Na Saleh Ally
BAADA ya Yanga kupoteza mchezo wake wa
kwanza wa michuano ya Kombe la Kagame dhidi ya Gor Mahia, yanaweza yakasikika
mengi sana yakiwemo ya kiufundi lakini mengi yanaweza kuwa ya kishabiki.
Lakini ukiangalia namna ambavyo Yanga
walipoteza mchezo huo, lawama zote zinaweza kumuangukia Donald Ngoma ambaye
alilambwa kadi nyekundu katika dakika ya 24 baada ya kumsukuma beki wa Gor
Mahia.
Hakika Ngoma alipaswa kuwa mvumilivu,
kutokuwa hivyo kumemfanya aiangushe Yanga. Lakini nilipotazama lile tukio
nilijiuliza mara mbili, kwamba ningekuwa mimi ningeweza kuvumilia?
Maana
yule beki alisimama makusudi juu ya mguu wa Ngoma. Kweli uvumilivu ni muhimu
sana. Je, Ngoma angeweza kuendelea kumvumilia aendelee kubaki juu ya mguu wake
baada ya kumkanyaga kwa makusudi baada ya kuwa wameanguka ili aiokoe Yanga?
Sijui!
Lakini utamlaumu Ngoma, lakini unakumbuka
jinsi nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alivyotia mbwembwe na kuipoteza penalti
muhimu? Huo ulikuwa wakati wake wa kufuta makosa ya Ngoma.
Utagundua kilichotokea ni mambo ya soka lakini
kuna mengi ya kujifunza kuanzia kwa Ngoma, Cannavaro na wengine walioshiriki
mchezo huo. Yanga bado ina nafasi kubwa ya kuendelea kufanya vizuri na
ikiwezekana kutwaa ubingwa.
Kikubwa nilichokiona mimi katika mechi hiyo
haikuwa Ngoma wala Cannavaro kwa kuwa nilikuwa nikiiangalia Yanga iliyosajili
kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga
inataka kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Imechoka kuishia
hatua za awali, lakini kuna kosa limefanyika na lisipofanyiwa kazi, hakika
watalia.
Namba sita, au kiungo mkabaji. Waingereza
wanamuita hub au roho ya timu. Yanga bado haina mchezaji sahihi kwa asilimia 80
au zaidi katika nafasi hiyo.
Mbuyu Twite kwa nafasi hiyo, anaweza kucheza
lakini bado si sahihi. Salum Telela kweli ana uwezo, lakini uchezaji wake
umekuwa ni maji kupwa, maji kujaa.
Si
mchezaji ambaye anaweza kuifanya kazi yake kwa ufasaha. Tokea ameondoka
Athumani Iddi ‘Chuji’ ambaye alifanya vema, bado Yanga haijapata mchezaji
sahihi wa nafasi hiyo.
Hata baada ya kutolewa kwa Ngoma, kama
ingekuwa na mchezaji sahihi katika namba sita, basi yeye ndiye angepewa nafasi
ya kuendesha timu. Lakini juzi ilikuwa vigumu kwa kuwa Twite angalau kidogo
kwenye kulinda, si kutembeza timu kwenda mbele.
Pia
kwenye ukabaji, kama unakutana na wachezaji wenye kasi sana kama ile ya Mbwana
Samatta, ambao ndiyo aina ya wachezaji wengi walio katika Ligi ya Mabingwa
Afrika, Twite anaonekana kuwa na upungufu mwingi na mfano mzuri ni bao la pili
walilofungwa Yanga na Michael Olunga.
Twite alikuwa karibu, lakini baada ya Olunga
kutembea mbele ya Kelvin Yondani, akawa hana tena msaada.
Wakati Yanga inaendelea kumkuza Said Juma
‘Makapu’ ambaye nina hakika akiendeleza anachofanya sasa atakuwa bora au
wakiendelea kumpa nafasi Telela, bado wanastahili kusajili kiungo namba sita wa
ukweli, yule ambaye atawachezesha na kuwalinda hasa katika michuano ya
kimataifa.
Kama
watakuwa na namba sita ambaye ana upungufu mwingi kama huo nilioutaja, basi
hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itaendelea kuwa hadithi tu kwa
Yanga kwa kuwa wana makali ya kuweza kung’ata, lakini hawana uwezo wa kujilinda
wasing’atwe.
Huenda kabla ya kwenda sehemu nyingine
kutafuta kiungo, basi michuano ya Cecafa kupitia timu kama APR, Gor Mahia,
Shandy na nyinginezo zinaweza kuisaidia Yanga kupata kiungo sahihi kwa ajili ya
kazi hiyo.







0 COMMENTS:
Post a Comment