June 17, 2015


Na Saleh Ally
SAKATA la suala la mkataba wa kiungo mshambuliaji wa Simba, Ramadhani Singano ‘Messi’, bado halijapata mwafaka kwamba tatizo ni nini hasa.


Ukisikiliza maneno ya wadau wa soka, anzia Simba, upande wa Messi utasikia mengi sana ambayo yanaweza kukushangaza.

Wapo wanaosema Messi amegushi, wapo wanaoamini Simba wamemuonea na ndiyo wamefanya mchezo mchafu. Lakini wapo wanaosifia kila upande, wakiamini ndiyo upo sahihi.

Lakini sakata hilo linavyokwenda, inaonekana kuna kitu ambacho huenda si kidogo kwa kuwa hata linavyopelekwa ni kutoka dogo kwenda kuwa kubwa.

Mfano ni baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuamua kuingilia na kukutanisha pande zote mbili kulimaliza.

Mwisho wa kikao, kila mmoja akasema lake, TFF lao, Simba lao na Messi la kwake. Mkanganyiko ukawa juu zaidi hata kuliko ilivyokuwa awali.


Wapo viongozi wa Simba wanalalamika, kwamba TFF inaonyesha ina nia mbaya nao. Kwa kuwa mkataba wa Simba waliosaini na Messi, unalingana kabisa na ulio TFF ambao ndiyo mkataba mama.

Lakini mkataba alionao Messi ambao ni kopi, haufanani hata kidogo na ule ulio TFF na walionao Simba. Lakini wanashangazwa kuona TFF inashindwa kutoa tamko hadi kusababisha mkanganyiko na watu wengi kuanza kupata hisia Simba imefanya usanii katika mkataba huo.

Sasa hapo unakuwa unajiuliza, kwa nini kweli TFF baada ya usuluhishi walishindwa kuweka hayo hadharani? Ukimya wao unalenga au unamaanisha nini? Bado majibu hakuna.

Simba wanaibua hoja nyingine, hata maofisa walioingia kusikiliza kesi yao na Messi, licha ya kuwa ni TFF lakini wote watatu kutoka katika shirikisho hilo walikuwa Yanga, hivyo wanahisi kuna mchezo wanachezewa.


Inawezekana kukawa na ukweli au ni hisia tu! Yote mawili yanawezekana lakini kukosekana kwa uwazi katika suala hilo ndiyo chanzo kikubwa cha mkanganyiko mkubwa uliojitokeza.

Binafsi nao sakata hilo ambalo inaonekana kweli kuna mkanganyiko usio na sababu, limetokea katika wakati mwafaka kabisa.
Angalia kwenye vyombo vingi vya habari, utaona  ni picha za wachezaji mbalimbali wanaojiunga na timu mpya katika Ligi Kuu Bara.

Hiki ndiyo kipindi cha usajili, kipindi ambacho alipitia Messi kwa furaha lakini sasa yuko katika malumbano. Wachezaji wengi wanakuwa kama wendawazimu wakati wa kipindi hiki.

Moja ni hamu kubwa ya kusajiliwa na timu fulani na akiipata, anakuwa kama amewehuka. Pili ni suala la fedha, wapo ambao wamekuwa wakipata fedha ambazo hawakuwahi kuzishika au kuzitegemea. Baada ya hapo, wazimu wa furaha na faraja ya alichokipata, unamfanya asahau kabisa suala la mkataba.

Wako ambao kwa ajili ya haraka hawataki hata kuisoma mikataba yao. Tena wanaona wanacheleweshwa na wanachoona ni muhimu wakati huo ni kuisaini tu na si vinginevyo.

Baada ya fedha kwisha, pia kuzoea kwamba sasa ni mchezaji wa timu fulani, macho yanafunguka upya na anaanza kukumbuka sasa kuusoma mkataba ambao alisaini mwaka au miaka miwili iliyopita. Hii ndiyo njia aliyopitia Messi.

Yeye kutokuwa na mkataba ni kosa lake, wengi wamekuwa wakikwepa kumueleza hilo lakini alistahili kuwa na mkataba wake. Simba huenda tunaweza kuwapa kosa kwa kushindwa kuonyesha uungwana na kumkumbusha, kama walimpa akautupa, basi hilo ni tatizo lake.

Wachezaji wanaosaini sasa wameliona hili la Messi? Je, limewasaidia kuisoma vizuri mikataba yao pamoja na vipengele vya kuvunja wakiwa wameamua kufanya hivyo au pale klabu inapoamua kuwaacha?

Wana uhakika wana mikataba orijino? Je, inalingana na ile ya klabu ambayo inakuwa mitatu. Mmoja wa mchezaji, mmoja wa klabu na wa mwisho wa TFF?

Hivyo, lazima kuwe na umakini, ikiwezekana hata waikabidhi kwa wataalamu kama wanasheria ili wawasomee na kupata uhakika wa mambo.

Haraka ya kutaka kumalizana na timu fulani au haraka ya kupata fedha za usajili, ndiyo tatizo kubwa linalowatafuna wachezaji. Vema wakajiamini na kuwa watulivu kwa kuwa mkataba wa kazi ndiyo mwongozo wa muda wote wa ajira.

Ukiyumba na kupotea, basi umejipoteza kwa muda wote wa kipindi cha kuwa kazini, iwe mwaka, miaka miwili, mitatu au zaidi. Lazima tukubali, kukiwa na umakini wakati wa kuingia mikataba, basi mwisho hakuna tatizo tena litakalojitokeza.

Alichokosea Messi au walichokikosea Simba hakipaswi kurudiwa na wengine. Ndiyo maana nimewakumbusha kwamba kinachotokea sasa kwa Messi na Simba, si sinema tu, ni shule kwenu.




1 COMMENTS:

  1. Saleh ulituonyesha katika mkataba wa Simba na Messi kipengele kinachosema 'mchezaji chini ya umri wa miaka 18 hataruhusiwa kusaini mkataba wa miaka mitatu'.Swadakta,sasa mbona Simba imemsainisha huyo Singano miaka mitatu wakati akiwa na umri wa miaka 17?Uoni hicho ndicho kipengele ndicho kilichofanya mkataba kuchakachuliwa?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic