May 1, 2015


Na Saleh Ally
Simba ndiyo kikosi kinachoongoza kuwa na wachezaji vijana ghali zaidi katika Ligi Kuu Bara.


Wachezaji wake watano wanaonyesha iwapo watataka kuuzwa, watakuwa na bei kubwa isiyo chini ya Sh milioni 40.

Inawezekana klabu nyingine zina vijana wengine ghali lakini Jonas Mkude, Hassan Kessy, Ramadhani Singano, Hassan Isihaka na Ibrahim Ajibu ‘Kadabra’ wanaifanya Simba kuwa na vijana ghali zaidi katika Ligi Kuu Bara.

Kwamba ni wachezaji ghali makinda ambao ukizungumzia suala la kuwauza, Simba ina uhakika wa kuingiza zaidi ya Sh milioni 300.

Kiungo Mkude, 23, ndiye anaongoza kwa kuwa mchezaji ghali zaidi kwa maana ya usajili kwa kuwa Simba ililazimika kumwaga Sh milioni 60 katika mkataba wake mpya.

Fedha hizo zinamfanya kuwa kiungo ghali zaidi wa hapa nyumbani na Simba inampa Sh milioni 2 kila mwezi kama mshahara wake.

Anayefuatia kwa kuwa ghali hadi sasa ni beki wa pembeni, Kessy, 21, aliyesajiliwa na Simba akitokea Mtibwa Sugar ambaye Msimbazi walilazimika kutoa Sh milioni 35 kumnasa.

Mkude anakuwa ghali zaidi kwa kuwa fedha yake ni nyingi katika usajili, pia alilipwa yeye na si klabu kwa vile amekulia Simba. Kessy analipwa mshahara wa Sh milioni mbili pia.

Singano, 22, analipwa mshahara mdogo Sh 800,000, hii ni kwa kuwa amepanda daraja kutoka timu ya vijana akiwa na mshahara mdogo zaidi kabla ya kuongezewa na kufikia anayolipwa sasa.

Ila kama kuna timu itataka kumnunua au Simba itataka kuongeza mkataba, lazima haitakuwa mshahara wa chini ya Sh milioni 1.5, pia thamani yake lazima itavuka Sh milioni 35.

Beki Isihaka, 21, analipwa Sh 400,000 kwa mwezi sawa na kiungo Ajibu, 19, lakini kama ni ishu ya kuuzwa au kuongezwa mkataba, hakuna atakayekuwa chini ya Sh milioni 35 hadi 40.

Tayari Isihaka ambaye sasa ni nahodha Simba, amesema anataka dau kama la Mkude lakini kwa Ajibu lazima thamani yake angalau iwe Sh milioni 50.

Wachezaji hawa wanakuwa na thamani kubwa kutokana na viwango vyao, pia umri unawaruhusu kucheza muda mwingi zaidi na hiki ni kigezo kingine cha kufanya bei ipande.

 1. Mkude
Kuzaliwa: 12/03/1992
Mshahara: Sh mil 2

2. Kessy
Kuzaliwa: 25/12/1994
Mshahara: Sh mil 2

3. Singano
Kuzaliwa: 3/4/1993
Mshahara: Sh 800,000

4. Isihaka
Kuzaliwa: 11/30/1994
Mshahara: Sh 400,000

5. Ajibu
Kuzaliwa: 9/12/1996
Mshahara: Sh 400,000




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic