March 25, 2015


Na Saleh Ally
YANGA inaongoza Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 37 baada ya kucheza mechi 18 huku ikiwa inafuatiwa na Azam FC yenye pointi 36.


Hesabu zinaonyesha Yanga inahitaji kufikisha pointi 58 ambazo zitaipa ubingwa kwa uhakika bila kujali Azam FC imeshinda au kupoteza ngapi.

Tofauti hiyo ya pointi moja dhidi ya mabingwa hao watetezi huku kila timu ikiwa imebakiza mechi nane inaifanya Yanga kuwa na presha kwa kuwa kama ikiteleza, tena katika hatua za mwisho, basi imekwisha.

Azam FC tayari inajua utamu wa Ligi Kuu Bara, imeutwaa kwa mara ya kwanza msimu uliopita. Lazima inataka kuutwaa kwa mara nyingine tena na haiko mbali sana na kutimiza ndoto zake.

Mfano, Yanga ikipoteza mechi moja, Azam ikashinda moja, itaivuka kwa pointi mbili na baada ya hapo yenyewe ndiyo itaanza kufanya kazi ya kuifukuza Azam tena.

Kocha Hans van Der Pluijm analijua hilo, kwamba hakuna wakati hata chembe wa kuruhusu hata kosa dogo kwa kuwa wakifanya hivyo, basi wamekwisha.

Kosa dogo linaweza kuwa baya zaidi na mara nyingi kosa linaloonekana dogo, ndilo husababisha hasara kubwa.

Yanga imebakiza mechi nane dhidi ya JKT Ruvu ambayo inachezwa leo na ndiyo itakuwa hesabu ya kwanza ya Yanga kuhakikisha inashinda ili kuweka pointi tatu kipindoni.

Iwapo itashinda mechi ya leo, Yanga itaanza kupiga hesabu ya pointi 21 baada ya kubakiza mechi saba mbele yake ingawa hakuna ubishi mechi tano katika nane ndizo muhimu zaidi na zinaweza kuipa Yanga ubingwa.

Mechi hizo ni dhidi ya JKT Ruvu, Coastal Union, Mbeya City, Polisi Moro, Stand United, Ruvu Shooting, Azam FC na Ndanda ambayo itakuwa mechi pekee ya ugenini, kwa maana ya itakayochezwa nje ya Jiji la Dar.

Mechi sita za mwanzo ni dhidi ya JKT Ruvu ambayo ni leo, Coastal Union, Mbeya City, Polisi Moro, Stand United na Ruvu Shooting na zote zinachezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, uwanja ambao Yanga imeuzoea na ina nafasi ya kucheza soka lake.

Ili kujihakikishia ubingwa, lazima Yanga ishinde mechi hizo sita, la sivyo itakuwa katika presha kubwa ambayo inaweza kuwa tatizo.

Presha:

Unapokuwa unawania kitu ambacho pia kinawaniwa na mwingine, kawaida presha hutawala. Iwapo Yanga itapunguza presha basi itakuwa katika nafasi nzuri ya kufanya maandalizi yake ya mechi zijazo kwa mipangilio bora.

Ili kuwe hakuna presha, Yanga ishinde mechi hizo sita. Mechi yake ya saba itakuwa ni dhidi ya Azam FC ambayo siku hiyo inaweza kuwa mechi mwamuzi.

Azam
Iwapo Yanga itakuwa imeshinda mechi sita za mwanzo, itakuwa na nafasi nzuri ya kufanya uamuzi wa ubingwa itakapokutana na Azam FC kwa kuwa haitakuwa na presha tena.

Itacheza vizuri mechi hiyo na kama itashinda, basi itakuwa imejihakikishia ubingwa au kusubiri sare au ushindi mmoja kabla ya kutawazwa ufalme.

Kama Yanga itashinda mechi zote sita, itakuwa na pointi 55, Azam ikishinda zote sita itakuwa na 54. Iwapo Yanga itaibuka na ushindi siku hiyo itakuwa na 58.

Pointi 58 ndiyo hakika kwa ubingwa kwa Yanga, kwani baada ya mechi hiyo dhidi ya Azam, itakuwa imebaki mechi moja kwa kila timu na hata Azam FC ikishinda, haitaweza kuzifikisha pointi 58.

Ligi Kuu Bara ni ngumu kuliko ilivyokuwa katika misimu mingine kumi iliyopita. Hakuna timu inaotabirika kwamba ni laini au inafungika kirahisi. Hivyo hakuna mechi itakayokuwa rahisi kwa Yanga au Azam FC.

Pamoja na ugumu huo, mechi sita kati ya nane ilizobakiza Yanga, zikichezwa vizuri ndiyo jibu la ubingwa. Ikizichezea badala ya kuzicheza, basi itakuwa imepoteza, hakuna mjadala.



MSIMAMO…

                                   P         W           D         L         F         A         GD        PTS
1. Yanga                  18         11         4         3         25         10         15         37
2. Azam                  18         10         6         2         25         12         13         36
3. Simba                  20         8         8         4         25         14         11         32
4. Kagera                  19         6         7         6         16         17         -1         25
5. Coastal                  20         5         9         6         14         14         0         24




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic