April 6, 2015



Na Saleh Ally
UNAWEZA kusema kila wakati una mfalme wake. Ndivyo ilivyo sasa katika Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA) na LeBron James.


James anayekipiga Cleveland amekuwa mchezaji anayeonyesha kiwango cha juu bila ya kuporomoka kwa kipindi kirefu.

Wakati anaondoka Miami Heat na kujiunga na Cleveland, wengi walitabiri ndiyo mwisho wake James kwa kuwa aliondoka katika timu kubwa huku wakisema ameamua kwenda kustaafu.

Lakini mwenendo wake kwa sasa, unafanya waliofikiri anakwenda kustaafu wabadili mawazo kwani amekuwa akiweka rekodi mpya kwa kuzivunja kadhaa za zamani.


Baadhi ya rekodi ambazo amekuwa akivunja ni zile alizowahi kuziweka yeye mwenyewe.

James amewahi kufunga pointi 61 katika mechi moja tu, hiyo ilikuwa ni wakati Miami Heat iliposhindwa kwa pointi 124-107 dhidi ya Charlotte Bobcats.


Si kwamba wengine hawajawahi kufunga, lakini ni nadra kutokea hivyo naye amerudia mara kadhaa kufunga pointi 50 hadi 60 katika mchezo mmoja.

Amewahi kufunga pointi 50 mara 10 katika michezo tofauti katika NBA. Amefunga pointi hizo mara nane akiwa na Cleveland Cavaliers, mara mbili akiwa na Heat.

James ndiye mchezaji aliyefunga pointi tatu mara nyingi zaidi kama utahesabu katika mechi 50 za NBA. Rekodi anayoishikilia pia ya kufunga pointi tatu mara nane katika mitupo kumi anayolenga lango.


Angalau Kobe Bryant ameonyesha naye ni mkali baada ya kuwa na rekodi ya kufunga mikwaju ya pointi tatu mara nane katika mitupo 12.

Lakini James akaweka rekodi nyingine kali zaidi baada ya kufunga mitupo yote minane ya pointi tatu aliyotupa dhidi ya Bobcats.

Mkali huyo ndiye anayeshikilia rekodi ya kufunga pointi nyingi katika robo moja baada ya kuivunja aliyoikuta.

James alifunga pointi 25 katika robo moja, akawa amevunja rekodi yake aliyokuwa ameweka ya kufunga pointi 24 katika robo moja.

Kama hiyo haitoshi, James ameweza kuvunja rekodi ya muda wote ya pasi zilizozaa mabao au asisti katika NBA.

Anashikilia rekodi ya msimu mmoja ya kutoa asisti nyingi zaidi. Msimu wa 2009-10 alitoa 651 akiwa na wastani wa 6.9 kwa mchezo mmoja.


Kwa msimu huu, tayari James ana wastani wa pointi 25.7 kwa mechi, asisti 7.3 na ribaundi 5.6.

Rekodi hiyo ilikuwa inashikiliwa na mkali Scottie Pippen aliyeng’ara sana na Chicago Bulls enzi zake.

Wakati akiitumikia Cleveland Cavaliers ikiitandika Detroit Pistons, James alitoa pasi nzuri kwa mshambuliaji Kevin Love aliyepiga pointi tatu na wao mwisho kushinda kwa 102-93.

Pippen aliweka rekodi hiyo kwa karibu miaka 10 iliyopita na kuiacha wakati anastaafu mwaka 2004 akiwa ametoa pasi zilizozaa pointi mara 6,135.

James aliyefunga pointi 19 na kutoa asisti 11 katika mechi hiyo sasa amefikisha asisti 6,142 na kubeba rekodi hiyo kwa wale wanaoendelea kucheza.

Katika NBA wakiwemo waliostaafu, James sasa ndiyo kashika nafasi ya 27 nyuma ya Jerry West mwenye asisti 6,238.

Mkali huyo ameendelea kufanya mengi licha ya kuwa amehama Heat, hali inayodhihirisha kuwa uwezo binafsi na juhudi alizonazo zinaweza kubadili mambo.

Cleveland Cavaliers sasa imekuwa tishio kwa sababu ya mtu mmoja tu. Hii inaonyesha kuwa kweli jamaa anajua na si kwa kuwa alikuwa pamoja na wengi wanaojua akiwa Heat.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic