Nahodha wa
Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, ametamka wazi kuwa wachezaji wenzake wa kikosi
hicho walikuwa wakigombania kupiga penalti katika mchezo wa Kombe la Kagame,
juzi Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar dhidi ya Telecom ya Djibouti.
Katika
mchezo huo ambao Yanga ilishinda kwa mabao 3-0, wachezaji wawili wa timu hiyo
Amissi Tambwe na Simon Msuva walikosa penalti katika dakika ya 39 na 44.
Cannavaro
amesema yeye ndiye mpigaji mkuu wa penalti wa timu hiyo lakini baada ya kukosa
katika mchezo dhidi ya Gor Mahia, ndipo aliamua kujiweka pembeni katika mechi
ya Telecom kwa kuwa wawili hao walikuwa wakitaka kupiga.
“Nilipokosa
katika mechi ya Gor Mahia, kocha akaamua kutupa mazoezi ya penalti kabla ya
mchezo dhidi ya Telecom, kila aliyepiga alionekana kuwa vizuri lakini mwisho wa
siku ni kama ulivyoona.
“Siwezi
kuwalaumu kwa kuwa penalti huwa hazina ufundi, hata wachezaji maarufu duniani
wanakosa,” alisema Cannavaro.
Upande wa
Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Mkwasa alisema hajui kilichotokea mpaka
wachezaji wake wakakosa penalti hizo licha ya kuwa walifanya vizuri katika
mazoezi.
Akizungumzia
hali hiyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, alisema yeye mwenyewe
hajui kwa nini walikosa wakati mazoezini walifanya vizuri zoezi hilo.
0 COMMENTS:
Post a Comment