UKIWA
katika mitaa mbalimbali ya jiji la Mwanza, wadau wengi wa soka wanaonyesha hofu
ya wazi kuhusiana na suala la klabu kongwe ya Toto African.
Wengi
wa wadau hao wanaonyesha waziwazi kuhusiana na suala la kama kweli timu hiyo
inaweza kuhimili vishindo na kubaki Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Tatizo
kubwa ni nguvu ya wanachama ambao wanaweza wakasema lolote bila ya kuhofia
chochote kwa kuwa wao “ndiyo wenye timu.”
Wanachama
wengi wa Toto African hawana tofauti kubwa na wale wa Yanga na Simba. Ambao
hujiita wenye mapenzi makubwa, lakini kikubwa kinakuwa ni kuendeleza maslahi
yao binafsi.
Mara
kadhaa, nimekuwa nikiingia kwenye migogoro na wanachama wa Yanga na Simba, hasa
wale wanaojiita Makomandoo. Kwa kuwa wanachofanya wao ni kuangalia watapata
nini kwa kivuli kuwa wanaipenda timu yao.
Lundo
la mashabiki wa Toto African wanaidai kuipigania timu yao si wanachama hai.
Hawana mpango endelevu zaidi ya kukimbilia kulaumu tu.
| KIKOSI CHA TOTO NA KOCHA WAO, JOHN TEGETE. |
Wako
walioshindwa katika uongozi kiutendaji na timu ikaporomoka daraja. Wako ambao
hawakushiriki hata kidogo katika harakati za timu kurejea Ligi Kuu Bara baada
ya kuwa imeporomoka. Kwa kuwa sasa imerejea, kila mmoja ana sauti.
Wako
walioanza kuamini viongozi walio madarakani sasa ndiyo wakati wa neema kwa kuwa
kuna fedha za udhaminiza Vodacom, Azam TV na huenda timu hiyo ikawapata
wengine. Huo ni ulaji na sasa lazima wauchangamkie!
Toto
African inasema haiwezi kukwepa historia, inataka iendelee kuwa chini ya Yanga.
Kitu ambacho kimekuwa tatizo kubwa kwa kuwa mashabiki wa Simba wa jiji la
Mwanza wanaamini timu hiyo si yao, jambo ambalo ni kosa kubwa.
Kwa
sasa ndani ya Toto African kuna mgogoro mkubwa kati ya viongozi na wale
wanaojulikana kama Toto African Ukawa. Ambao nao wana yao wanayotaka
wasikilizwe, huenda ni sawa au si sawa, kwangu naona si vibaya wakisilizwa.
Wasikilizwe
uli kutatua mgogoro huo, pia wakati wanasikilizwa, nao wanapaswa kukubaliana
katika kuhakikisha suala hilo linakwisha. Kikubwa kiangaliwe ni maslahi ya
klabu. Badala ya watu binafsi.
Lazima
tukubaliane na kila mtu aitazame nafsi yake kwamba miongoni mwenu, wako
mnaofuata maslahi na wale si mapenzi yenu na klabu. Mnaangalie kama kuna
wengine watafaidika, nanyi mnataka. Mko mnaopiga kelele sababu ya njaa tu,
mnajidai wakorofi lakini hamlengi maendeleo ya klabu.
Lakini
wako mlio madarakani huenda mmetanguliza dharau, mkiamini nyie ndiye kila kitu
na lazima muwepo ili katika klabu mambo yaende, jambo ambalo si sahihi pia.
Kikubwa
hapa ni pande zote mbili kukutana zikiwa na lengo moja, maslahi ya klabu.
Nilielezwa jana kuliratajiwa kuwa na mkutano wa wanachama kwa lengo la kumaliza
tofauti hizo.
Kama
utafanyika na kuwakutanisha pande hizo mbili, zikafikia mwafaka, basi utakuwa
wakati mwingine wa kuonyesha upevu katika suala la maendeleo ya soka katika
mkoa wa Mwanza.
Itakuwa
aibu kuu mwakani Toto African ikiporomoka tena kwa ule mtindo wake wa “maji
kupwaa…”.
Kuna
haja ya Wanatoto African kuunganisha nguvu ya pamoja ili kuhakikisha nguvu ya
klabu na pia kikosi kitakachokuwa kinapambana uwanjani.
Baada
ya hapo Wanatoto African waunganishe nguvu na Wanamwanza wengine kwa kuwa Toto
African ndiyo timu pekee inayoshiriki Ligi kuu Bara. Ndiyo itakayowasaidia
kuziona timu zote zikicheza pale CCM Kirumba.
Hivyo
kwa kipindi hiki, bado sapoti ya Toto African inaweza kuwa ya Kimkoa. Lazima
muungane ili kufanya mambo makubwa. Kama mnataka kutengana na kufanikiwa, basi
maisha ya klabu yenu na nyie wenyewe katika michezo yatakuwa ya kubahatisha
tu!.








0 COMMENTS:
Post a Comment