SIKUFIKA
uwanjani katika mechi ya Ligi Kuu Bara kati ya Ruvu Shooting dhidi ya Yanga
ambayo iliisha kwa vijana wa Hans van Der Pluijm kushinda kwa mabao 5-0.
Ushindi
huo mnono wa Yanga umewaingiza katika dakika 90 tu wanazotakiwa kukamilisha
kazi ya msimu, yaani kutwaa ubingwa.
Yanga
wanashuka dimbani leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kucheza na
Polisi Morogoro na kama wakishinda, basi rasmi watatawazwa kuwa mabingwa wapya.
Nikiwa
nashuhudia mechi hiyo kwenye runinga ya Azam TV, nilimshuhudia beki George
Michael Osei akimpiga kiwiko Mrisho Ngassa wa Yanga.
Teknolojia
mambo mengine bwana! Azam TV walirudia mara nyingine kuonyesha kwa uzuri kabisa
beki huyo aliyepewa jina la beki katili akimtwanga kiwiko Ngassa akaanguka
chini.
Kitu
kizuri kabisa kilichokuwa wazi, mwamuzi Isihaka Shirikisho wa Tanga alikiona
kiwiko hicho na haraka akamuita beki huyo na kuingiza mkono katika mfuko wake
wa kaptula ikiwa ni dalili angetoa kadi nyekundu.
Wachezaji
wa Ruvu Shooting walimzonga Shirikisho kwa nguvu zote wakisisitiza kwamba
Ngassa alidanganya na kujiangusha ili beki huyo apate adhabu kama ambavyo
imekuwa ikielezwa kwamba anasingiziwa.
Shirikisho
alikosa nguvu na mwisho akaamua kutoa kadi ya njano ambayo kwangu ilinishangaza.
Mchezaji anampiga mwenzake kiwiko, tena hawagombei hata mpira unawezaje kusema
ni bahati mbaya?
Ngassa
alikuwa anapishana na Osei, akitokea upande mmoja kwenda mwingine na hakuna
aliyekuwa akigombea mpira. Ilivyokuwa inafanana sana na ile ishu ya Emmanuel
Okwi wa Simba dhidi ya Aggrey Morris wa Azam FC.
Kama
unakumbuka Morris alifungiwa kwa kuwa Okwi alizimia. Lakini Osei pia alifungiwa
baada ya picha yake akimkaba koo mshambuliaji Amissi Tambwe wa Yanga kunaswa na
wapiga picha mahiri wa gazeti la Championi.
Ingawa
ilizua mjadala, wapo waliosema anaonewa kwa kuwa walitanguliza ushabiki, mwisho
alipewa adhabu ya kufungiwa mechi tatu. Shukrani kwa Championi kwa kazi nzuri
kabisa.
Aliporejea,
mechi dhidi ya Stand United, Osei akalambwa kadi nyekundu tena kutokana na
kucheza rafu mbaya.
Msemaji
wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amekuwa akimtetea sana Osei kwamba si mtu
mkorofi badala yake wamekuwa wakimchokoza tu. Lakini ukiangalia marejeo ya yeye
na Ngassa unagundua ni ukatili unaopita kiasi na mimi ninaamini hawezi kusonga
mbele zaidi ya hapo.
Mchezaji
anayeingia uwanjani kuwaumiza wenzake makusudi. Kwa kuwa anaamini mpira si kazi
yake ana uhakika na ajira yake kwa kuwa ni askari.
Vipi
unampiga mtu kiwiko bila sababu ya msingi, kwa makusudi, tena mkiwa hamna
mpira! Mbaya zaidi siku chache zimepita tangu uboronge na mabosi wako wametumia
nguvu nyingi kukusafisha.
Mimi
naamini ukiwa askari nidhamu inakuwa juu zaidi. Vipi huyu Osei na ajabu bado
viongozi kama Masau wanaweza kufungua mdomo na kumtetea tena kwa tukio hilo.
Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) litawashangaza wengi kama litamuadhibu rais wake, Jamal
Malinzi, maana ndiye bosi. Lakini vipi suala la Osei kwa mara nyingine
linatokea na hakuna lolote! Huyu beki ni maarufu sana? Akikosekana mambo yote
ya Ruvu au soka la Tanzania yatakwama?
Ubaguzi
unapigwa vita katika soka, watu wanabeba mabango, wachezaji wanavaa fulana na
vinginevyo.
Inawezekana ni wakati wa kumpinga Osei kwa mabango kwamba amezidi
na anapaswa kujitambua, aache mambo ya kizamani, yasiyokuwa na msingi, mambo
yanayofanywa na watu wasiojitambua na kama askari anapaswa kuwa mfano katika
nidhamu.
Osei,
acha longolongo, cheza soka. Pia litakuwa ni jambo sahihi TFF wakichukua hatua
kwa mara nyingine kukomesha upuuzi kama huo katika Ligi Kuu Bara.
0 COMMENTS:
Post a Comment