Na Saleh Ally
ZIMEBAKI mechi sita tu
Simba kukamilisha msimu wa 2014-15 na sasa zaidi inapambana kupata nafasi ya
pili angalau iondoe ugwadu wa kutoshiriki michuano ya kimataifa.
Wakati inapambana kwa kila
namna, lazima kuwe na hesabu za usajili kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake
kwa kuwa kuna mambo mengi yamejitokeza.
Mfano, wachezaji wake wa
kimataifa watano wote ni Waganda, lakini hadi sasa walioonyesha kiwango cha juu
ni wawili tu, Emmanuel Okwi na Juuko Murishid. Joseph Owino, Simon na Dan
Sserunkuma, hawakuwa sawa sana!
Kikosi kina vijana wengi,
baadhi ya wakongwe walioachwa kama Amissi Tambwe sasa ni tegemeo Yanga.
SALEHJEMBE ilifanya mahojiano maalum na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe ambaye
ni askari wa jeshi mstaafu ili aweze kuzungumzia mipango yao.
Zaidi kujua baada ya
yaliyotokea, nini hasa wamepanga kufanya kuimarisha kikosi chao.
Mpango wa awali, mnataka
kuimarisha kikosi kwa kusajili wachezaji katika nafasi ngapi?
Hans Poppe: Nafasi tatu ndiyo
nina uhakika, beki wa kati, kiungo mmoja mchezeshaji pamoja na straika mmoja.
Mengine, ni suala la kuangalia pia kusikiliza nyongeza ya mapendekezo ya mwalimu.
Dan Sserunkuma, ameonekana kushutumu kuhusiana na masuala ya
kishirikina. Taarifa zinasema aliandika barua anataka kuondoka, halafu
akabadili uamuzi. Unalizingumziaje hili?
Hans Poppe: Inawezekana
kuna mambo yanatokea na sielewi lolote. Hilo la ushirikina yeye mwenyewe
kakanusha, mimi nalielewa suala hilo tofauti. Sserunkuma aliomba ruhusa kwenda
kumuuguza mkewe, akapewa siku tatu.
Alipofika akaambiwa
anatakiwa kufanyiwa upasuaji, hivyo ilikuwa ni lazima akae zaidi. Akapiga simu
kuomba ruhusa siku zaidi, akaruhusiwa.
Unafikiri akibaki anaweza
kuisaidia Simba, au ni bora angeenda na kuwapisha Wazalendo katika nafasi yake?
Kama ni mawazo yangu
nitasema ndiyo. Inawezekana bado aina yake ya uchezaji watu hawajaielewa, ana
nguvu, mwepesi wa maamuzi na msumbufu sana kwa mabeki.
Watu lazima wajue kwamba
Sserunkuma si lazima afunge, akitoa pasi au akiwapa wengine wakafunga bado atakuwa
ni msaada kwa timu.
Nilimuona Kigali katika
Kombe la Kagame, katika mechi mbili alifunga mabao matatu, tena alitokea
benchi. Kwangu bado naamini ni mchezaji mzuri na atatusaidia.
Inaonekana kama unajitetea
kuonyesha viongozi hamhusiki na ushirikina?
Hans Poppe: (Kicheko), Zungumza
na kiongozi yoyote wa Simba atakueleza. Kwanza sijui kama wanafanya mambo hayo,
hakuna anayeweza kufanya ushirikina mbele yangu.
Siwezi kuzungumza kuhusiana
na ushirikina kwa kuwa siamini na siwezi kushiriki. Kila mtu Simba analijua
hilo kuhusiana na mimi.
Taarifa nyingine ni kwamba
Patrick Kiongera anarejea Simba, nani sasa ataondoka katika wachezaji watano wa
kigeni mlionao?
Hans Poppe: Tutakaa na
kujadili, nani anaondoka na nini cha kufanya. Kiongera ni kweli tunamrudisha
kwa kuwa hadi sasa ni mchezaji wetu na tunamlipa mshahara. Tulimpeleka Kenya
kwa mkopo ili aendelee kucheza na wao wanajua atarudi Tanzania.
Wachezaji wengi hawapendi
kutibiwa, baada ya Kiongera kuumia, bado aliendelea kulazimisha kucheza.
Tukamuambia tuliyaona hayo wakati wa Owino ambaye alichelewa kwenda kutibiwa na
hadi sasa amekuwa na matatizo ya majeruhi.
Pia Owino alitakiwa
apumzike mwaka baada ya matibabu, sisi tukakubaliana na daktari alivyoagiza
lakini Owino akaona kama anaonewa, akaamua kujiunga Azam. Siku chache kaumia,
msimu mzima akakaa nje!
Hatukutaka kurudia makosa,
ndiyo maana tulimsisitizia Kiongera lazima aende India, katibiwa na
tumemsimamia hadi alipopona na sasa anacheza. Tuliona uwezo wake, hivyo atarudi
kuja kusaidia safu ya ushambuliaji, hili halina shaka.
