Na Saleh Ally
JUMAPILI ijayo ndiyo siku ambayo
makocha wawili wa Yanga na Simba wanaweza wakawa wanatamani isifike au ipite
wakiwa wamelala.
Hans van Der Pluijm wa Yanga na Goran
Kopunovic wa Simba, kila mmoja anajua ana kazi ngumu kupita zote kwa kuwa timu
zao zinakutana.
Yanga inakutana na Simba ikiwa inataka
ushindi kwa mambo mawili, kwanza kujiongezea heshima na kulipa kisasi kwa Simba
ambao wamekuwa ‘wakiwadharau’ kila wanapokutana nao.
Simba wanajua, hali yao ni mbaya na
pointi tatu ni muhimu kupita kiasi. Tena mechi inakuja baada ya ushindi wa
mabao 5-0 dhidi ya Prisons na kumalizika kwa mkutano mkuu uliokuwa na mikakati
kibao.
Wanachama wa Yanga wanahitaji ushindi,
mashabiki watafurahi kuona Mnyama kaanguka. Lakini pia Mwenyekiti wa Yanga,
Yusuf Manji, angetaka kumaliza ‘kuonewa’ na Simba huku yule wa Simba, Evans
Aveva angetaka kuonyesha kweli ni kiboko ya Yanga kama anavyoaminika alipokuwa
kiongozi wa Friends of Simba (Fos).
Presha zote mwisho zinawaangukia
makocha hao wawili ambao mapigo yao ya moyo yatakuwa yanazidi kupanda kwa wiki
nzima ya maandalizi ya mechi hiyo.
Kuanzia jana, siku saba kamili, saa
168 ngumu kwa makocha hao, hakuna ubishi hawatakuwa na usingizi wa pono kwa
kuwa mipango na presha ya ushindi itakimbiza usingizi wao.
Kila upande unataka ushindi, makocha
wote wanalijua hilo. Hatari yake ushindi unatakiwa kuwa kwa timu moja,
ikishindikana ni sare ambayo hakuna anayeitaka.
Kopunovic:
Atakuwa anafurahia ushindi wa mabao
5-0 dhidi ya Prisons, lakini Jumapili ni siku ambayo hajawahi kuiona katika
maisha yake akiwa kocha.
Amefundisha nchini Rwanda akiwa na
Polisi, halafu Vietnam alipokuwa kocha wa Long Don Tam.
Jumapili atashuhudia umati wa mashabiki
wengi zaidi. Lakini presha itakuwa juu kuliko zote ambazo amewahi kuwa nazo.
Huenda ile tabia yake ya midadi
inaweza ikazidi kwa kuwa atatamani kuona timu yake inashinda na asipofanikiwa,
basi ni kazi kwake.
Simba na Yanga wanapokutana ni presha
kubwa, kocha anachotakiwa ni kushinda tu na hakuna mjadala mwingine.
Pointi 23 za Simba baada ya ushindi
dhidi ya Prisons, iwapo watashinda dhidi ya Yanga watafikisha 26 na kuwa
wanazidiwa tano tu na Yanga yenye 31.
Hiyo inaonyesha presha kubwa zaidi kwa
Kopunovic na kikosi chake kwa kuwa wanajua iwapo watapoteza, pamoja na kupoteza
furaha ya mashabiki, Yanga itafikisha 34 na kuwazidi kwa tofauti ya pointi 11, huku
ikiwa na mchezo wa kiporo.
Pluijm:
Mholanzi Pluijm anaijua presha ya
mechi hiyo, ingawa amefundisha nchini Ghana lakini aliona utofauti wa Yanga na
Simba.
Pointi 31 ni nzuri kwake, zinaifanya
Yanga kukaa kileleni lakini kuiruhusu ishinde dhidi yake ni kuiacha Simba isogee
kwa tofauti ya pointi moja mgongoni mwao, si kitu sahihi.
Pia presha kubwa ni kwamba pamoja na
Simba kuonekana haina kikosi imara, bado imekuwa ikiendelea kuinyanyasa Yanga
inavyotaka.
Ushindi wa Yanga kwa Simba imekuwa ni
sare. Kwa kikosi alichonacho, kushindwa kuifunga Simba, kibarua chake kitakuwa
rehani.
Simba ina kikosi lakini si cha
kudharau hata kidogo kwa kuwa kina wachezaji wanaoweza kubadili matokeo kwa
uwezo wao binafsi.
Angalia Emmanuel Okwi, Danny
Sserunkuma, Ibrahim Ajibu, Ramadhani Singano na wengine. Lakini Yanga bado ina
wachezaji wengi wazoefu na wenye uwezo wa juu.
Hivyo presha ni kubwa zaidi kwa Pluijm
ambaye analijua hilo na atapambana kuhakikisha anashinda.
Tatizo la Yanga, inatengeneza nafasi
nyingi za kufunga lakini haizitumii. Kama itafanya hivyo mbele ya Simba, basi
itajiponza.
Tena wachezaji kama watafanya hivyo,
kuna uwezekano mkubwa wa kukutana na kashfa kwamba wamepewa ‘mlungula’ ili
wasifunge wakati wamekuwa wana tatizo katika mechi kibao zilizopita na mfano
mzuri ni zile mbili dhidi ya BDF XI jijini Dar es Salaam na kule Lobatse.
0 COMMENTS:
Post a Comment