Na Saleh Ally
USHINDI wa jumla wa mabao
5-2 dhidi ya FC Platnum ya Zimbabwe umeipeleka Yanga katika raundi ya pili ya
Kombe la Shirikisho.
Mfumo wa michuano hiyo ya
pili kwa ukubwa upande wa klabu barani Afrika ni hivi; kila mnavyozidi kupanda,
ndiyo ugumu unavyozidi kuongezeka.
Hadi jana jioni, Yanga
ilikuwa ikisubiri mshindi kati ya Benfica ya Angola dhidi ya Etoile du Sahel ya
Tunisia.
Lakini utaona ndoto ya
Yanga kuingia hatua 16 bora ya michuano hiyo ilivyo na ugumu na lazima kuwe na
mipango sahihi wakati wa maandalizi kwa kuwa si rahisi.
Yanga inahitaji dakika 360
za uhakika wa mambo ili kuingia katika hatua ya 16 bora ambayo itaanza kuchezwa
kwa mfumo wa ligi.
Dakika 360 ni mechi nne
ambazo Yanga itatakiwa kucheza, mbili wakati wa raundi ya pili na kama ikifuzu
mbili tena katika hatua ya mtoano ya mwisho.
Iko hivi, sasa Yanga itacheza raundi ya pili, itakuwa kazini
dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia. Zitakuwa mechi mbili ambazo ni dakika 180.
Baada ya hapo, inaingia katika play off round ambayo italazimika kucheza dakika
kama hizo na ukizijumlisha unapata 360.
Inajipanga vipi? Hilo ndiyo
suala muhimu kwa Yanga hata kama wakiamua kuchagua raundi kwa raundi kabla ya
kusonga.
Mfano, hesabu ziwe za
raundi ya pili ambazo ni dakika 180, wakimaliza waingie katika raundi nyingine
yenye dakika 180.
Ugumu unaonekana wazi kuwa
sasa timu zilizo katika raundi mbili zilizobaki zitakuwa zinatokea katika nchi kama
Algeria, Afrika Kusini, Mali, Tunisia, Gabon, Ivory Coast, Ghana na DR Congo.
Hii ni sehemu tosha ya
kuonyesha Yanga imefanya vema hadi sasa lakini ndiyo inaingia katika mzigo
mkubwa zaidi na inalazimika kujua imeingia hatua ambazo zinahitaji umakini
zaidi.
Hakuna hata timu moja ya
Afrika Mashariki iliyopita baada ya. Dedebit ya Ethiopia kutolewa jana na Warri
ya Nigeria, halafu Rayon ya Rwanda ikiwa nyumbani ikakumbana na kipigo kibaya
cha mabao 3-0 ikiwa nyumbani dhidi ya Zamalek ya Misri ambayo katika mechi ya
kwanza ilishinda pia kwa mabao 3-1 ikiwa nyumbani jijini Cairo.
Kuhofia si sahihi, kuchukua
tahadhari ndiyo sahihi na kuamini kuwa inaingia katika hatua ngumu zaidi ni
jambo la msingi.
Pamoja na kuandaa mambo
mengine. Yanga inatakiwa kujiimarisha kwa mipango ya ugenini. Uimara wa Yanga
katika mechi za ugenini umeonekana uko chini.
Mechi ya kwanza dhidi BDF
XI ya Botswana ilisonga mbele kwa jumla ya mabao 4-3. Nyumbani ilishinda 2-0,
ilipokwenda ugenini ikafungwa 2-1 tena baada ya kutangulia kwa bao la Mrisho
Ngassa.
Mechi ya pili dhidi ya FC
Platnum, Yanga ilianza vizuri nyumbani kwa mara nyingine kwa ushindi wa mabao
5-1. Iliposafiri hadi Zimbabwe ikafungwa kwa bao 1-0 na kufuzu kwa jumla ya
mabao 5-2.
Hesabu za Yanga inapokuwa
nyumbani ziko bomba sana. Lakini inaonekana haina ‘matairi’ ya kusafiri safari
ndefu, jambo ambalo si sahihi.
Ikiwa itakosea katika mechi
ya nyumbani. Mfano mechi ijayo ikianzia nyumbani ikapata sare au kupoteza, basi
tayari itakuwa imetoka.
Ukiangalia uchezaji wa
ugenini, Yanga imekuwa ikicheza kwa kujiamini na inawezekana hata kushinda.
Lakini ule ugonjwa umekuwa ukiwakabili hata katika Ligi Kuu Bara, kupoteza
nafasi nyingi umekuwa tatizo lisilo na ufumbuzi.
Yanga wanapata nafasi
nyingi za kufunga lakini zimekuwa na msaada mdogo kwao kwa kuwa wanafunga hadi
30% ya nafasi wanazozipata ambalo si jambo sahihi.
Ugumu unazidi kupanda,
Yanga wanalazimika kubadili mambo zaidi kwa kuwa sasa wanapanda na wanazidi
kuingia katika kundi lenye timu makini zaidi na zenye hamu kubwa ya kupata
mafanikio.
Miezi mitatu kuanzia Aprili,
Mei na Juni tayari Yanga itakuwa ina jibu sahihi imefikia wapi. Kwani Aprili na
Mei itakuwa imemaliza mechi mbili za raundi ya pili, itajua kama imefuzu.
Ikifanikiwa, itakuwa inaingia
raundi ya mwisho ya mtoano kabla ya kuingia katika makundi na mechi zake mbili zitachezwa kati ya Mei 17 na 19 halafu kurudiana
ni Juni 5 na 7.
Miezi hiyo mitatu kwa Yanga
inapaswa kuwa ni ya maisha tofauti katika mambo mengi. Ianzie kwa wachezaji
kutambua majukumu yanayowakabili lakini iende kwa makocha na viongozi kwani
maandalizi ya timu yanapaswa kuwa tofauti wakijua ugumu na umuhimu mechi hizo.
Mfano ule usajili wa
kishabiki kwa kuwa Simba wamemchukua nani, ufe. Wachezaji wajilinde, pia wajue
umuhimu wa kazi iliyo mbele yao kwa kuwa sasa Yanga inapambana kwa ajili ya
maslahi ya klabu yao, lakini kwa taifa zima la Tanzania.
0 COMMENTS:
Post a Comment