Uongozi wa timu ya African Sports ya Tanga, iliyopanda kucheza
Ligi Kuu Bara msimu huu, umetamka wazi kuwa, upo kwenye mipango ya kutuma
maombi kwa Klabu ya Yanga ili kupata ridhaa ya kumnasa beki wa timu hiyo,
Edward Charles.
African Sports wamefikia hatua hiyo baada ya beki huyo kutokuwa na
nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha Yanga kinachonolewa na
Mdachi, Hans van Der Pluijm.
Meneja wa African Sports, Ahmed Bozinia, amesema wameona beki huyo
ana uwezo mzuri na anaweza kuwa nguzo muhimu katika kukiimarisha kikosi chao
kwenye mikiki ya Ligi Kuu Bara, hivyo wameamua kufikia uamuzi wa kufuata njia
sahihi ili kumnasa.
“Mipango yetu inaendelea vizuri na sasa tunafanya utaratibu wa
kutuma maombi kwa wenzetu wa Yanga ili watuachie Edward Charles, iwe kwa mkopo
au kwa kumsajili moja kwa moja ili aitumikie timu yetu msimu ujao.
“Tumeona Yanga hawamtumii, lakini kwa uwezo alionao na umri wake,
anaonekana kabisa kwetu atakuwa msaada kwa sababu atapata nafasi ya kucheza
mara kwa mara. Kama tutamalizana vizuri na Yanga, basi atakuwa mchezaji wetu
msimu ujao,” alisema Bozinia kwa msisitizo.
Charles alitua Yanga kwa mbwembwe msimu uliopita akitokea Ruvu
Shooting, lakini amekuwa hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosini hapo
kutokana na upinzani kutoka kwa mkongwe, Oscar Joshua.








0 COMMENTS:
Post a Comment