GARCIA AKIPIGA MAHOJIANO NA SALEH ALLY |
Na Saleh Ally
LUIS Garcia Sanz ni kati ya wachezaji wenye
kumbukumbu nyingi ndani ya klabu ya Liverpool ya England, pia Barcelona ya
Hispania.
Luis Garcia tayari yuko nchini kwa ajili ya
kujiandaa na mechi dhidi ya nyota wa Tanzania itakayochezwa Jumamosi wenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, yeye akiwa katika kikosi cha wakongwe wa
Barcelona.
Wakongwe hao watacheza dhidi ya nyota wa
Tanzania waliowahi kuwavaa wakongwe wa Real Madrid.
AKISHANGILIA NA RONALDINHO |
SALEHJEMBE, imefanya mahojiano maalum na Garcia ambaye pamoja na kuahidi kuonyesha mambo ya uhakika
hiyo Jumamosi, amejibu maswali lukuki ambayo wengi wangependa kujua.
Anajulikana kwa mafanikio makubwa wakati
akiichezea Liverpool kuanzia mwaka 2004 hadi 2007 alipoamua kurejea Hispania na
kujiunga tena na Atletico Madrid.
Garcia anasema mechi zake 121 akiwa na
Liverpool aliyoifungia mabao 30, zinajenga mapenzi ya dhati na kamwe hatoacha
kuipenda timu hiyo ya England hadi mwisho wa maisha yake.
AKISHANGILIA BAADA YA KUFUNGA BAO WAKATI AKIKIPIGA LIVERPOOL. |
Katika miaka minne ya Liverpool, walibeba
mataji matatu, moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Tena katika miaka hiyo wakafika
fainali ya Ligi ya Mabingwa mara mbili, si kitu kidogo.
Anasema mashabiki wa Liverpool wamekuwa
wakiendelea kuimba na kumsifia hadi leo hata wanapokwenda kucheza mechi za Ligi
Kuu England, jambo linalomfanya aamini Anfield ni nyumbani kwake milele.
Maisha yake ya soka linalotambulika yalianzia
Barcelona B mwaka 1997, lakini ana mengi ya kuyakumbuka England likiwemo lile
bao maarufu kama “Ghost Goal” alilofunga katika mechi dhidi ya Chelsea.
Kocha Jose Mourinho ndiye alilitoa jina la
“Ghost Goal” akionyesha kupinga kwa kuwa mpira haukuvuka msitari. Lakini
mwamuzi hakuona na kuonyesha kati, jambo lililomuudhi sana Kocha huyo Mreno
huyo.
AKISHANGILIA BAADA YA KUWAFUNGA CHELSEA "GHOST GOAL" |
“Mourinho alikasirika sana, lakini baada ya
mchezo alikuja na kunipongeza kwa mchezo mzuri siku ile ila hakuzungumzia
kabisa kuhusiana na bao hilo,” anasema Garcia katika mahojiano na gazeti hili
jijini Dar, jana.
“Nimekutana na Mourinho mara kadhaa baada ya
mechi ile, hakuwahi kukumbushia tena ingawa kwingine alilalamika sana.”
AKIFUNGA MBELE YA JOHN TERRY |
Wimbo wake:
Kwake anaona ushindi au kufunga bao ilikuwa
moja ya kazi yake kubwa kwa kikosi cha Liverpool.
Mashabiki wa Liverpool, wanaonyesha
kuyakumbuka mazuri yake kwa kuendelea kuimba wimbo wake maalum wa “You’re my
sunshine”.
“Nilifanya kazi nzuri, mashabiki hadi leo
wanapoimba maana wana furaha na mimi. Marafiki na ndugu wamekuwa wakinieleza
kuhusu wimbo huo na mashabiki wengine kupitia mitandao kama Twitter wamekuwa
wakinieleza hilo. Ni Jambo la kujivunia, inanipa furaha sana.”
AKISHANGILIA NA XAVI... |
Mashabiki wa Liverpool waliwahi kumpa nafasi
ya 34 katika wachezaji 100 waliowahi kuichezea Liverpool.
Nafasi hiyo aliipata kutokana kura
zilizopigwa na mashabiki hao wa Liverpool na hiyo ni sehemu ya kuonyesha kuwa
ye ni kati ya vipenzi wa Liverpool.
Kipigo Arsenal:
Mechi yake ya mwisho Liverpool alikutana na
kipigo cha mabao 6-3 dhidi ya Arsenal katika mechi ya Kombe la Ligi.
Garcia anasema ni kipigo ambacho hatakisahau
kwa kuwa walikuwa nyumbani na Arsenal wakawaadhibu vibaya. Mbaya zaidi ilikuwa
mechi yake ya mwisho.
Siku chache baadaye Liverpool wakatangaza
aliumia na alitakiwa kukaa nje miezi sita. Ajabu, wakatangaza tena anakwenda
Atletico Madrid ambako mwaka huohuo wa 2007 akaanza kucheza!
“Kidogo iliwashangaza mashabiki wa
Liverpool, najua walipenda nibaki. Kweli niliumia, lakini mimi ndiye nilifikia
uamuzi wa kurudi Hispania na kujiunga na Atletico Madrid ambayo niliondoka
mwaka 2003 na kujiunga na Racing Santander. Ulikuwa ni uamuzi, kwamba narudi
kucheza nyumbani Hispania:
Torres:
Kuondoka kwake kurejea Atletico Madrid, ilielezwa
kuwa mwanzo wa uhusiano kwa klabu hiyo uliosaidia Liverpool kumpata Fernando
Torres.
“Kweli ilisaidia, mazungumzo yalianza baada
ya Rafa Benitez kwenda Liverpool. Lakini uhamisho wangu ulikuwa chanzo uhusiano
mzuri kwa klabu hizo.
“Lakini kazi yangu nzuri pia ilichangia
imani kwa Liverpool na wachezaji kutoka Hispania,” anasema Garcia.
Mshambuliaji huyo aliyekuwa akiujua mpira
vema, aliamua kustaafu soka alipotangaza rasmi Januari 14, 2014.
“Kweli nilitangaza siku hiyo yenye namba 14
mara mbili. Hiyo ndiyo ilikuwa namba yangu ya jezi niliyokuwa ninaipenda sana.
“Ilikuwa ni siku mwafaka kwangu kutangaza
kujiuzulu, lakini baadaye nimerudi na kucheza tena soka nchini India. Sasa nina
miaka 36, katika klabu ya Atletico Kolkata ni mchezaji lakini zaidi ni
kuhamaisha.
“Ninaweza kurudi tena India, wanajitahidi
kukuza soka lao. Litafika mbali hivi karibuni,” anasema.
AKIPAMBANA NA FIGO... |
Jumamosi Taifa:
“Wanakuja wachezaji wengi, mfano Mandieta,
Deco, Sambrosa, Kulivert na wengine. Lakini tunalazimika kujiandaa kwa kuwa
tulielezwa mechi Madrid ilikuwa ngumu.
“Tumeelezwa kuhusiana na kasi yao na pia
nguvu. Tutajitahidi kucheza staili ya Barcelona na kushinda, lengo ni kushinda
ingawa tunajua haitakuwa lahisi,” anasisitiza Garcia.
Garcia amecheza na wachezaji wengi wa
kiwango cha juu, mfano Ronaldinho, Luis Enrique ambaye sasa ni kocha Barcelona.
Pia Sergio Aguero akiwa Atletico Madrid, Steven Gerrard wakiwa Liverpool na
wengine wengi.
“Wengi wanajua mpira, lakini Ronaldinho
alikuwa kitu kingine. Kila aliyecheza naye atakueleza. Ni nyota hasa wa mpira
ambaye anastahili.”
0 COMMENTS:
Post a Comment