Wewe ndiye bosi wa kamati
ya usajili, kamati yako imemuacha Tambwe! Sasa inaonekana kama ilichekesha,
kweli mliona ni uamuzi sahihi na sasa kama mnaona haya mnatupia mzigo Kocha
Patrick Phiri?
Hans Poppe: Nafikiri leo
wakati mwafaka wa kuweka hili wazi, kwamba mimi ndiye nilisisitiza Tambwe
aondolewe. Kweli Phiri hakutamka tumuondoe, lakini alisema vitu vinavyomaanisha
kwamba hamhitaji.
Alipokuja alianza kumtumia
Tambwe katika mechi za mwanzo, baadaye akaanza kumuweka benchi anaingia dakika
za mwisho na baadaye ikawa anaingia kidogo. Nakumbuka mechi ya mwisho
alimuingiza dakika tatu za mwisho.
Nikamuita kocha na
kumuuliza vipi mfungaji bora wa msimu uliopita anaonekana kushindwa kucheza
kwake. Phiri akaniambia kwa mfumo wake mchezaji wa box (anayesubiri kufunga)
hawezi kufanya vizuri.
Kama hawezi kufanya vizuri,
pia anamuingiza mwishoni au anakaa benchi kabisa. Sasa tunastahili kuwa na mchezaji
anayekaa tu tena wa kimataifa?
Akifunga Yanga, haina maana
ni kosa kumuacha. Alishindwa ku click (kufanya vema) katika mfumo wa Phiri.
Angalia Yanga leo wana yule Mliberia (Kpah Sherman), ni mchezaji mzuri kabisa
lakini sasa mambo hayaendi vizuri.
Hivi ni vitu vinavyotokea.
Akiondoka leo Yanga anaweza kwenda kwingine akacheza vizuri na kufunga pia.
Sasa ishu ya Tambwe isituumize sana vichwa.
Tena nisisitize, hata alipofika
Yanga, bado Tambwe hakufanya vizuri hadi kocha wao (Hans van der Pluijm) alipobadili
mfumo na kuanza kutumia viungo watatu kama Simba, angalau sasa unaona
anaonekana.
Katika hili la Tambwe,
nafikiri Simba tungepongezwa kumsaidia, sasa amepata timu imeendana na uchezaji
wake. Angebaki huenda tungeua tu kipaji chake!
Sasa vipi viongozi wenzako
walisema Phiri ndiye alisema Tambwe aachwe?
Hans Poppe: Kweli hilo
silijui, ila nisisitize Phiri naye alikuwa tatizo. Alikuwa muoga wa lawama,
aliwaamini wachezaji aliowajua zamani kama Shabani Kisiga na Amri Kiemba,
unajua alidhani ndiyo walewale wa enzi zile, kumbe sivyo.
Kiemba aliboronga mechi na
Prisons. Baada ya mechi tukamuuliza alimuonaje, yaani alivyocheza, akasema
vizuri sana. Tulipomuonyesha mkanda wa video wa mechi, akasema ameshangazwa
sana kuwa aliona amehujumiwa. Ikatushangaza sana, kwamba hakumuona pale
uwanjani hadi aone tena kwenye mkanda?
Pia usisahau alikuwa hawaamini
sana vijana. Angalia Said Ndemla na Abdi Banda, alisema wapelekwe kwa mkopo
kwamba wanahitaji kukua kwanza, sikuwa nakubaliana naye.
Alipokuja Goran Kopunovic
timu ilikuwa Zanzibar, tulimpeleka na kumuacha afanye kazi yake. Mwisho umeona
leo Ndemla na Banda ni tegemeo na wanaisaidia Simba.
Kulikuwa na taarifa mmeamua
kubadilisha kocha msaidizi, Selemani Matola alikuwa anaondoka, vipi imekuwa
kimya?
Hans Poppe: Unaweza ulipita
upepo mbaya, kipindi kile kila mmoja alionekana ni mchawi! Lawama kuna fulani
tatizo mara vile.
Hakuna ambaye hakulaumiwa, hata
mimi nilionekana ni tatizo kwa kutosajili vizuri. Sasa timu ni ileile na
angalau inafanya vizuri. Kiongozi mmoja alionekana kumlaumu sana Matola,
kuamini anaharibu. Lakini sasa mambo yametulia.
Je, bado mtaendelea na
mkongwe Joseph Owino katika safu yenu ya ulinzi?
Kwangu naona Owino
ameonyesha yuko tayari kustaafu. Maana aliondoka kwa madai alifarakana na
kiongozi mmoja. Nikampigia simu na kumueleza haikuwa njia sahihi ya kuondoka,
anapaswa kukumbuka ameishi vipi na watu, akarudi.
Lakini hiyo sehemu ya
kuonyesha kwamba yu tayari kwenda. Ni mchezaji mzuri, lakini naona mwisho wake
Simba umefika. Lakini naweza kusema ni suala la subira na kukaa pamoja ili
tuone itakuwaje.







0 COMMENTS:
Post a Comment