KIVUMBI cha Ligi Kuu Bara
kinafikia tamati leo Jumamosi kwa timu zote 14 zinazoshiriki ligi hiyo kushuka
viwanjani kuonyesha ubabe.
Ikiwa ndiyo ligi ya msimu
huu inafikia tamati, vita kubwa inatarajiwa kuwa kwa zile timu ambazo mpaka
sasa hazina uhakika kama zitanusurika na balaa la kushuka daraja ama la ambapo
ni nane tu zenye uhakika wa kushiriki ligi hiyo msimu ujao.
Baada ya kutangaza
ubingwa wa msimu wa 2014/15, Jumatatu ya wiki iliyopita kwa kuichapa Polisi
Moro mabao 4-1, juzi Jumatano ilikabidhiwa rasmi kombe lao ikiwavua Azam ambao
walikuwa mabingwa watetezi.
Nani bingwa, hilo si
swali tena. Hata nafasi ya pili, tayari Azam FC wameishapata majibu kwamba wao
ndiyo wataiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho msimu ujao.
Kwa rekodi za nani mkali
wa kufunga mabao kati ya Yanga na Simba ambao huutumia Uwanja wa Taifa kama
uwanja wa nyumbani, hapo kuna utamu mwingine.
Wengi wamekuwa wakisema
goli au lango la Kusini huwa halilali njaa lakini takwimu zinaonyesha lile la
Kaskazini ndiyo noma zaidi, kweli halilali njaa hata kuliko lile la Kusini.
Ingawa Yanga wana mabao
mengi zaidi, lakini inaonekana hata Simba imefunga mabao mengi zaidi kwenye
lango hilo la Kaskazini.
Kama ni bahati, kwa timu
zote mbili inaonekana imeangukia Kaskazini kuliko Kusini kama ambavyo wengi
wamekuwa wakiamini.
Katika uchunguzi wa
takwimu za mabao hayo kupitia Championi Jumamosi, tangu michuano ya ligi hiyo
ilipoanza Septemba 20, mwaka jana. Jumla ya mechi 33 zinazozihusisha Simba na
Yanga zimepigwa uwanjani hapo ambapo Simba imebakiza mmoja ambao wanatarajia
kucheza leo dhidi ya JKT Ruvu.
Kwa hali hiyo jumla ya
mechi 34 msimu huu zinatakiwa kuchezwa uwanjani hapo ambapo mpaka kukamilika
kwa msimu mmoja, Yanga itakuwa imecheza mechi 17, vivyo hivyo kwa Simba.
REKODI:
Zifuatazo ni rekodi za
timu hizo katika mechi hizo 33 ambazo tayari zimepigwa uwanjani hapo.
Yanga:
Mpaka kufikia Jumatano
iliyopita Yanga ilikuwa imecheza mechi 17 uwanjani hapo na kushinda 11, sare 4
na kufungwa mara mbili. Katika mechi hizo, imefanikiwa kufunga mabao 37 na
imefungwa 12.
Mabao 24 kati ya 37
waliyofunga uwanjani hapo waliyafunga katika goli la upande wa Kaskazini. Hili
ni lile lililo upande wa Simba na 13, upande wa Kusini hili linakuwa ule upande
wa Yanga.
Kwa yale ya kufungwa,
mabao tisa walifungwa goli la Kaskazini na matatu upande wa Kusini.
Wachezaji wa Yanga ambao
walifunga mabao mengi zaidi uwanjani hapo ni Mrundi, Amissi Tambwe (ametumbukia
nyavuni mara 12, kati ya hayo saba akiyafunga katika goli la Kaskazini), Simon
Msuva (kafunga 11, saba kati ya hayo ameyafunga goli la Kaskazini) na Mrisho
Ngassa (4, yote kayafungia goli la Kaskazini).
Simba:
Kwa upande wa Simba mpaka
kufikia hiyo jana ilikuwa imecheza mechi 16 uwanjani hapo na kushinda 9, sare 4
na kufungwa mbili.
Katika mechi hizo, Simba
imefunga mabao 22 na imefungwa 10. Mabao 13 kati ya hayo waliyafungia kwenye goli
la upande wa Kaskazini na tisa waliyafungia goli la Kusini.
Kwa yale ya kufungwa,
mabao matano walifungiwa goli la upande wa Kaskazini na matano mengine goli la
upande wa Kusini.
Wachezaji wa Simba
waliofunga mabao mengi uwanjani hapo ni Mganda, Emmanuel Okwi (8, manne kati ya
hayo kayafungia upande wa Kaskazini), Ibrahim Ajibu (4, yote Kaskazini) na
Ramadhan Singano ‘Messi’ (4, matatu kafungia Kaskazini).
Kutokana na takwimu hizo,
Yanga ndiyo iliyokuwa na bahati zaidi na uwanja huo msimu huu kuliko watani
zao, Simba.
Hata hivyo, goli la
Kaskazini ndiyo linaonekana kuwa halilali njaa ingawa watu wengi wamekuwa
wakiamini lile la Kusini ndiyo halilali njaa.
TIMU MABAO
Kaskazini Yanga 24
Kusini Yanga 13
TIMU MABAO
Kaskazini Simba 13
Kusini Simba 9
Tambwe Mabao
Kaskazini 7
Kusini 5
Okwi Mabao
Kaskazini 4
Kusini 4
SOURCE: CHAMPIONI







0 COMMENTS:
Post a Comment