Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm, hajaridhika na kiwango cha
straika Said Bahanuzi aliyetolewa kwa mkopo Polisi Moro, hivyo uongozi wa timu
hiyo unatafuta timu ya kumpeleka ili kumalizia mkataba wake.
Mkataba wa Bahanuzi na Yanga umebakiza miezi 12, lakini kitendo
cha Polisi Moro kushuka daraja, kinaifanya timu hiyo kumtafutia mahali kwingine
akacheze msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kwa kuwa hana nafasi kwao.
Bahanuzi ni miongoni mwa wachezaji watatu wa Yanga waliotolewa kwa
mkopo msimu uliopita, wengine wakiwa ni Omega Seme aliyepelekwa Ndanda FC na
Khamisi Thabiti aliyekwenda Stand United.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Murro, ameliambia
Championi Jumamosi kuwa, Bahanuzi hayupo katika mipango ya Pluijm, hivyo
anatafutiwa timu akamalizie mkataba.
“Tutampa Bahanuzi nafasi ya kutafuta timu ya kuchezea msimu ujao
ili akaboreshe kiwango chake, kwani hapa nafasi hana,” alisema Muro.
“Tumeamua kufanya hivyo kutokana na kocha Pluijm kutowajumuisha
katika hesabu zake za wachezaji anaowahitaji kuwepo ndani ya kikosi chetu kwa
ajili ya msimu ujao wa ligi.”
0 COMMENTS:
Post a Comment