Na Saleh Ally
HAKUNA anayejua nani atafunga kwa upande wa
Yanga au Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam, kesho Jumapili.
Lakini ni rahisi kusema Mrisho Ngassa, Simon
Msuva kwa Yanga au Emmanuel Okwi na Ibrahim Ajibu ‘Kadabra’ watafunga kwa
Simba.
Wako unaoweza kuona hawana lolote, lakini
haupaswi kuwadharau kwa kuwa wakati mwingine mechi za watani, wafungaji ni wale
usiowatarajia.
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ni hatari kwa Simba
sababu ya vichwa, hali kadhalika awe Joseph Owino au Juuko Murshid, Waganda hao
pia ni wazuri hewani, Yanga wachunge.
Hata hivyo, bado hauwezi kuwadharau wachezaji
wafuatao kwamba wanaweza kucheka na nyavu kesho;
Yanga:
Tambwe:
Huenda akataka kumaliza kiu yake kesho, lakini
unajua Amissi Tambwe ni mjanja na huenda ndiye mtu ambaye Simba wanapaswa
kumuangalia sana ndani ya 18. Wako walioamini kweli ameisha, wameanza kuona
tofauti.
Kichwa chake ni silaha zaidi ya bunduki.
Anajua kukitumia hata akiwa kwenye kasi na shingo yake kama feni, inakata kona
na kumaliza kazi. Wamchunge.
Tegete:
Jerry Tegete hajafikisha miaka 30,
ameishafunga Simba mabao matano. Ana mechi saba haijaifunga Simba. Lakini
akipewa nafasi, Simba wasidhani amesahau kufunga, ng'ombe hazeeki maini,
atawazuru kwa kuwa ufungaji wake ni kipaji.
Javu:
Huyu jamaa ni mzuri, Simba wanamkumbuka akiwa
Mtibwa Sugar. Uwezo wake wa kufunga uko juu sana na Kocha wa Yanga, Hans van
der Pluijm akimpa nafasi, basi Simba lazima wajue hatari iko mbele yao kwa kuwa
anapiga mashuti, si muoga na ana uwezo mkubwa wa kulenga.
Mrwanda:
Hata iweje, uzoefu utambeba. Anajua wakati
gani afunge au abadili njia. Tayari ana bao moja dhidi ya Simba msimu huu
wakati akiwa Polisi Moro, walioliona lile bao watakumbuka alitumia ustadi
mkubwa kuuwahi mpira na kufunga. Kwa pasi za kiungo Haruna Niyonzima, Simba
wanapaswa kuwa makini na ubora wa umaliziaji wa Daniel Mwarwanda ‘Mrwanda’.
Sherman:
Tayari anaonekana hafai, hajafunga tokea aanze
kuchezea Yanga. Lakini iwapo atakutana na mipira ya chini karibu na lango la
Simba, ubora wake ni mzuri katika umaliziaji.
Amekuwa msumbufu asiyefunga, lakini atakuwa
anajifunza kila kukicha kuhusu soka ya Tanzania. Hivyo lazima ataonyesha
mabadiliko na anajua, Yanga wanataka afunge na siku nzuri ni kesho.
Simba:
Awadh:
Unamjua, unaweza kusema ana bahati na mechi za
watani, pia ana juhudi. Awadh Juma amefunga mechi zote za Mtani Jembe, maana
yake anaweza kufanya hivyo kesho kwa kuwa atakuwa na kiu ya kufunga na hata
uoga hana.
Awadhi si mchezaji mwenye mbwembwe, huenda
usimuone hadi katika tukio husika. Mjanja, ana nguvu halafu ni ‘mapafu ya mbwa’
na anapopaka nafasi, asilimia 80 anaitumia.
Sserunkuma:
Danny Sserunkuma ni mjanja, mzoefu na mwepesi
wa maamuzi. Mechi ya kesho anaweza kutoa pasi ya bao au kufunga mwenyewe na
hiyo ndiyo sababu kuu kwamba ni vigumu kukabika, haujui atafanya nini mwisho.
Anapoingia katika eneo la 18, anakuwa mtulivu
kuliko kobe na hiyo ndiyo presha kubwa kwa mabeki. Ndugu yake Simon Sserunkuma
kama atacheza au kuingia, pia ni hatari kwa kuwa mwepesi wa maamuzi na ana
uwezo wa kupiga mashuti na pasi za mabao.
Maguri:
Elius Maguri si mchezaji mwenye uwezo mkubwa
wa soka la kuvutia, lakini ni ‘mnyama’ ambaye anataka kutikisa nyavu hata mara
tano katika mchezo mmoja. Ana nguvu, hachoki na kiwango chake cha juhudi kiko
juu.
Akianza, Kelvin Yondani na Nadir Haroub ‘Cannavaro’
lazima wawe makini kwa kuwa katika Nani Mtani Jembe aliwafunga bao lililowaacha
wakiwa wamezubaa, alipiga mpira, ukagonga mwamba, kabla hawajafika akauwahi na
kufunga. Maana yake katika umaliziaji, ni mwepesi zaidi.
Ndemla:
Kinda ambaye alionyesha uwezo mkubwa katika
michuano ya vijana Ujerumani. Said Ndemla aliingia katika mechi dhidi ya Yanga
Oktoba 20, 2013 na kuisaidia Simba kusawazisha mabao yote matatu baada ya
kwenda mapumziko ikiwa haina kitu.
Mwepesi, anajua wapi pasi yake iende kabla
mpira haujamfikia, lakini ana uwezo wa kukatisha na mpira katikati ya uwanja
akiwapita mabeki. Usisahau ni mzuri kwa mashuti.
Singano:
Moja angalia krosi zake, mbili usumbufu wake
kwa mabeki. Lakini katika ufungaji, anaweza kuwa katika tano bora ya ufungaji.
Inapofikia anatakiwa kuutupia mpira wavuni, hutulia kama dereva wa kijiko
aliyekiendesha kwa miaka 30, hana hofu.
Beki Mbuyu Twite ni bora kwa ukabaji, Singano
aliwahi kumkalisha chini. Maana yake ana uwezo wa kumpita beki yeyote kesho.
Pia ni mzuri wa pasi za mwisho.
0 COMMENTS:
Post a Comment