Na Saleh Ally
UNAPOKWENDA Ulaya, jezi inayoongoza kwa kuuzwa kuliko
zote ni ya rangi nyeupe na ufito mweusi au rangi ya dhahabu.
Hiyo ni jezi ya mabingwa wa Ulaya, Real Madrid ambao
tayari wameuza zaidi ya jezi milioni 1.5. Pamoja na kuboronga Ligi Kuu England,
Manchester United inashika namba moja England na mbili Ulaya kwa kuuza jezi
milioni 1.4.
Nafasi ya pili Hispania inakwenda kwa Barcelona ambayo
inashika nafasi ya tatu Ulaya ambayo imeuza zaidi ya jezi milioni 1.2.
Chelsea wako nafasi ya pili England na nne Ulaya baada
ya kuuza zaidi ya jezi 910,000 ikiwa ni mara ya kwanza kufanya vizuri zaidi na
kuzipiku Arsenal na Liverpool.
Takwimu za Ulaya zinaonyesha ziko juu sana kama
utalinganisha na za hapa nyumbani, lakini jezi yenye rangi za njano na kijani
ndiyo imeonekana kuuzwa zaidi kwa msimu unaomalizika mwezi huu.
Kupitia tathmini kadhaa zilizofanywa na gazeti hili,
inaonyesha jezi ya Yanga ndiyo iliyouzwa zaidi ya jezi nyingine yoyote.
Yanga imeuza jezi yake kwa kiasi kikubwa kupitia chache
ambazo ni ‘orijino’ na nyingi zaidi ambazo ni feki.
Katika mahojiano na wauzaji na baadhi ya wanunuzi,
inaonekana wengi wamekuwa wakinunua jezi za Yanga na kiwango cha manunuzi kilipanda
kwa asilimia 68 kuanzia Januari, mwaka huu wakati Yanga ilipoanza kushiriki
michuano ya kimataifa.
Asilimia 12 za mauzo kupanda ziliongezeka mwezi uliopita
wakati Yanga ilipoanza kuonyesha ina asilimia kubwa zaidi ya kubeba ubingwa wa
Tanzania Bara. Ilipofanikiwa kuubeba, mauzo yalizidi kuwa juu zaidi kwa jezi
hizo za kijani na njano.
Wauzaji wakubwa wa jezi feki, wengi wanaamini huuza hadi
jezi 1,000 kwa mwezi zikiwamo zinazokwenda mikoani. Maana yake kwa wauzaji hadi
10,000 zinaweza kufikia au zaidi ya jezi 100,000 ambazo zinanunuliwa kwa bei
kuanzia Sh 8,000 hadi Sh 10,000.
Jezi za Simba pia huuzwa hadi bei kama hiyo ya Yanga
ingawa kutokana na timu yao kutofanya vizuri, wanaouza jezi orijino wamekuwa
wakilazimika kushusha hadi Sh 20,000 ili kuzisaidia kuuzika. Hii inaifanya jezi
ya Yanga kubaki juu zaidi kwa bei na kuifanya kuwa ghali kwa msimu huu pia
iliyouzika sana.
Jezi orijino, ambazo huuzwa kuanzia Sh 25,000 hadi
30,000 zinaonekana kuwa na mauzo ya chini kabisa kwa kuwa kwa mwaka mzima zimeuzwa
10,000 tu, tena pamoja na za Simba na hii tathmini ni kupitia kwa kampuni ya
Romario ambao ni wasambazaji wa vifaa vya michezo vya Uhlsports ambavyo
hutumiwa na Yanga, Simba na timu nyingine za Ligi Kuu Bara.
Kwa msimu mzima, inaonyesha Yanga imeuza jezi zipatazo
180,000 kwa feki ambazo ni nyingi zaidi pamoja na orijino.
“Unajua sisi tuna mkataba wa kusambaza jezi za Ligi Kuu
Bara. Huwa zinabaki chache tu ambazo tunaweza kuziuza lakini si rasmi kwamba
tunauza za mashabiki.
“Lakini Yanga na Simba kwa pamoja wanaweza kufikisha
hadi jezi elfu kumi zinazonunuliwa. Ila wale wanaouza feki ndiyo wanauza zaidi,”
kilieleza chanzo kutoka kampuni hiyo maarufu ya kusambaza vifaa vya michezo
nchini ya Romario.
Wauzaji wengi wa mtaani, wanaonekana kupata faida kubwa
kutokana na bei yao kuwa chini na jezi za Simba ndiyo zinazofuatia kimauzo.
Simba hawako nyuma sana, wana uwezo wa kuuza hadi jezi
125,000, wameporomoka kimauzo kutokana na timu yao kuyumba mfululizo kwa misimu
mitatu sasa.
Wengi wamekuwa wakinunua jezi hizo kwa wingi kabla na
baada ya mechi dhidi ya Yanga ambayo wana imani kubwa ya kufanya vizuri.
Timu ya tatu kwa mauzo imekuwa Mbeya City. Taarifa
zinaeleza imeingia mkataba na Kampuni ya Romario ili watengenezewe jezi orijino
wauze kwa mashabiki.
Wao wamefanikiwa angalau kudhibiti kidogo uuzwaji wa
jezi feki lakini kwa Dar es Salaam bado zinauzika na kwa mwezi hadi jezi 2,000
huuzwa kwa mwezi. Wakati Nyanda za Juu, Kusini nako wana soko zuri.
Angalau kwa mwezi, Mbeya City wanaweza kuuza jezi 2,500
kulingana na wakati. Kwa msimu mzima, wameuza zaidi ya jezi 24,000 ukijumlisha
feki na orijino. Msimu uliopita, ulikuwa mzuri zaidi, lakini msimu huu kuyumba
kwa kikosi chao, kukayumbisha soko mtaani.
Azam FC imekuwa na mfumo mzuri wa usambazaji wa jezi
zake. Hivyo kufanya iwe na soko angalau la jezi 11,000 kwa msimu.
Hata hivyo, inaonekana uchache wa mauzo unatokana na
timu hiyo kuonekana si ya wananchi kama zilivyo Yanga, Simba na Mbeya City.
Hata hivyo, mpangilio mzuri wa uuzwaji wa jezi hizo
unazifanya angalau kupatikana na sasa imezipiga bao hata timu za wananchi kama
Coastal Union, Stand United na nyingine chache.
Mpangilio mzuri zaidi wa uuzwaji, upatikanaji na ubunifu
unaweza kusaidia jezi za timu za Tanzania Bara kuuzwa zaidi.
0 COMMENTS:
Post a Comment