June 26, 2015


Rasmi sasa kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, ametangaza rasmi kwamba, hana mpango wa kumsajili kiungo aliyekuwa akifanya majaribio kikosini hapo, Msierra Leone, Lansana Kamara, ila akatamka kauli ya kishujaa kuwa ndani ya wiki hii atakamilisha usajili wa wachezaji wawili wa kimataifa.


Kamara aliyekuwa akijifua Yanga kwa wiki tatu mfululizo, ametemwa kikosini hapo baada ya majaribio ya mechi ya kwanza ya kirafiki waliyocheza na Friends Rangers ya Magomeni kwenye Uwanja wa Karume, juzi Jumatano.


Mchezaji huyo alipewa taarifa hiyo rasmi na kocha huyo jana ambapo alimuweka wazi kuwa katika mechi hiyo ya kwanza ya mazoezini hakuonyesha kitu, hivyo anapaswa kuchagua mawili, aidha kuendelea kujifua na Yanga bila matumaini yoyote ya kuichezea timu hiyo msimu ujao au aangalie maisha sehemu nyingine.

Imeelezwa kuwa kauli hiyo ilimchefua mchezaji huyo na kuamua kukacha mazoezi ya Yanga yaliyoendelea jana Karume kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao wa kirafiki dhidi ya SC Villa ya Uganda, utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.


“Kamara nimemwambia kwamba kwa kiwango alichonionyesha mazoezini na kwenye mechi ya juzi ni cha kawaida sana kwa mchezaji profesheno kama yeye, halafu pia kiwango chake hakikuweza kuzidi viungo nilionao hapa. Kwa staili hiyo sitaweza kumsajili mchezaji wa kiwango kama chake.

“Kwa hiyo nikamwambia anaweza kuja kuendelea kufanya mazoezi na sisi kama kawaida lakini sitamchukua, sasa sijajua imekuwaje kama ameacha kufanya mazoezi au ni vipi kwa sababu leo (jana) sijamuona hapa, hata hivyo hainisumbui kitu kwa sababu nilishamweleza ukweli wake,” alisema Pluijm.

Alipoulizwa kama timu pinzani za ligi kuu zikimnasa Kamara itakuwaje, alisema: “Wamnase tu (anacheka kuonyesha hajali), kwa mpira alionao sidhani kama ataweza kusumbua safu ya viungo wangu, aende tu hata Simba, Azam au timu nyingine yoyote hakuna tatizo.”

Katika mazungumzo hayo, Pluijm hakuishia hapo tu, bali aliongeza kuwa kuanzia leo Ijumaa, ndani ya siku tatu lazima asajili wachezaji wawili wenye viwango vya juu kutoka nje.

“Kuna wachezaji wawili wanakuja, nikuhakikishie tu kwamba wiki hii haiishi yaani haifiki Jumapili, kuna wachezaji profesheno tunamalizana nao na wana viwango vizuri tu, sikutajii nchi gani wala wanacheza nafasi gani ila utawaona tu. Nakuhakikishia tena kwamba kabla ya wiki hii kuisha,” alimalizia Pluijm.


Wiki iliyopita gazeti hili liliweka wazi kuwa Kamara hana nafasi ya kuichezea Yanga kutokana na kuonyesha uwezo wa kawaida licha ya baadhi ya wadau walio karibu na timu hiyo kuonekana kumpigia debe, hivyo neno limetimia.

1 COMMENTS:

  1. Kuna tofauti kati ya Mzungu na mswahili!! Kama anataka kulinda kibarua na kutengeneza CV lazima asajili walio bora. Angekuwa mbongo hapo angefuata kelele za mashabiki na kusajili garasa la kukuaa benchi

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic