July 24, 2015


Na Saleh Ally
BENCHI la ufundi la Simba limeanza kazi, kwa maana ya muonekano kila mmoja ameona kwamba ni makocha waliopania kuleta mabadiliko katika kikosi hicho.


Uongozi wa Simba, nao unaonekana umepania kuleta mabadiliko ili kukabiliana na ushindani mkubwa wa msimu ujao ambao unaonekana wala hauhitaji kumulikwa maana kila timu inajiandaa vilivyo kuanzia kwenye usajili.

Wakati hayo yanaendelea, Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr raia wa Uingereza, amependekeza kusajiliwa kwa kipa mwingine mkongwe katika kikosi hicho.

Inawezekana hilo ni wazo la Kerr, lakini inawezekana ni wazo kutoka kwa mtaalam wa makipa ambaye ni kocha mpya wa Simba. Huyu ni Iddi Salim ambaye amejiunga na Simba akitokea AFC Leopards ya Kenya. Pia amewahi kuwa Kocha wa Makipa wa Gor Mahia na Harambee Stars.

Kerr na Iddi, wote wawili ni makocha au wataalam wa kazi yao. Ndiyo maana wamependekeza kusajili kwa kipa mwingine licha ya Simba kuwa na makipa watatu wenye uwezo wa kudaka katika michuano migumu kama ya Ligi Kuu Bara.

Achana na makinda wawili ambao mara nyingi wamekuwa katika mazoezi ya kikosi cha kwanza cha Simba, yaani David Kisu na Dennis Richard, Simba ina makipa wengine watatu.

Kwanza ni mkongwe Ivo Mapunda, kinda ambaye ameshaonyesha uwezo wake, Peter Manyika pia ilisajili kipa mpya Mohammed Abrahman Mohammed ambaye anatokea JKU ya Zanzibar akaonekana kwenye vyombo vya habari akisaini mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, nafikiri unakumbuka.


Simba tayari imekubaliana na wazo la Kerr na benchi lake la ufundi, imeingia katika mazungumzo na kipa Boniface Oluoch kutoka Gor Mahia. Hakika kipa huyo ni kati ya makipa bomba kabisa.

Pamoja na uzuri wa Oluoch, najaribu kujiuliza mustakabali wa kipa Manyika ambaye msimu uliopita, Simba ilimpa nafasi ya mechi zaidi ya sita na akaonyesha kwamba ni mmoja wa makipa bora wa baadaye.

Takribani mechi tatu zikiwemo zile za Mtibwa Sugar na Prisons, Manyika alifanya makosa yaliyoiponza Simba kupoteza pointi mbili kutokana na kulazimishwa sare.
Huenda msimu huu, Manyika angekuwa anatakiwa kuilipa Simba kutokana na makosa yake yale ya kitoto aliyoyafanya. Hakuna ubishi, ilikuwa ni lazima afanye vile ili aweze kukua!

Sasa Simba ina makovu ya makosa yake, lakini ajabu inakuwa na makipa wawili wakongwe juu yake, kama kweli itamsajili Oluoch. Maana yake, Manyika anashuka kutoka kipa wa pili hadi wa tatu. Nafasi yake ya kucheza katika mechi za Ligi Kuu Bara itateremka kwa asilimia 80, jambo ambalo halina ubishi litamrudisha nyuma kwa mara nyingine.

Kwa kukosa nafasi ya kucheza kwa asilimia 80, Simba isimtegemee Manyika kukua kwa kasi kama ambavyo alifanya msimu uliopita. Miaka mingine miwili ijayo, huenda Manyika akaendelea kubaki yuleyule wa siku zote.

Niliona isingekuwa sahihi Simba kukimbilia kusajili kipa mpya kwa kuwa kocha tu amesema. Kweli ni mtaalamu, lakini anaweza kushauriwa.

Mambo mawili yangefanyika awali, moja ni kumueleza kocha huyo mpya Simba ilikopita na Manyika na safari yake ilivyokuwa, pia malengo yao kwa kijana huyo. Pia ikarudi kwa Manyika na kumueleza kilichotokea, hivyo apambane asiwaangushe viongozi, asiwaangushe mashabiki na wanachama wa Simba, pia asijimalize kama atashindwa kuitumia nafasi hiyo.

Halafu jambo la mwisho, Kerr tena akimtumia mtaalamu wa makipa kama Iddi Pazi wakafanya kazi ya kuboresha zaidi kiwango cha Manyika kwa kuwa kipaji cha soka katika nafasi hiyo, kimo ndani ya damu yake.

Sasa anachohitaji ni mafunzo bora ya ukipa. Lazima tukubali, makipa wa Tanzania wanaweza kubaki na viwango vilevile kwa kuwa hawana walimu wenye elimu ya juu na ya kisasa kwa upande wa makipa.

Kerr anaweza kuhitaji kipa sasa, kwa kuwa anaangalia mafanikio yake ya haraka ndiyo maana anasisitiza ‘readymade’, lakini bado Manyika anaweza kumsaidia yeye na akiondoka, atabaki kuendelea kuisaidia Simba.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic