Na Saleh Ally
KAMA utazungumzia viongozi wa soka kwa sasa, basi
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Mahbub Manji ndiye gumzo zaidi kuliko mwingine
yeyote.
Manji ambaye amekuwa kimya kwa muda mwingi, mgumu
kusikika kwenye vyombo vya habari akizungumza lakini jina lake halitoki
midomoni mwa mashabiki wapenda soka, wawe wa Yanga, Simba na timu nyingine.
Hali hiyo inatokana na mwenendo mzuri wa Yanga katika
Ligi Kuu Bara hadi ilipofanikiwa kutwaa ubingwa ikiwa na michezo mkononi.
Lakini aina ya uongozi wake umeibadili Yanga na kuifanya
sasa ni moja. Hakuna migogoro na kwa pamoja mashabiki wanachotaka ni mafanikio
ya timu na klabu yao kwa jumla.
Katika mahojiano maalum na Championi Jumamosi, Manji
anasema Yanga aliyoitaka ya umoja ndiyo iliyopo sasa kwa kuwa ni klabu ya watu
wanaoshirikiana wenyewe, wanaoshirikiana na klabu nyingine, pia wanaoelewa
kwamba michezo ni umoja na si uadui.
Tokea uongozi umeingia madarakani, kipi hasa unaweza
kujivunia?
Manji: Najivunia kuwa na watu wenye umoja. Nikukumbushe,
nguvu ya Yanga ni watu. Ndiyo maana nimekuwa nikisisitiza kuwa hii ni klabu ya
watu, inamilikiwa na watu.
Zaidi ninajivunia umoja wao, kuwa na wanachama na
mashabiki walio pamoja. Uongozi imara, kikosi imara na benchi bora la ufundi.
Hivi karibuni ilionekana kama uongozi wako umetikisika
na viongozi kadhaa waliondolewa. Huoni ni tatizo?
Manji: Kuna wakati kiongozi inabidi uwe imara. Ilikuwa
ni lazima kurekebisha matatizo yaliyojitokeza, ndiyo maana leo unaona Yanga
imetulia.
Uongozi ni imara kwa kuwa waliopo ni watu sahihi. Tuna
katibu ambaye ni daktari wa michezo, tuna viongozi wengi ambao ni vijana na
wachapakazi. Tumebadili mambo, unaona vitu vinakwenda.
Kuna kitu ambacho kilikushinda mara baada ya kuwa
umeingia madarakani na unatamani kukikamilisha kabla ya muda wako kwisha?
Manji: Ninaamini hakuna.
Vipi kuhusiana na kurejesha bao tano ambazo Yanga
walifungwa na Simba misimu mitatu iliyopita?
Manji: Hapa watu wamekuwa wakichanganya, wakati naingia
kugombea Yanga nilieleza kilichonifanya nigombee. Tulifungwa mabao tano bila na
Simba na ikaonekana kama tumepoteana, tulisambaratika.
Niliamini kipindi hicho Yanga walihitaji mtu imara
ambaye angeweza kusimama na kuwasahaulisha yaliyopita kwa ajili ya kupambana
ili mambo yaendelee.
Niliahidi kurudisha umoja ambao sasa unauona. Kuwafunga Simba tano ni jambo jingine
kabisa na kama halijatokea wakati wa uongozi wangu, wengine watafanya.
Simba ni watani wenu, unacho cha kujivunia kama vile
uliwahi kuwafanya washindwe kufanya jambo fulani?
Manji: Uongozi wa Simba uliopita na uliopo sasa unajua.
Kwa misimu mitatu sasa Simba hawajashika nafasi ya pili wala kushiriki michuano
ya kimataifa, ndiyo kipindi cha uongozi nimekuwa madarakani.
Kwa miaka mitatu nikiwa na uongozi wangu, tumeiwezesha
Yanga kuchukua ubingwa mara mbili, nafasi ya pili mara moja. Ndiyo maana nasema
kama Simba wakinyoosha vidole vitano, mimi nitanyoosha vitatu ambacho kimekuwa
kipindi kigumu sana kwao katika ligi na michuano ya kimataifa.
Je, ulifanya lolote kusaidia kudumisha uhusiano wa
kimichezo kati yako na Simba?
Manji: Nafikiri hujawahi kusikia nikiwasema Simba vibaya
au kuwabeza hata mara moja. Simba si adui zetu, ni wapinzani na watani wetu.
Utaona hata baada ya Rais mpya wa Simba, (Evans) Aveva kuingia madarakani,
nilikuwa kiongozi wa kwanza kumpongeza.
Pia wakati tunataka kumsajili (Amissi) Tambwe nilimpigia
Aveva na kumueleza kuwa pamoja na kwamba walimuacha, sisi tulihitaji kumchukua.
Hii ilikuwa ni kuonyesha sisi ni watu ambao tunaweza kushirikiana.
Uongozi wa wakati wangu umezika mambo mengi ambayo
yalifanyika nyuma na sasa soka ni sehemu ya kujenga, kufurahisha na
kushirikiana pia.
Unafikiri nini kifanyike zaidi kudumisha yaliyopo ili
kuepusha kupiga hatua mbili mbele na baadaye kurudi nyuma tatu?
Manji: Ushirikiano, viongozi kufanya kazi kwa maslahi
kwa maendeleo ya klabu, pia upendo. Utaona leo kila mchezaji ikiwezekana kutoka
kila timu anatamani kuichezea Yanga.
Hii inaonyesha tunaishi katika mwendo ulio sahihi na
wengi wanatamani kufikia tulipo, hivyo lazima tudumishe.
Yanga imefanya vizuri nyumbani. Vipi kuhusiana na
michuano ya kimataifa inaonekana bado mtihani?
Manji: Naungana na wewe, ni mtihani, lakini kwa sisi
mnaotaka tuchukue ubingwa Afrika tukiwa hatuna hata uwanja wa mazoezi, nafikiri
hamtutendei haki.
Nakumbuka uliahidi kujenga uwanja na sasa muda wako wa
uongozi unakaribia kwisha, vipi sasa?
Manji: Nataka nikuhakikishie hiyo ilikuwa nia yangu mimi
na viongozi wote wa wakati wetu, lakini umeona juhudi zetu za kuiomba na kuishawishi
serikali kutupa eneo zilivyoshindikana.
Kweli ni ahadi, sasa uwanja tutajenga wapi. Wataalamu
wameonyesha uwanja sahihi unavyopaswa kuwa na eneo ambalo serikali imetunyima.
Kunaweza kuwa na sababu kwamba ni eneo la hifadhi, lakini kuna kituo cha mabasi
kimewekwa pale.
Kwangu haikuwa changamoto kubwa, serikali imenikatisha
tamaa. Nimeona wameshindwa kutupa eneo hilo kwa miaka mitatu sasa, wangeweza
vipi kufanya hivyo ndani ya mwaka mmoja!
Uchaguzi unakuja. Je, una mpango wowote wa kugombea kwa
mara nyingine?
Manji: (Tabasamu), nafikiri ni wakati mzuri wa
kuwashawishi Wanayanga wengine wenye uwezo wagombee. Kwangu sioni changamoto
nyingine mbele yangu. Kama ningekuwa nina eneo, ninatakiwa kujenga uwanja,
angalau ningesema kuna la kufanya.
0 COMMENTS:
Post a Comment