Kikosi cha Mwadui FC ya Shinyanga, imeeleza kuwa haihitaji
kumuongeza mkataba mwingine mchezaji wa timu hiyo, Uhuru Selemani kutokana na
kutoridhishwa na kiwango chake.
Uhuru, aliyewahi kuichezea Simba, amemaliza mkataba wake na Mwadui
FC ambayo aliisaidia kuitoa Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita na sasa
inatarajiwa kucheza ligi kuu.
Hadi sasa Mwadui imeshasajili wachezaji kadhaa ambao wataitumikia
timu hiyo msimu ujao akiwemo Nizar Khalfan, Jabir Aziz, Shabani Kado, David
Luhende, Paul Nonga, Rashid Mandawa pamoja na wachezaji wengi ambao tayari
wameshapewa mikataba mipya.
Mwenyekiti wa Mwadui FC, Omary
Khatibu, alisema idadi hiyo ya wachezaji waliowasajili ndiyo inayokamilisha
usajili wa timu hiyo na kudai kuwa Uhuru hayupo katika mipango ya kocha Jamhuri
Kihwelo ‘Julio’ kutokana na nafasi yake kujaa.
“Kwa sasa tayari tumejitosheleza, kwani mipango yetu ni
kuhakikisha tunasajili wachezaji wasiozidi 25 ili kuimarisha kikosi.
“Uhuru hakuwa katika mipango ya kocha, kwani yeye ndiye
aliyependekeza kuachana naye. Kwa kifupi, kwa sasa hayupo katika mipango ya
timu,” alisema Khatibu.







0 COMMENTS:
Post a Comment