Huu ni msimu wa Yanga! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya vijana hao wa Jangwani kuendeleza wimbi la ushindi kwenye Ligi Kuu Bara na sasa wamebakiza siku tano tu watawazwe mabingwa wa ligi hiyo.
Hii ni baada ya jana
kupambana na kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Stand United katika mchezo
mkali uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, uliohudhuriwa na
mashabiki wachache.
Yanga iliingia kwenye mchezo
huo, zikiwa zimepita siku mbili tu tangu ipate sare ya bao 1-1 dhidi ya Etoile
du Sahel kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho.
Ushindi wa jana, unaifanya
Yanga iwe imeweka rekodi ya kushinda michezo sita mfululizo kwenye Ligi Kuu Bara
na kuonekana kama tayari imeshausogeza ubingwa Jangwani.
Yanga hivi sasa imejikita
kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi 49 na inatakiwa ishinde michezo miwili tu
ijayo itakayochezwa ndani ya siku tano zijazo ili iutwae ubingwa. Michezo hiyo
ni dhidi ya Polisi Moro keshokutwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Taifa na ule dhidi ya
Ruvu Shooting Jumatatu ijayo kwenye uwanja huo.
Kama Yanga ikishinda
michezo hiyo, itafikisha pointi 55 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote ile,
kwani Azam FC ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 42 na kama ikishinda michezo
yake yote iliyobaki, itafikisha pointi 54.
Hivi sasa Yanga ambayo
imeshinda mechi zote za ligi zilizofuata tangu ifungwe na Simba Machi 8,
imeiacha Azam FC kwa tofauti ya pointi saba.
Baada ya mchezo wa jana,
Kocha Hans van Der Pluijm, alisema: “Mchezo ulikuwa mzuri lakini hatukuwa
katika kiwango chetu.”
Naye Kocha wa Stand,
Mathias Lule, alisema wamesikitishwa kupoteza mchezo huo kwa kuwa walipambana
kadiri ya uwezo wao lakini akatamba watahakikisha wanashinda michezo yao mitatu
iliyobaki ili kujinusuru na kushuka daraja.
Stand United inabaki katika
nafasi ya tisa ikiwa na pointi 28.
Yanga waliuanza mpira kwa
kasi na dakika ya nne tu Mbrazili Andrey Coutinho, aliyerejea dimbani baada ya
kukaa nje ya uwanja kwa miezi miwili kutokana na kuumia katika ushindi wa 3-1
dhidi ya Mbeya City, Februari 22, alipiga shuti kali lililokwenda nje kidogo ya
lango.
Vinara walifanya mabadiliko
ya wachezaji wanne katika kikosi kilichotoka sare ya 1-1 na Waarabu, Etoile du
Sahel, baada ya kuwaanzisha Deogratius Munishi ‘Dida’, Said Juma Makapu, Rajab
Zahir na Andrey Coutinho.
Yanga ndiyo walioonekana
kuanza kwa kulisakama lango la wapinzani wao huku Stand wakifanya mashambulizi
ya kushtukiza.
Hata hivyo, Stand walikuwa
wa kwanza kuliona lango la Yanga katika dakika ya 19 kupitia kwa Kheri Mohammed
baada ya kumzidi ujanja kipa Dida aliyekuwa ametoka katika eneo lake.
Baada ya hapo, Yanga
walizidi kulisakama lango la Stand na kufanikiwa kusawazisha dakika ya 30
kupitia kwa Amissi Tambwe aliyefunga akipokea pasi ya Mrisho Ngassa.
Ngassa aliifungia Yanga bao
la pili dakika ya 45 baada ya kugongeana vizuri na Juma Abdul kisha kuachia
shuti lililotinga kwenye wavu wa juu.
Wakati Yanga wakidhani
mambo yameshakuwa rahisi kwao, Kheri aliingia tena wavuni dakika ya 65 na
kufanya matokeo kuwa 2-2.
Iliwalazimu Yanga wapambane
kupata bao la ushindi ambalo lilipatikana kwa njia ya mkwaju wa penalti dakika
ya 79, iliyotumbukizwa na Simon Msuva baada ya Tambwe kufanyiwa madhambi ndani
ya eneo la hatari.
Baada ya mchezo huo, kocha
Hans van Der Pluijm alionekana akizozana na beki wake Mbuyu Twite akimlaumu
kucheza chini ya kiwango lakini raia huyo wa Rwanda naye alisikika akimjibu
kuwa wachezaji wengi walicheza chini ya kiwango, hivyo haikuwa sahihi kumlaumu
yeye tu.
0 COMMENTS:
Post a Comment