April 17, 2015



Na Saleh Ally
JUMAMOSI itakuwa siku ambayo Chelsea inaanza kupata majibu rasmi kuhusiana na kutwaa au kutokutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England.


Inakutana na Manchester United ambayo itakuwa ugenini. Kwa Chelsea kila pointi tatu ni muhimu kuliko jana, lazima ishinde ili kuweka vizuri hesabu zake za kutwaa ubingwa.

Huenda mechi tatu zinazofuata zitakuwa ngumu zaidi kwa Chelsea, ikishinda zote, basi hakuna timu inayoweza kusogea na kuisimamisha kuwa bingwa.

Ina pointi 73 kileleni, ikifuatiwa na Arsenal yenye 66 na Man United iliyojikusanyia pointi 65. Mambo yamebadilika, Arsenal na Man United zilizoanza kwa kusuasua, zimebadilika na zipo kwenye kundi la zinazowania ubingwa. Manchester City imeonekana kupotea njia.


Chelsea inatakiwa kuipiga Man United Jumamosi, iimalize Arsenal, Aprili 26 na baada ya hapo iwafumue Leicester, Aprili 29 na itakuwa imefikisha pointi 81.

Arsenal ikishinda mechi zake zilizobaki itabeba pointi 18, ila kama itakuwa imepoteza dhidi ya Chelsea itakuwa imebakiza pointi 15 inazogombea na ikizipata zote, idadi ya jumla ya pointi itakuwa 81. Kumbuka Chelsea bado itakuwa na mechi nne mkononi.

Hivyo, hesabu za ushindi wa mechi tatu zinazofuatana ndiyo zitakazoihakikishia Chelsea ubingwa. Inakutana na timu mbili zinazowania ubingwa au nafasi ya pili na moja Leicester inayopambana kuokoa ‘roho yake’ ili ibaki ligi kuu, haitakuwa kazi rahisi.

Mechi hizo tatu huenda ndiyo zikawa ngumu zaidi kwa Chelsea. Iwapo ikishinda hizo, inaweza kuwa na uhakika hata wa kuchukua ubingwa kwa sare tu katika mechi nne zilizobaki.

Kwa jumla Chelsea inabidi kupambana na timu makundi matatu tofauti ili kuwa bingwa. Kundi A, lina Man United na Arsenal zinazowania ubingwa pia. Kundi B lina timu moja tu ya Liverpool inayotaka kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya au Ligi ya Europa.

Kundi C, lina timu tatu zinazopambana kujiokoa kuteremka daraja ambazo ni Leicester, West Brom na Sunderland.

Haiwezi kuwa kazi rahisi lakini pia haitakuwa kazi rahisi kuiangusha Chelsea ambayo itakuwa na mipango mingi ya uhakika mwishoni. Kocha Jose Mourinho lazima ataendelea na mfumo wake uleule, bora sare kuliko kupoteza.

Anajua sare dhidi ya Man United na Arsenal, bado itakuwa faida kwa kuwa kama amepoteza pointi nne dhidi ya timu hizo, nazo zitakuwa zimepoteza pointi mbili kila moja hivyo kufanya msimamo uendelee kubaki kama ulivyo dhidi yao.

Kikosi cha Chelsea kina wachezaji lundo waliowahi kubeba ubingwa wa England na nchi nyingine mbalimbali. Mourinho pia ni mzoefu na akishinda haitakuwa mara yake ya kwanza kuchukua ubingwa England. Hivyo hesabu atakazofanya, haziwezi kuwa ndiyo anazifanya kwa mara ya kwanza.

Bado inawezekana kabisa kipindi hiki kikawa ni cha Chelsea kutoonyesha soka la kuvutia sana, badala yake ni kuhakikisha wanalinda sana na kufunga mabao ili wapate pointi tatu. Kwao ushindi ni muhimu hata kama ni wa bao 1-0.


MECHI 7 ZILIZOBAKI:
Apr 18
Chelsea Vs Man U

Apr 26
Arsenal Vs Chelsea

Apr 29
Leicester Vs Chelsea

Mei 3
Chelsea Vs C. Palace

Mei 10
Chelsea Vs Liverpool

Mei 18
West Brom Vs Chelsea

Mei 24
Chelsea Vs Sunderland





0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic