May 11, 2015


Na Saleh Ally
KIUNGO Haruna Niyonzima ndiye injini ya kikosi cha Yanga, ukibisha hili utakuwa haujui mpira.
Hivi karibuni amejaaliwa neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu baada ya mkewe kujifungua mapacha, mabinti wawili waliopewa majina ya Atka na Atfa.

Mabinti hao warembo ni faraja kuu katika familia ya Niyonzima ambayo sasa ina watoto wanne. Kazi ipo kwa kiungo huyo na mkewe, kwamba wamekuwa wakipata shida kujua yupi ni Atka na yupi ni Atfa, yaani Kulwa na Doto wanachanganya ile mbaya kutokana na wanavyofanana!

Katika mahojiano maalum na SALEHJEMBE, Niyonzima anasema mkasa huo wa mabinti zake amekuwa akiufananisha na ule wa rafiki zake pacha, Mbuyu na Kabange Twitte ambao alicheza nao APR ya Rwanda na sasa anacheza na mmoja Yanga.

“Kwa kweli namshukuru sana Mungu kwa hii neema, lakini kwa sasa tumekuwa tukipata shida kuwatambua. Angalau siku zinavyokwenda tunaanza kujua Atfa ni yupi na yupi ni Atka,” anasema Niyonzima.

“Nakumbuka nimefanya kazi na Mbuyu na Kabange kwa miaka saba, lakini ilinichukua miaka mitano kugundua yupi hasa ni fulani.

“Mbaya zaidi, ulikuwa ukimuita Mbuyu kwa jina la Kabange anaitika tu. Walishajua watu wamekuwa wakisumbuka kuwajua.”

Mkeo amejifungua Aprili 17, mwaka huu siku ambazo mlikuwa na mechi ya kimataifa dhidi ya Etoile, vipi uliweza kujiandaa vizuri?
Niyonzima: Ulikuwa wakati mgumu sana, ingawa mechi moja sikucheza. Lakini hata ile nyingine nilicheza kwa ugumu kwa kuwa mke wangu alikuwa katika hatua za mwisho na tulishajua ni mapacha. Nilijitahidi sana, kambini kidogo, natoka nakuja nyumbani.

Kulea mapacha si mchezo, unatakiwa kazini kila mara. Je, unawezaje kufanya mambo yote?
Niyonzima: Ni kazi kubwa sana, mama anashika mtoto mmoja na mimi mwingine, basi tunabembeleza tu. Mapacha akilia mmoja, mwingine pia analia. Mmoja akiwa ananyonya, mwingine pia anataka. Lakini tunapambana na asubuhi nakuwa kazini, sina ujanja.

Umesema una watoto wanne, labda una mpango wa kufikisha kumi na ngapi ili kuijaza dunia?
Niyonzima: (Tabasamu), Kwa sasa naweza kusema napumzika kwanza ili nipambane kuwapatia hawa malezi mazuri. Mengine yatajulikana baadaye inshallah.

Yanga una misimu minne sasa, umechukua ubingwa wa bara mara mbili, Kagame mara moja. Unalizungumziaje hili?
Niyonzima: Kwanza niwashukuru wachezaji, viongozi, wadau wa Yanga na mashabiki. Kweli nimepambana sana, nakumbuka msimu wa kwanza ulikuwa mgumu sana kwangu, lakini niliapa kupambana.

Nini kilikufanya upambane sana, ulikuwa na mapenzi na Yanga kabla?
Niyonzima: Yanga niliijua tu, lakini nikawa na nia ya kutoka nje ya Rwanda ili kupata changamoto. Namshukuru sana Abdallah Bin Kleb, aliniongoza hadi kufika Yanga.
Kilichochangia sana nijitume na kutaka kuwalipa Wanayanga ni wale watu waliokuja kwa wingi uwanja wa ndege kunipokea. Nililia kwa furaha, nilishangazwa na ile hali, moyoni nikasema nitawalipa hawa watu. Naamini nimejitahidi kadiri ya uwezo wangu.

Lakini mashabiki hao wamekuwa wakikuzomea na kusema unapoteza muda kwa kucheza taratibu?
Niyonzima: Si wote wanaojua mpira, najua wapo wanaonielewa. Yanga tumechukua ubingwa mara mbili Tanzania Bara mimi nikichezesha timu. Si kweli kupiga mpira mbele ndiyo kuwahi ufike langoni.

Kila ninapotulia na mpira, ninatengeneza jambo. Kocha anajua, hajawahi kunizuia na mchezaji unayejitambua hauwezi kucheza na jukwaa. Kawaida mashabiki siku zote wanataka bao, wanataka kuona mpira umeingia langoni, lakini haiwezi kuwa kwa kupiga tu bila ya mipango.

Suala hilo huwa linakuchanganya uwanjani?
Niyonzima: Haijawahi kutokea, sijawahi kuchanganywa na mashabiki wa timu yangu au timu pinzani. Nacheza soka kwa malengo, najua nafanya nini, mimi ni mvumilivu na siku zote namtanguliza Mwenyezi Mungu.

Wakati fulani kulikuwa kuna taarifa unakwenda Simba, vipi msimu huu na mkataba wako na Yanga unafikia tamati?
Niyonzima: Kweli Simba walinitaka, tulizungumza nao na mwisho walishindwa kunitimizia nilichotaka, hiyo ni miaka miwili iliyopita.
Soka ni kazi yangu, lazima niangalie maslahi. Hadi sasa kuna timu mbili hapa Tanzania na nyingine za nje zinanitaka. Itategemea Yanga, wanaonaje na kama vipi mimi ninaonaje ingawa nitamshukuru zaidi Mungu nikipata timu nje.

Kwa nini ukipata timu nje na si hapa Tanzania, umepachoka?
Niyonzima: Hapana, Tanzania ni sehemu bora kabisa kuishi na kufanya kazi kutokana na ukarimu wa watu wake, hata familia yangu ina furaha sana hapa. Ila mimi ni mtu wa kupenda changamoto mpya. Ndiyo maana niliondoka Rwanda wakati APR inanihitaji sana.

Uliwahi kutakiwa na El Merreikh ya Sudan, lakini ikaelezwa uliamua kubaki Tanzania. Je, ni mapenzi yako kwa Yanga?
Niyonzima: Kweli, El Merreikh walinifuata Kenya wakati wa Chalenji, wakaahidi kutoa dola 150,000 (Sh Milioni 296) kwa mkataba wa miaka mitatu. Yanga wangepewa dola 70,000 (Sh Milioni 138) lakini ilishindikana.
Ningependa kwenda, Yanga pia ingepata faida kwa kuwa ilinisajili kwa dola 30,000 (Sh Milioni 59) kwa mkataba wa miaka miwili. Tena nilikuwa nimebakiza miezi sita tu, lakini uongozi haukukubali. Mwisho niliona haikuwa riziki, mimi ni Mwislamu, ninaamini majaaliwa ya Mwenyezi Mungu.

Unakizungumziaje kikosi cha Yanga kilichotwaa ubingwa msimu huu na nini kifanyike?
Niyonzima: Hiki ndiyo kikosi bora zaidi cha Yanga, nakuhakikishia kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati hakuna timu inayoweza kutupa shida.
Ingawa hatujakamilika asilimia mia. Vizuri kujitahidi kuwabakiza wengi. Mfano Simon Msuva, Mrisho Ngassa, Mbuyu Twitte kama wataondoka ni shida kwa timu.

Unaona si sahihi wao kwenda kusaka maisha nje ya nchi au kwingine?

Niyonzima: Hapana, kule wanafuata maslahi, klabu ikiweza kuwapa, basi vizuri kwa kuwa wachezaji pia wanahitaji kuzoeana ili kucheza vizuri. Wakija wageni, hawawezi kuwa na ubora kama watakaoondoka ikiwezekana kwa msimu mzima.

Ila nasisitiza, kama mtu kwenda nje ni ndoto yake, basi apewe nafasi. Hii pia itaisaidia Tanzania kufanya vizuri kimataifa. Hili nimekuwa nikilisisitiza sana hata nyumbani Rwanda.

Unafikiri kuna siku Yanga itarudisha bao tano ilizopigwa na Simba?
Niyonzima: Tulifungwa tano na Simba nikiwa uwanjani nacheza. Ninaamini hili litachukua muda na Yanga italipa kisasi siku isiyotegemewa.

Ingewezekana siku tulipotangulia kwa mabao matatu hadi mapumziko. Lakini watu wakatuchanganya, hata wasiojua mpira nao walitufundisha kwa kuwa waliona rahisi. Mwisho wakatuvuruga. Nakuambia kama zingeongezeka dakika tano siku ile, tungefungwa bao la nne.


 SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic