston
Villa katika mechi ya Kombe la Ligi.
Miaka 10 baadaye, ilikuwa 2008, Terry akawa
adui baada ya kuteleza na kukosa penalti ya mwisho katika fainali ya Ligi ya
Mabingwa Ulaya mjini Moscow, Urusi dhidi ya Manchester United.
Maisha yanasonga, mengi yanapita lakini kibaya
kinaweza kubadilika na kuwa kizuri kama mhusika anajitambua. Hakuna anayeweza
kukataa kwamba kweli Terry maarufu kama JT sasa ni shujaa wa Chelsea.
Beki ambaye atakumbukwa, nahodha ambaye atakuwa
gumzo kwa kipindi kirefu baada ya kustaafu. Sasa anasonga ukiongoni akiwa na
miaka 34, lakini anaendelea kuibebesha Chelsea vikombe na mikono yake ndiyo
mpokeaji mkuu.
Alianza kujihakikishia namba katika kikosi cha
Chelsea katika msimu wa 2000-01, alipocheza mechi 23 zote akianza. Msimu
uliofuata akawa tegemeo akishirikiana na Marcel Desailly na Desemba 5, 2001,
rasmi akakabidhiwa unahodha.
Miaka 14 sasa tokea amekuwa nahodha wa kikosi
cha Chelsea, tayari JT ana makombe 14 mkononi mwaka aliyoshinda akiwa na klabu
yake hiyo ya Chelsea.
Hauwezi ukamzungumzia JT bila ya utukutu na
kashfa lukuki, mwaka 2002 akizichapa na baunsa, wakamchangia na mwisho
akapandishwa kizimbani. Miezi michache baadaye akakutana na kashfa nyingine ya
kumdhalilisha mtalii wa Kimarekani, ikawa kesi nyingine.
Usisahau, JT aliingia katika kashfa ya kutembea
na mpenzi wa mshikaji wake kitambo, beki Wayne Bridge. Hiyo haitoshi, akambagua
Anton Ferdinand na kusababisha ugomvi mkubwa kati yake na aliyekuwa mshikaji
wake, Rio Ferdinand.
Kwa kifupi, JT ni mtukutu hasa lakini unaporudi
kazini, JT ni kati ya mabeki bora zaidi England hadi msimu huu kwa kuwa Chelsea
inapambana kupata ubingwa wa Ligi Kuu England na kama itashinda, atakuwa
amebeba kombe la 16.
Maana yake JT tayari ameweka rekodi mpya katika
mikono yake ya unahodha wa miaka 14 na makombe 15 aliyoyashika.
Nani anaweza kusema JT hajitumi, si mbunifu au
si makini? Ubora wa kazi zake unafuta makosa na utukutu wake wote na ndivyo
binadamu wanavyoishi, kwamba wakati mwingine vizuri kuangalia katika mazuri ya
mtu kuliko kujali zaidi makosa.
Makombe la Ligi ya Mabingwa, Europa, Ligi Kuu
England, FA, Kombe la Ligi na mengine. Mchezaji yupi wa nyumbani Tanzania
anawaza atakuwa amefanya nini wakati soka lake litakapokuwa limefikia ukingoni?
Inawezekana kukawa na tofauti kubwa kati ya Ibrahim Ajibu wa
Simba na JT. Kweli kinda huyo wa Simba, ndoto yake kuwa na gari kali
ikiwezekana nyumba pia, lakini mafanikio makubwa yanajenga kila kitu na gari na
nyumba, zenyewe zinamfuata, tena anachagua.
Mchezaji yupi kinda au anayefanya vizuri wa Yanga, Azam FC,
Coastal Union na kwingine anayeamini kama mafanikio hayajakaa vizuri katika
timu anayochezea, anaweza kutoka nje ya Tanzania na kubadilisha mambo? Alipo,
ndipo alipo na amefika! Vipi atafikia alipofikia JT?
Wachezaji nao ni mashabiki, kazi yao kusifia vinavyofanywa na
wenzao wakati wao hawafanyi lolote. JT angeweza kufanya hivyo, lakini hawezi
kwa kuwa alikuwa anataka kufanya zaidi ya alivyotaka kufanya. JT tayari ana
makombe hayo 15, anatafuta la 16. Wewe je?
MAKOMBE NA KLABU:
3 – Ligi Kuu England: 2004–05, 2005–06, 2009–10
5 - FA Cup: 1999–00, 2006–07, 2008–09, 2009–10, 2011–12
3 – Kombe la Ligi: 2004–05, 2006–07, 2014–15
1 – Ligi ya Mabingwa Ulaya: 2011–12
1 - Europa League: 2012–13
2 – Ngao ya Jamii: 2005, 2009
VIKOMBE BINAFSI:
1 – Mchezaji wa mwaka wa PFA: 2004–05
3 – Mchezaji katika kikosi cha mwaka cha PFA: 2003–04, 2004–05,
2005–06
2 – Mchezaji wa mwaka Chelsea: 2001, 2006
1 – Ndani ya kikosi Bora cha Kombe la Dunia: 2006
5 – Mchezaji bora wa FIFPro World XI: 2005, 2006, 2007, 2008,
2009
3 – Beki bora wa klabu wa UEFA: 2005, 2008, 2009
4 – Timu bora ya mwaka ya UEFA: 2005, 2007, 2008, 2009
0 COMMENTS:
Post a Comment