May 4, 2015


Licha ya kufungwa bao 1-0 na Etoile du Sahel na kutolewa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, amesema kikosi chake kilicheza vizuri na kupotea nafasi mbili za kufunga.


Yanga juzi Jumamosi usiku ilifungwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Olympique katika mji mdogo wa Sousse huko Sahel, Tunisia na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Pluijm raia wa Uholanzi alisema ni bahati mbaya tu timu yake kufungwa bao moja kwani ilicheza kwa kiwango kizuri, hasa kipindi cha pili.


“Ilitokea tumefanya kosa moja na wapinzani wetu wakafunga. Hatukuwa na bahati tu kwani tungeweza kufunga bao moja hadi mawili kwa sababu tulipata nafasi za kufanya hivyo,” alisema Pluijm.

“Huu ni mpira, lolote linaweza kutokea na ndivyo ilivyokuwa. Nimeridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu yangu, kwani hatukuwaogopa na tulicheza vile tulivyotaka.”


Pluijm alisema licha ya kucheza ugenini, muda wote walicheza kwa mipango waliyotaka na wapinzani wao hawakuweza kuwabadilisha.

Yanga iliondoka jana Jumapili mchana mjini hapa na inatarajiwa kufika jijini Dar es Salaam, Tanzania leo Jumatatu mchana.


1 COMMENTS:

  1. Ni moja kati ya matokeo ya mpira.
    Nimependa walivyokuwa wanajiamini,hawakuwa na woga kama miaka ya nyuma,wajipange kwa mashindano yanayofuata.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic