Klabu ya St George ya Ethiopia, imetuma ombi la kumtaka Andrey
Coutinho wa Yanga wakati kiungo huyo mshambuliaji raia wa Brazil akipiga hesabu
za kupewa uraia wa Tanzania ili aichezee Taifa Stars.
St George ambayo ni timu ya zamani ya Kocha wa Rwanda, Milutin
Sredojevic ‘Micho’, imetenga dola 70,000 ili imsajili Coutinho ili ifanye
vizuri katika ligi kuu ya nchi hiyo.
Mmoja wa mabosi wa Yanga amesema, St
George imetuma ombi la kumhitaji Coutinho na sasa viongozi wanamsubiri mchezaji
huyo na Kocha Hans van Der Pluijm ili kufikia muafaka.
“Kuna uwezekano mkubwa Coutinho akaondoka Yanga kwani St George
imetoa ofa ya dola 70,000, hata hivyo tumeshindwa kutoa uamuzi hadi mchezaji
atakaporudi na kocha pia,” kilisema chanzo chetu.
Wakati huohuo, habari zinasema Coutinho ameuandikia barua uongozi
wa Yanga akiomba asaidiwe kupata uraia wa Tanzania ili aichezee Taifa Stars
kwani hana nafasi ya kuichezea Brazil.
“Inaonekana amefurahia maisha ya Tanzania, kwani ametuomba
ikiwezekana tumsaidie kupata uraia wa Tanzania ili aweze kucheza Taifa Stars,”
kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Yanga, Jerry Muro, alisema: “Sisi wenyewe tunasikia tu taarifa hizo, hazijafika
kwetu.”
0 COMMENTS:
Post a Comment