Simba SC jana ilikutana na kocha wake aliyemaliza mkataba kwa sasa, Mserbia, Goran
Kopunovic na kufanya naye mazungumzo ya kuendelea kukinoa kikosi hicho kwa
msimu ujao lakini mambo hayakwenda sawa katika makubaliano na kuifanya ishu
kuwa ngumu.
Kopunovic
alitua kuinoa timu hiyo katikati ya msimu huu kwa mkataba wa miezi sita na
kuifanikisha kumaliza kwenye nafasi ya tatu baada ya kuikuta inapumulia ‘mashine’
kwenye nafasi ya 12.
Simba
imeonekana kuvutiwa na kazi ya kocha huyo anayeonekana kulipenda soka la vijana
na jana ikalazimika kumuita na kuzungumza naye juu ya mustakabali wake ambapo
inaelezwa kuwa kikao hicho kilichohudhuriwa na baadhi ya wajumbe wa kamati ya
utendaji kilichukua takriban saa mbili bila ya majibu ya uhakika ya kocha huyo
kuendelea na kazi.
Mmoja
wa watu wa ndani wa Simba ameliambia Championi Jumatatu kuwa kikwazo kikubwa
kuhusiana na kusaini mkataba mpya kwa kocha huyo ni kutokana na dau kubwa la
usajili wake alilolitaja ambalo ni dola 50,000 za Kimarekani ambazo ni sawa na
Sh milioni 100.
Chanzo
hicho kiliongeza kuwa Kopunovic alitaka ada hiyo kwa mkataba wa miezi tisa
mpaka 12 ambapo uongozi wa Simba kwa upande wao umepinga muda huo na
kupendekeza wampe miaka miwili.
“Ishu
inaonekana kuwa ngumu kwa sababu kocha amekazia ada yake ya usajili dola
50,000, fedha ambazo uongozi unaona ni nyingi na kingine ada hiyo anataka iwe
kwa miezi tisa au 12 lakini uongozi unataka apewe miaka miwili, hapo ndipo
kwenye mvutano mpaka sasa na mpaka wanatoka kwenye kikao hakukuwa na muafaka,”
alisema mtoa taarifa huyo.
Baada
alitafutwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe
kuzungumzia suala hilo lakini hakupatikana baada ya simu yake ya mkononi kuita muda
mrefu bila ya majibu.
Haikuishia
hapo, alipotafutwa makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Kassim Dewji alisisitiza bado
hawajashindwana na kocha huyo na kwamba mazungumzo bado yanaendelea.
“Si
kweli kwamba tumeshindwana na kocha, isipokuwa bado tupo kwenye mazungumzo ya
kuafikiana, leo (jana) tulikuwa kwenye kikao na tumekiahirisha mpaka siku
nyingine ila mazungumzo yetu yakifika mwisho au kuafikiana chochote basi rais
(Evans Aveva) atatoa tamko rasmi kuhusiana na hilo,” alisema Dewji.
0 COMMENTS:
Post a Comment