Na Saleh Ally
LOUIS van Gaal ni mmoja
wa makocha bora duniani kama utazungumzia kwa kiwango cha klabu na hata timu za
taifa.
Mafanikio yake akiwa na
Ajax, Barcelona na Bayern Munich yanajulikana. Amekuwa bosi wa makocha wengi
bora duniani akiwemo Pep Guardiola na Jose Mourinho.
Sasa amekuwa akihaha
kuhakikisha Manchester United anayoinoa inasimama. Ana mipango mingi sana.
Hakuna anayeweza kumgeuza
Van Gaal au kumfundisha kazi ila ushauri inawezekana. Kwa mujibu wa takwimu,
inaonekana Man United ni timu ya nne kwa ubora hadi sasa England.
Si ubora kwa maana ya
msimamo, takwimu za uchezaji mechi, ufungaji mabao zinaonyesha katika timu nne
za juu Man United ndiyo dhaifu zaidi ya timu nyingine.
Udhaifu wake umegawanyika
katika jambo kuu la ulinzi ambalo unaweza kuligawanya mara kadhaa.
Ingawa amemsajili Memphis
Depay ambaye anaelezwa kuwa na uwezo zaidi ya Cristiano Ronaldo, lakini bado
hilo linaonekana si tatizo la Man United kwa msimu huu ambao umebaki mechi tatu
ufungwe na bingwa Chelsea tayari akiwa ameshajulikana.
Tatizo la Man United ni
ulinzi, kwani unapochukua timu nne za juu kwenye msimamo, Man United ndiyo timu
iliyofungwa mabao mengi zaidi.
Man United ndiyo timu
iliyopoteza michezo mingi zaidi, sare nyingi zaidi. Hiyo inaonyesha ulinzi,
unapaswa kuimarishwa zaidi kwa kuwa kikosi hicho bado kina wachezaji wengi sana
wa ushambuliaji kama Wayne Rooney, Juan Mata, Angelo Di Maria, Radamel Falcao,
Robin van Persie na wengine lundo.
Kufungwa:
Man United inaonekana
kuwa na tatizo kubwa katika ulinzi. Kwani katika mechi zake 35 ilizocheza,
imepoteza nane. Ndiyo nyingi zaidi katika timu zote nne za juu.
Chelsea ambao ni mabingwa
wamepoteza mbili tu, Man City saba na Arsenal wamefungwa mara sita.
Kufungwa kumezidi
kuiathiri Man United, utaona ilifungwa mechi tatu mfululizo na kuifanya iwe
timu iliyoruhusu mabao na kupoteza michezo mingi mfululizo sawa na Wes Brom,
Newcastle na Hull City.
Sare:
Katika timu hizo nne za
juu Manchester United ni miongoni mwa zenye sare nyingi. Inazo nane, sawa na
Chelsea, wakati Arsenal na Man City kila moja ina saba lakini kumbuka sare
zinapoteza pointi mbili katika kila mchezo, hivyo si za kuzifanyia sherehe pia.
Ushindi:
Huenda hapo ndiyo Van
Gaal ameanza kupafanyia kazi, kwani Man United ndiyo timu iliyofunga mabao
machache zaidi katika timu nne za juu. Imefunga mara 59.
Mabingwa Chelsea
wamefunga mabao 69, tofauti ya mabao 10 na Man United. Man City wamefunga 71 na
Arsenal wana 66. Maana yake, Van Gaal kweli anatakiwa kuangalia nguvu ya ‘kucheka’
na nyavu na kuhakikisha inaimarika.
Ushindi ni muhimu kuliko
jambo lolote kwa kuwa unatengeneza pointi tatu ambazo ni pointi nyingi zaidi
katika soka kwenye mchezo mmoja.
Mourinho wa Chelsea
amekuwa akijihakikishia ushindi bila ya kujali soka lake ni la kuvutia au la.
Si lazima Van Gaal acheze
soka lisilo na mvuto lakini mvuto bila ya ushindi pia hauna faida kwa timu na
hata shabiki.
Hakuna msimamo wa pasi au
wa soka la kuvutia. Hivyo ingawa Van Gaal ameanza mpango wa kumsajili beki
kisiki wa Borussia Dortmund, Matts Hummels lakini bado hakwepi kutakiwa kutwaa
viungo bora wa ukabaji kuhakikisha Man United inafanya vizuri.
Kama itaendelea kuwa
laini katika safu ya ulinzi, haiwezi pia kuwasaidia mafowadi wake kufanya
vizuri mbele hata kama watakuwa na ubora wa juu sana. Maana watafunga na mabao
yatarudi kirahisi. Mwisho, watakata tamaa.
Kwa maana ya ubora, maana
yake, Man United kwa sasa haina ubora wa Arsenal, Man City na Chelsea na hicho
ndicho kinachopaswa kuangaliwa na Van Gaal, sasa aonyeshe ubora wa ujuzi wake.
Man U katika msimamo wa
Premier
P W D L GF GA GD Pts
4. Man United 35 19 8 8 59 35 24 65








0 COMMENTS:
Post a Comment