Na Saleh Ally
NDIYO maana mara nyingi nimekuwa nikisisitiza
sipendi mambo mengi yanayohusiana na siasa kwa kuwa yamejaa unafiki, uongo na
uzandiki.
Watu wengi wapo kwenye siasa kwa ajili
ya kujitumikia wao, wachache sana wamekuwa wapo pale kwa ajili ya kuwatumikia
wananchi ambao ndiyo wanakuwa mabosi wao.
Kesho, Chama Cha Mapinduzi (CCM),
kitakuwa katika mchakato mkubwa kumsaka mgombea wake wa urais mjini Dodoma.
Hofu imejaa, wapo wanaoamini wanaonewa,
wapo wanaosubiri kupendelewa, wapo wanaojiandaa kwa lawama lakini siku ya
mwisho Wana-CCM ndiyo wataamua wanamtaka nani.
Uchaguzi wa kitu ni haki kupitia kura
na ili kuepusha hofu na kujenga umoja, basi lazima kuwe na haki katika zoezi
zima.
Haki inaondoa mengi yakiwemo ya
kutoaminiana na kuua upendo. Huenda Coastal Union wanaweza kuwa kati ya
waliofanya uchaguzi wao kwa kuangalia matakwa ya wachache na si wote.
Uchaguzi wao uliofanyika wiki
iliyopita, ulijaa mizengwe kupitiliza na unaweza kusema mambo mengine yalikuwa
kichefuchefu.
Eti viongozi wote walio kwenye uongozi
wa Coastal Union walipita bila kupingwa baada ya wanachama wengine kuzuiwa
kuingia ukumbini kwa madai hawakuwa wamepewa kadi.
Awali kupitia usimamizi wa Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), waliwaeleza wanachama wenye kadi na wale wenye risiti
za benki wakiwa wamesajiliwa kwenye klabu pia watapiga kura kwa kuwa tayari ni
wanachama halali.
Baadaye wakiwa ukumbini utaratibu
ukabadilika, maelezo yakawa tofauti na wale waliokuwa wamelipia benki kabla ya
kupata kadi wakatolewa nje na baadhi yao walikuwa ni wagombea, hivyo
kusababisha hata idadi ya wagombea kupungua na wajumbe wote wakapita bila
kupingwa kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine. Ni sawa na kubandika picha juu
ya nyingine.
Hofu ya Wana-CCM ni kukosa haki, hali
inayoweza kujenga chuki baadaye. Ndiyo maana kila mmoja yupo macho, fitna
zinaendelea na kadhalika.
Coastal pia wamelifanya hilo tena
waziwazi na baadhi wakaonekana kufurahia lakini wakasahau klabu yao imekuwa na
migogoro miaka nenda rudi na inatakiwa kuwa na umoja wa wote ili kuirudisha
kwenye hadhi yake ya juu kama moja ya klabu kongwe zilizowahi kuwa na
mafanikio.
Coastal ndani yake tayari kuna ubaguzi,
walishaanza kuitana ‘Waarabu na sisi’. Jambo ambalo nalo ni tatizo kubwa sana
na kama likiendelea kupewa upenyo zaidi linaweza kuchangia kuleta shida kubwa.
Sitaki kusema uchaguzi urudiwe, lakini
nataka kuwakumbusha Coastal Union kwamba fitna za uoga wa kuepusha baadhi
kutokuwa viongozi zimekuwa kubwa kuliko uwezo wa kupigania maendeleo katika
klabu hiyo ambayo inakwenda kwa mwendo wa kusua licha ya ukubwa wake.
Inawezekana Coastal wamesahau kwamba
msimu ujao umoja wao unahitajika zaidi kuliko wakati mwingine kwa kuwa
wapinzani wao wakubwa African Sports ‘Wana Kimanumanu’ wamerejea Ligi Kuu Bara
na itakuwa kazi kubwa kwao waanze kuchomoza ndani ya Tanga kwanza.
Inawezekana wapo watakaopinga kila
nilichoandika katika makala haya. Lengo langu si kuwatenga zaidi Coastal Union,
badala yake kuwakumbusha mambo mawili tu.
Kwanza, ni hilo la kuwa waliufanya
uchaguzi wao kutokuwa wa haki, kubagua watu, kuingiza viongozi madarakani
utafikiri Tanzania ya chama kimoja cha siasa, ile ya chagua mgombea au kivuli,
kitu ambacho hakiwezi kuwa sahihi hata kidogo.
Kitu cha pili ni kwa kila upande wa
Coastal Union, nimesikia tayari ambao hawakutendewa haki wamepinga matokeo
hayo, ninaona wana haki.
Pamoja na hivyo, niwakumbushe umuhimu
wa maisha ya klabu yao. Hivyo ikiwezekana wasamehe, waungane na walioshinda
ingawa kimagumashi, waipiganie Coastal kupata maendeleo. Wale walioshinda, pia
wawapokee.
Nina maanisha hivi, makundi ndani ya
Coastal yavunjwe na upendo uwe sehemu ya muongozo ili kuianzisha Coastal Union
moja na mpya ili mpira uchezwe uwanjani waungwana. Eehh!
0 COMMENTS:
Post a Comment