July 20, 2015


Na Saleh Ally
MAPEMA kabisa, utamu wa michuano ya Kombe la Kagame umeanza kuonekana. Tumeanza kuona kwamba hata timu zilizoonekana hazitafanya lolote, zinaweza kuwa na upinzani mkubwa.


 KMKM walioonekana hawatakuwa na lolote, wameanza na ushindi, Yanga walioonekana wataitandika kila timu, wameanza na kipigo.

 Al Shandy ya Sudan ambayo ilionyesha soka safi na la kuvutia, imeishia kupokea kipigo katika mechi yake ya kwanza dhidi ya APR ya Rwanda ambayo katika mechi ya kwanza, haikuwa katika kiwango chake cha juu kama timu, isipokuwa wachezaji kuonyesha uwezo wao binafsi.

 Kila kitu kimeanza tofauti na ilivyokuwa ikionekana itakuwa kabla haijaanza. Huo ndiyo mchezo wa soka, ndiyo maana unapendwa kuliko mwingine wowote kwa kuwa hauna majibu au matokeo mgando. Yanabadilika wakati wowote.

 Wakati michuano hiyo inaendelea, kila mchezaji angependa kujiuza kwa maana ya kupata soko zaidi, iwe katika timu zinazoshiriki michuano hiyo au nje ya hapo.

Juhudi katika kazi, maana yake upate mafanikio. Mafanikio maana yake ni kupata maslahi zaidi. Runinga maarufu ya masuala ya michezo barani Afrika, inaonyesha michuano hiyo moja kwa moja.

Kabla sijaelezea faida zake, kidogo ngoja nieleze haya kuhusiana na watangazaji wengi wa runinga hiyo ambayo naona ina faida kubwa ya kuwauza wachezaji wa ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa inaonekana katika eneo kubwa la Bara la Afrika na kwingineko duniani.

 Asilimia kubwa ya watangazaji wake, hata watu wanaoshika kamera wanatokea nchini Kenya. Sasa kiasi fulani walionyesha ushabiki wa waziwazi wakati Yanga ikipambana na Gor Mahia. Baadhi yao hata makosa ya wazi ya wachezaji wa timu hiyo ya Kenya, walikaa kimya bila ya kuyazungumzia, lakini waliyofanya wachezaji wa Yanga, yakazungumziwa.

Nawakumbusha, michuano hii inachezwa Tanzania. Hapa kuna vyombo vingi vya habari kuliko kwao. Ikiwa ni suala la kukiuka weledi, basi ubaya utawaangukia wao. Wafuate weledi kwa maana ya kuusaidia ukanda wetu, ushabiki upungue.

Nikirudi kwenye faida, timu tatu za Tanzania zinazoshiriki michuano hiyo yaani Yanga, Azam FC na KMKM zina nafasi ya kufanya vema na pia kupata faida ya wachezaji wake kuonekana.

Hali inavyoonekana, timu za Tanzania ndizo zinazotaka wachezaji kwa ajili ya kuwasajili kupitia michuano hiyo. Si Jambo baya, lakini tujiulize, kwani wachezaji wa Tanzania hawataki kusajiliwa Sudan, Kenya, Rwanda au kwingineko barani Afrika au Ulaya?

 Sasa vipi Watanzania waangalie kununua tu bila ya kuuza? Kama kweli soka ni biashara, sasa vipi wao wanafanya biashara ya kununua pekee bila ya kuuza kwa faida ili kuthibitisha soka sasa ni biashara?

 SuperSport ina nafasi ya kuwafikishia ujumbe mawakala katika nchi rundo za Afrika kuhusiana na michuano hiyo. Vizuri kama juhudi kwa wachezaji 60 kutoka wachezaji wanaocheza katika timu za Tanzania ikawa ni nguzo kwa maana mbili.

 Moja ni kuzisaidia timu zao kubeba ubingwa, pili ni kukuza soko lao na kupata nafasi ya kwenda mbali zaidi. Lazima wachezaji wajue, kuwa na wachezaji wengi nje ya nchi ni sehemu ya maendeleo kisoka.

Kucheza nje ya nchi yako, hata kama itakuwa jirani ni sehemu ya kujifunza. Inaleta mabadiliko na tabia ya kuwa mshindani. Hivyo lazima wapambane na kujiuza kwa maana ya kusaka maendeleo zaidi.

 Kununua katika michuano hiyo si vibaya, lakini ili kuonyesha tumepiga hatua kiuchezaji. Basi vizuri pia tukauza tena ikiwezekana nje ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kuwa michuano hiyo inafuatiliwa.











0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic