Na Saleh Ally
NILIKUTANA na Mshauri wa Ufundi wa Rais wa
TFF, Pelegrinius Rutahyuga wakati nimekwenda kuhudhuria hafla ya utoaji wa
nishani katika waliochangia soka ya Tanzania kwa takriban miaka 50 tangu
Tanzania ijiunge na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Kama ilivyo kawaida yake, alitumia muda
mwingi kulalamika kwamba naandika fitna tu kuhusu TFF, tena akafikia kutoa
mfano kuwa Sepp Blatter watu ‘wamemfix”, hivyo hata mimi wanaweza “kunifix”,
kwa kuniondoa Championi.
Nikamkumbusha kwamba hapa mimi ni muajiriwa
tu, kama ana uwezo wa kuniondoa kweli basi nitafanya kwingine, najiamini kazi
yangu, kokote itaonekana tu. Akaenda mbali zaidi, kwamba “kufix” anakozungumzia
ni kunipoteza kabisa.
Nilijua
anamaanisha nipotee duniani, nikacheka na kumueleza kamwe mimi si mtu wa hofu
ya kifo, hasa kama nitauawa na mtu mwoga kama yeye ambaye anashindwa kujibu
hoja za msingi na kutishia au kukimbilia kumpoteza mtu.
Msisitizo wangu ulikuwa hivi; “nikifa,
ninaamini nimeacha watu wengi waliopita katika mikono yangu, baadhi yao
watakuwa hodari, hawatakubali kuwa waoga wala kuukubali unafiki.”
Msisitizo wangu ni kwamba, lile nililolisema
Jamal Malinzi katika kazi amezungukwa na watu wengi ambao hawatakuwa na msaada
kama Rutayuga ambaye kwangu hata hiyo nafasi ya ushauri wa Rais wa TFF nimekuwa
nikihoji, anamshauri ufundi upi, kwa kipi alichowahi kukifanya kikapata
mafanikio hadi kuwa hapo?
Kabla ya hapo, Rutayuga alijisifia jambo
moja la ajabu kabisa, ukiliita la kipuuzi, kamwe hautakuwa umekosea hata
kidogo. Kwamba yeye ni kati ya watu waliojifunza fitna kutoka kwa mwenyekiti wa
zamani wa Fat, Muhidini Ndolanga, hivyo kamwe hatishiki na fitna.
Mimi nilikuwa kati ya waandishi wachache tuliobadili
uandishi wa fitna kama zile za wakati wa Ndolanga na Ismail Aden Rage kuwa
ndiyo habari kubwa, hadi kwenda katika habari za uwanjani. Sasa huyu Rutayuga
ambaye ni mshauri wa ufundi, vipi anajisifia kwa ubora wa fitna za uongozi?
Hayo ndiyo anayomshauri Malinzi? Upuuzi mwingine huu.
MANYIKA PETER (KULIA), MMOJA WA WACHEZAJI WALIOICHEZEA TAIFA STARS 'NJAA' KWELIKWELI, LAKINI WALIPIGANA KWA AJILI YA TAIFA LAO. |
Hapo ndipo hoja yangu inapoibukia, kwamba
kweli kuna mtu anaweza kujisifia kwamba alifundishwa fitna au jambo na Ndolanga
na akajivunia? Hata TFF nishani waliyompa, kwangu naona haikuwa sahihi hata
kidogo.
Naikumbuka Taifa Stars ya kipindi kile ambayo
ilikuwa ikiweka kambi pale Jeshi la Wokovu jijini Dar es Salaam. Kwa waliowahi
kufika kipindi kile wanaweza kuwa mashahidi wangu, palikuwa pachafu, vitanda
vibaya na haikustahili kabisa kuishi timu ya taifa.
Utasema hakukuwa na wadhamini, kweli. Lakini
haikuwa rahisi kwa shirika lolote kukubali kutoa fedha zake katika Fat yenye
migogoro rundo kama ile ya Ndolanga. Fat iliyokuwa na makomandoo hata kuliko
Yanga na Simba.
Fat ambayo viongozi waligeuza kama mali yao,
walifanya wanavyotaka na hapo ndipo kipindi Tanzania ilipoyumba zaidi
kimichezo. Naweza kusema kifo cha soka ya Tanzania rasmi kilianzia wakati wa
Fat hiyo ambayo ilikuwa ni ya kibabe, isiyosikiliza watu, isiyojali maendeleo
na haikuwa na lolote la kujivunia hadi leo hii.
Nishani ambayo TFF walimtuza Ndolanga,
angalau wangewapa baadhi ya wachezaji wa Taifa Stars iliyojaa shida wakati ule
kama akina Salvatory Edward, Edibily Lunyamila, Manyika Peter na wengine.
Bado naona nishani hiyo, angalau ingepewa Kampuni
ya Bin Slum Tyres ambayo misimu miwili iliyopita ilikuwa kampuni inayodhamini
Coastal Union iliyopanda daraja.
Msimu uliopita, kampuni hiyo ikazidhamini
timu tatu za mikoani ambazo ni Mbeya City, Stand United na Ndanda FC, mbili
ndiyo zikiwa zimepanda daraja. Angalia mfanyabiashara huyo alivyoonyesha
mapenzi makubwa katika mchezo wa soka.
Ingekuwa suala la faida, basi angekimbilia
Simba, Yanga au Azam FC. Lakini ameonyesha pamoja na biashara, anajali soka
kweli kwa mapenzi, kazidhamini timu changa tena za mikoani. Ndolanga amesaidia
nini? Ameipa Tanzania kipi cha kumkumbuka zaidi ya yale mahojiano yake na
Maulidi Kitenge?
Sasa bado pia najiuliza, huyu Rutahyuga
anajivunia kipi hasa kuwa mwanafunzi wa Ndolanga? Ninatafakari, halafu nitarudi
tena.
Saleh umesema kweli ni bora angepewa nishani mjomba wako 'mfungwa' Ndumbarooo! kwa maana amejaribu kupingana waziwazi na malinzi na rafikiye wambura.
ReplyDeleteTuache majungu, hata Yesu au Mtume Muhamad hawakukubalika kwa watu wote!! Lazima tukubali akina Ndolanga ni foundation ya akina Tenga!! Sijaona hoja zaidi ya mambo yako binafsi na Rutahyuga, tutajuaje kama mnagombania demu!! Wanaandika wengi, kwanini utishiwe wewe!!?
ReplyDelete