MWASHIUYA |
Na
Saleh Ally
NILIPATA
kurudia mara kadhaa kupitia king’amuzi kuangalia mara nyingine tena na tena bao
ambalo alifunga kinda Geofrey Mwashiuya wakati Yanga ikipambana na Telecom ya
Djibouti.
Kila
binadamu ana nafsi isemayo ukweli, unaweza kudanganya au kukataa kama utaipuuza
tu. Baada ya kuliangalia bao hilo kwa kiasi nilichoona nimeridhika, nikatamka
“bonge la bao.”
Hakika
lilikuwa ni bonge la bao, kwani Mwashiuya alifunga baada ya kuwatoka mabeki
wawili kwa kasi kubwa lakini kabla alimzidi mmoja mbio akitokea pembeni,
akaingia ndani ya 18 na kufunga.
Kabla
ya kufunga, utaona anabadilisha mguu na kupiga shuti na mwingine. Vitu ambavyo
angeweza kufanya mchezaji nyota kabisa na tegemeo huenda kama Kpah Sherman,
Amissi Tambwe ambao kati yao, sijawahi kuona akifunga bao kama hilo.
Bao
la Mwashiuya limejaa mambo mengi ambayo anaweza kuwa nayo mchezaji
aliyefundishwa kwenye akademi akapikika kweli kufikia hapo.
Bado
niliona bao hilo limejaa hali ya kujiamini isiyo ya kawaida ambayo angeweza
kuifanya mchezaji aliyeshiriki michuano kama ya Kagame mara mbili au tatu kabla
ya kufikia kujiamini alivyofanya bwana mdogo huyo ambaye hata Ligi Kuu Bara
hajawahi kucheza zaidi ya Ligi Daraja la Kwanza, tena akiwa na timu ya Kimondo
ambayo hata daraja haikupanda!
Achana
na bao, angalia krosi zake tatu. Moja aliitumia Malimi Busungu kufunga bao,
moja akakosa na nyingine pia haikutumika vizuri. Zote zilikuwa na macho na
utengenezaji wake hadi kufikia kuwa krosi, inaonekana kuna ubunifu mkubwa wa
kinda huyo.
Jibu
sahihi nililolipata ni kwamba, Mwashiuya ni kati ya wachezaji wenye vipaji vya
juu kabisa ambaye Tanzania imempata baada ya Mbwana Samatta ambaye sasa yuko DR
Congo akiichezea TP Mazembe.
Utaona
mambo kadhaa wanalingana, kwanza kujiamini, uchezaji wa kasi na utumiaji akili,
lakini hata kabla ya ligi kuu, tayari anaonyesha uwezo mkubwa kimataifa kama
ambavyo Samatta ambaye hakuwa na uzoefu mkubwa lakini akawapa shughuli Mazembe
hadi wakaamua kumsajili.
Lengo
hapa si kumvimbisha kichwa Mwashiuya. Mara nyingi nimekuwa nikiwasikia
mashabiki wa soka wakisema wachezaji wanaharibiwa kwa kuvimbishwa vichwa na
vyombo vya habari.
Mimi
ninafanya kazi yangu kuelezea nilichokiona na nini cha kufanya. Kama kweli Mwashiuya
‘atakufa’ kwa mimi kueleza hali halisi, basi hilo ni tatizo lake.
Nichachoona
cha msingi hasa ni kamati za usajili za klabu kurejea na kukaa chini ili zione
kama zinaweza zikatumia nguvu nyingi kurejea mikoani au katika timu za daraja
la kwanza na kwingineko kuwaangalia vijana wetu kwa kuwa inaonekana kuna kina
Samatta na Mwashiuya wengi sana, sema mmekuwa mkikimbilia kwenye usajili wa
kusikika sana na kuwafurahisha mashabiki wengi.
Kusajili
wageni si jambo baya, lakini lazima tukubaliane, Tanzania si nchi ya
kumpapatikia mchezaji kama Michael Olunga wakati tuna wengi sana wenye uwezo
maradufu na bora kuliko wake.
Kamati
za usajili, ziwe ni zile zinazoamini kuwa Tanzania ina vipaji vingi na kuwe na
sababu ya kuwatafuta kwa kupanga utaratibu bora kabisa wa kuwafikia. Tena
vizuri kuwe na programu ya muda mfupi na mrefu.
Kama
Samatta alipatikana, leo anakuja Mwashiuya, lazima wapo wa zaidi yao, chini yao
au wanaolingana nao na bado wanaweza kuzisaidia timu zetu na baadaye timu za taifa.
Tafadhali,
tuachane na imani kuwa vipaji bora kwa maana ya wafungaji na viungo, vinapatikana
katika nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda na kwingineko. Vijana wapo wengi,
vizuri muwafuate au wafuatilieni.
0 COMMENTS:
Post a Comment