KUNA jambo moja, linaweza lisiwe geni sana kwa wengine
lakini mimi lilinivutia na kuona ni wakati mzuri sana ninaweza kulizungumzia,
tukalijadili kwa pamoja.
Lengo langu ni kutaka muone namna gani tunavyoweza kuwa
tofauti upande wa makosa, hasa linapofikia suala la utaifa.
Najua mashabiki wengi wa Yanga hawawezi kuishangilia
Simba inapokuwa na majukumu ya kitaifa. Hali kadhalika, mashabiki wa Simba,
hawawezi kufanya hivyo kwa Yanga.
Kila mmoja ana itikadi zake, mwingine anasema kuizomea
Yanga ni raha yake, mwingine kuishangilia ni mwiko na mengine mengi lakini linapofikia
suala la utaifa, kuna kila sababu ya kubadilika.
Etoile du Sahel wameamua kwa pamoja, kukodi ndege moja
na kikosi kingine cha Esperance ili kwenda Sudan na kuja Tanzania kwa ajili ya
mechi mbili zilizo chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Esperance wanashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika,
wanakwenda Sudan kupambana na El Merreikh walioitoa Azam FC na baadaye wakaing’oa
Kabuscorp ya Angola, haitakuwa mechi rahisi.
Etoile wanakuja nchini kupambana na Yanga katika mechi
yao ya kwanza ya Kombe la Shirikisho. Pia wameitoa Benfica ya Angola wakati
Yanga iliitoa FC Platinum ya Zimbabwe.
Etoile waliitoa Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika
mwaka 2009 kwa kuichapa mabao 3-0 pale Tunis, nilikuwa uwanjani. Timu hiyo
inatokea katika mji huo mkubwa na wapinzani wake wakubwa ni Club African.
Etoile inatokea katika mji mdogo wa Sousse, lakini
zinapokutana kwenye Ligi Kuu ya Tunisia, maarufu kama League 1, kumekuwa na
ushindani mkubwa baina ya timu hizo. Wakati mwingine zimekuwa zikitokea vurugu
kubwa katika mechi zinazokutanisha Etoile na Esperance.
Lakini leo wamekwea ndege moja, kwa pamoja na umoja
wakiwa marafiki wanaoweza kuzungumza lugha moja kwa kuwa wanakwenda kulitetea
taifa lao la Tunisia.
Wanakwenda nje ya mipaka ya Tunisia kama wanajeshi wa
nchi hiyo. Kama watashinda watarejea nyumbani wakiwa mashujaa wa taifa lao
wakisubiri mechi za nyumbani kumaliza kazi.
Ndege inapita Sudan kuwashusha Esperance, inapaa tena
hadi Dar es Salaam kuwasubiri Etoile. Baada ya mechi wanapitia Sudan kuwachukua
ndugu zao, wanarejea nyumbani. Huu ndiyo ulikuwa mpango uliotangazwa na klabu
zote mbili zikakubaliana.
Hata kama usingefanikiwa, nia yao ya kulitekeleza hili
imenifanya niwe na maswali kama Yanga wanaweza kupanda ndege na Azam FC kwenda
nchi fulani kupambana kwa ajili ya taifa!
Imenikumbusha jambo hili pia, kwamba je, wale mashabiki
wa Simba wanaoizomea Yanga wanajua kwamba inapigana kwa ajili yao na nchi yetu?
Hata wale ambao hawakuwahi kuishangilia Simba ilipofanya vizuri kimataifa,
kweli leo hawakumbuki na kujuta? Kwamba hawakuwa wazalendo!
Mimi sijali ni Yanga au mimi ni Simba lakini kwangu
naona siwezi kuwashangilia watu nisiowajua, wasio na faida kwangu ambao baada
ya kuifunga timu ya Tanzania wanarejea kwenda kupokelewa kwao kwa shangwe.
Ninajua, hii hata kwako kuwa tuna marafiki, ndugu au
wazazi wanaweza kuwa Yanga, sisi Simba. Au wewe Yanga, unaweza kuwa na ndugu na
marafiki wakawa ni Simba. Sasa vipi uishangilie timu inayotokea usipopajua?
Huenda kelele za kishabiki, mfano usikie shabiki wa
Yanga anasema hahitaji mchango wa Simba au sapoti, huyo anaweza akawa
amezungumza kishabiki tu lakini ukweli lazima tukubali, lazima tubadilike na
kuamini kulipenda taifa letu hakuwezi kuishia kwenye maneno tu.
Kwangu naona mtu ambaye anaona hataki kuishangilia Yanga
ikipambana na wageni, si vibaya akabaki nyumbani ili baadaye ahadithiwe
ilivyokuwa. Si sahihi kwenda uwanjani kuwavunja nguvu. Nasema hili leo kwa
Yanga, kesho iwe kwa Simba au timu yoyote inayoliwakilisha taifa. Mimi ni
mzalendo.
BIG UP MWANDISHI.
ReplyDeletelazima nikashangilie Etoile du Sahel hao yanga sipendi hata kuwatazama,..na huyo mwanahabari wao jeri muro...tutaukatana mwakani..TUSIDANGANYANE KWA HILI...WAO NDO WA KWANZA MWAKA 1993 KUIBA UZALENDO UMEWASHINDA WAKATUZOMEA PALE SHAMBA LA BIBI ...SO MUOSHA HUOSHWA
ReplyDelete